MTUMWA NI NANI?- SEHEMU YA TATU - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Friday, November 9, 2018

MTUMWA NI NANI?- SEHEMU YA TATU


Bwana Yesu asifiwe mpendwa katika Bwana! Ninakusalimu na nina hakika unaendelea vyema na kazi zako za kila siku, imempendeza Mungu wakati huu tujifunze neno lake kwa ajili ya kutubadili kumbuka ni neno la Mungu linatuletea mabadiliko tunayoyahitaji maishani mwetu!

Ninamuomba Mungu Baba katika Jina la Yesu Kristo akupatie ufunuo wa neno la leo, Neno la Mungu lililoleta ufunuo ndio lenye mabadiliko halisi, wale ambao wapo makini sana ndio wanaofunuliwa na kila ufunuo unaopatiwa hakikisha unachukua jukumu la kuufanyia kazi

Tulipoishia ....

Zaidi ya yote tambua kama ungekuwa mtumwa Mungu asingeimimina Roho yake ndani yako, unaanza kukua na kuwa mwana baada ya kubatizwa kwa moto yaani Roho Mtakatifu Wagalatia 4:6-7 "Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa mwanawe mioyoni mwetu, aliye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu

Kama hukujifunza nasi somo hili la mtumwa ni nani sehemu ya pili jana unaweza Kubofya hapa kujifunza pamoja nasi!

Tunaendelea....

Juzi na jana tulikuwa tunaweka msingi wa neno mtumwa ni nani, na kama nilivyosema kila mtu aliyempokea Yesu Kristo siyo mtumwa bali ni mtu huru na uhuru huo ameupata ndani ya Yesu Kristo Bwana na mwokozi wa maisha yetu, hivyo siyo sahihi kuitwa mtumwa wa Kristo kwa sababu mtumwa ni mtu asiyefahamu bwana wake anafanya nini, ni mtu asiye na haki, ni mtu asiye na urithi kwa bwana wake

Leo pia ninaendelea kuweka msingi wa mtumwa ni nani? kabla ya kuanza somo hili na kujifunza aina mbalimbali za utumwa na tabia za utumwa na yapi ni madhara ya utumwa kwa binadamu yeyote yule 

Wokovu unatuweka katika sehemu moja na Bwana Yesu Kristo, kile alichokifanya anasema nasi tutafanya tena na zaidi kama tukimwamini na kulishika neno lake, Yoh 14:12 "Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba

Kama kumwamini Yesu Kristo kunatuwezesha kufanya kila alichokifanya na zaidi ina maana sisi siyo watumwa bali ni watu huru ndani yake, mtu asiyeamini ndiye ambaye hayupo huru kwa maana nyingine ni mtumwa wa kutokuamini, na usipoamini vitu havitokei na tunataka kuishi maisha ya vitu kutokea, sehemu nyingine Mtume Paulo akasema mtu asiyeamini atakaula mboga yaani vitu dhaifu, hivyo imani inamfanya kila anayeamini kula kile anachokitaka, kuona anachokitaka na kuishi anachokitaka

Lakini ni kazi gani ambazo Yesu Kristo alizifanya na zaidi? haitoshi kujua utafanya zaidi yake kwa imani bila kujua alifanya nini Mdo 10:38 "Habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huku na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye

Ni dhahiri kazi ya Yesu wa Nazareti ilikuwa ni kuihubiri Injili ambayo ilipelekea watu waliovunjika moyo kugangwa, kuwaweka huru mateka na kuwafungua waliofungwa hii iliambatana na uponyaji, kufunguliwa na ishara na maajabu, hivyo sehemu yeyote ambayo hakuna Injili yenye kusababisha mambo haya bado hapajafikia kiwango cha kazi ya Yesu wa Nazareti

Kama unafikiri wewe ni mtumwa angali umeokoka hata yule uliyempokea ni mtumwa, kwa sababu katika kukiri wokovu ni lazima umkiri Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako anayeingia ndani ya moyo wako ni Yesu Kristo, kama Yesu aliwahi kujiita mtumwa na wewe jiite mtumwa, siwezi kamwe kujiita mtumwa kwa sababu ninajua thamani yangu ndani ya Yesu

Utumwa huambatana na roho ya woga ndio maana neno usiogope limeandikwa mara 365 katika Biblia kila ukiamka Mungu anakuambia hauna haja ya kuogopa 2Timo 1:7 "Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi, woga ni kwa watumwa hofu ni kwa walio huru kwa sababu hofu imeambatana na heshima, adabu na unyenyekevu

Wokovu unatufananisha na Yesu Kristo unatufanya tukae pamoja naye tena mtu aliyeokoka angali anaonekana yupo duniani lakini haishi hapa yupo juu mawinguni mbali na kila mamlaka, ufalme, nguvu na utawala Waefeso 1:20 "Alilolitenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka katika mkono wake wa kulia katika ulimwengu wa roho, juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na utawala, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ujao pia

Yesu Kristo alipoamua kuutoa uhai wake kwa ajili yetu, sisi nasi tulikufa pamoja naye na alipofufuka tulifufuka pamoja naye, unaweza usielewe hili lakini ndivyo ilivyo na ndiyo maana ukiokoka unafananishwa naye na unaweza kufanya kila alichokifanya hata na zaidi Waefeso 2:6 "Akatufufua pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu, na ndio maana tumeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, ambayo hii haikutokana na nafsi zetu, bali ni kipawa cha Mungu

Katika somo la jana niliweka msisitizo kwamba watu wanaotenda dhambi ndio watumwa, kusema uwongo ni moja ya dhambi kubwa, kwa sababu dhambi ya uwongo haifanyiki mara moja unahitaji uwongo mmoja kufunika uwongo mwingine Wagalatia 2:4 "Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulionao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani

Uhuru ninaoongelea kwa kila aliyeokoka upo ndani ya Kristo Yesu siyo kwake mwenyewe, maana nyingine ni kusema kwamba kila ambacho Yesu Kristo hawezi kukifanya haufanyi, hivyo ni uhuru wa kutimiza matakwa ya Yesu Kristo ndani yetu ndio maana wokovu ni kubadilishana nafasi kwa wanaoelewa zaidi ni kumpa Yesu nafasi yako na wewe kuichukua yake 

Ukitamka yeye kazi yake ni kuthibitisha, wokovu hauna tofauti na ndoa na ndio maana mahusiano yetu na Yesu Kristo ni ya zaidi ya mke na mume, hata namna ambavyo alilipenda kanisa ambalo ni mimi na wewe hata akautoa uhai wake Waefeso 5:25 "Enyi waume wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake, hivyo hata wanaume pia wameolewa na Yesu Kristo kwa njia ya Imani

Tutaendelea tena kesho.......!
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana