MTUMWA NI NANI?- SEHEMU YA NNE - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Sunday, November 11, 2018

MTUMWA NI NANI?- SEHEMU YA NNE


Bwana Yesu asifiwe, ninakusalimu katika Jina la Bwana Yesu Kristo huu ni mwanzo mpya wa wiki na kila wiki ina baraka zake mpya ni maombi yangu Mungu akufanikishe tena zaidi na zaidi sawa na hitaji la moyo wako katika Jina la Yesu Kristo

Tukiwa tunaelekea mwisho wa mwaka ni kipindi kizuri cha kuendelea kukuza imani zetu na kuamini kwamba bado tuna nafasi ya kupata kile tunachohitaji, kumbuka maono hunena kwa nguvu mwishoni na Mhu 7:8 inasema "Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake"

Mimi sikupi moyo inawezekana kabisa kila ulichokuwa unakitafuta mwaka huu bado hujakipata, lakini utakipata mwezi huu au mwezi ujao pambana mpaka tone la mwisho kwa sababu unafahamu fika kwamba mwenye haki anaishi kwa imani na imani halisi haijawahi kushindwa, Mungu akupatie kila unachohitaji katika Jina la Yesu Kristo

Tulipoishia..

Ukitamka yeye kazi yake ni kuthibitisha, wokovu hauna tofauti na ndoa na ndio maana mahusiano yetu na Yesu Kristo ni ya zaidi ya mke na mume, hata namna ambavyo alilipenda kanisa ambalo ni mimi na wewe hata akautoa uhai wake Waefeso 5:25 "Enyi waume wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake, hivyo hata wanaume pia wameolewa na Yesu Kristo kwa njia ya Imani 

Kama hukutengeneza nafasi ya kujifunza nasi somo lililopita la Mtumwa ni nani- sehemu ya tatu unaweza ⇒⇒⇒Kubofya hapa kujifunza nasi!

Tunaendelea...
Tumekuwa na siku tatu nzuri za kuweka msingi maana ya mtumwa ni nani, na katika somo la leo tunaanza kwa undani kuangalia kiundani na kitabia maana ya mtumwa, huenda hili ndio somo lako mwaka huu ninaomba Roho Mtakatifu akufunulie sawa sawia na ufahamu wako ili uweze kutendea kazi hiki unachojifunza hapa katika Jina la Yesu Kristo

Sifa ya kwanza Mtumwa ni mtu anayetegemea mtu mwingine kutimiza mahitaji yake, tambua ya kwamba hapa duniani umekuja peke yako na kila linalokuhusu ni jukumu lako, wakati fulani tulijifunza hata wokovu ni jukumu la mtu binafsi siyo la kikundi, familia, taasisi au chama ni wewe peke yako unahubiriwa Injili inakuingia unaokoka

Neno la Mungu linaposema nchi linamaanisha mtu mmoja, waswahili wana msemo wa jeshi la mtu mmoja huu umetolewa kwenye Biblia, changamoto yao huwa hawasemi huyo mtu mmoja yuko na nani? Ni jeshi la mtu mmoja aliye na Yesu Kristo hata kama dunia nzima leo hii ikinipinga kama nina Yesu nina uhakika wa kuishinda

Abrahamu aliambiwa na Mungu Mwanzo 12:2 "Nami nitakufanya kuwa taifa kubwa, na kukubariki na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka" hivyo kimsingi mtu ni taifa, mtu ni nchi inayotembea ni mpaka ujione namna hii ndipo unakuwa na baraka zisizo na kikomo, huna haja ya kutegemea nchi nyingine kukusaidia

Mimi ninaamini sababu kubwa ambayo inafanya nchi nyingi zisiendeleae ni kwa sababu wanategemea kusaidiwa na watu wengine, wao hawajioni kama ni nchi wanajiona masikini na hawana uwezo kumbuka Mungu anasema katika Mithali 23:7 "Maana onavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo" mpaka ujione ukisaidia wengine ndipo utakapoacha kuwa tegemezi na ombaomba

Tunapofikia hadhi ya kujiona kama nchi na siyo watu ndipo tunapoweza kukopesha mataifa mengine Kumb 15:6 "Kwani BWANA, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utatawala mataifa mengi, usitawaliwe nao

Hivyo huna haja ya kutegemea mtu kutimiza mahitaji yako, watu wengi wameishia kuambulia laana kwa sababu hiyo Yer 17:6 Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, Na moyoni mwake amemwacha BWANA

Kama kwa namna yoyote ile unategemea ndugu yako, rafiki yako kukutimizia au kukusaidia mambo fulani na siyo Mungu jua umelaaniwa na huwezi kutoka hapo ulipo mpaka utubu kwa sababu dawa ya laana ni toba, wengi wanakosa hata ajira kwa sababu wanategemea watu fulani wawasaidie na siyo Mungu ndiyo sababu hawapati na hata wakipata hawafanikiwi

Katika nyakati hizi tumekuwa na kizazi cha kulaumu serikali kwa kila kitu kama vile serikali inahusika na kutupatia mahitaji yetu, labda nikupashe habari hii serikali haijakuumba wewe kazi ya serikali ni kukutungia sheria na kuhakikisha hakuna machafuko nchini mengine yote ni jukumu lako acha kusingizia kodi kubwa na kumzuia Mungu kukubariki

Jinsi unavyoiweka akili yako katika kuangalia ubaya hata zuri likikujia huwezi kuliona tafuta mazuri na songa nayo mbele, katika kipindi hiki watu ndio wanafanikiwa vizuri, mambo ndiyo yamelegea, Mungu ndio anatumia watu na anainua vijana wenye nguvu katika kuhubiri Injili 

Tena watu wasio na kazi wanapaswa kabisa kuwajibishwa kwa kulipa kodi serikalini kulingana na neno la Mungu kwa sababu hawataki kufanya kazi Mh 12:24 "Mkono wa mwenye bidii utatawala; bali mvivu atalipishwa kodi" kama hutaki kulipa kodi ongeza bidii nchi za Afrika zinatawaliwa maana kumejaa wavivu na wanaotegemea misaada kila wakati hata kwa mambo yasiyo na msingi na maana na ndiyo maana hata baraka za Mungu zinapishana nazo

Kama ulikuwa haujui ni kwamba nyumbani kwako unalipa bili kubwa ya umeme kuliko kiwandani kwa sababu hauzalishi nyumbani hivyo unastahili kodi kubwa, kiwanda kinakuza uchumi, kinaajiri, kinazalisha hivyo mwenye nacho astahili kulipa kodi kidogo katika umeme kuliko wewe unaetumia umeme kuangalia luninga

Katika nchi za Afrika kuna siku za kuadhimisha watu waliokufa hakuna siku za maombi na toba kwa ajili ya nchi, katika hali kama hii ni vigumu sana kuona baraka za Mungu zikitiririka kwa wananchi, pia tambua ya kwamba jukumu la wazazi wako lilikuwa kukuleta duniani na kukulea, shukuru Mungu kama ulienda shule mengine ni jukumu lako, pambana ndio maana ukapewa akili siyo ya kuombaomba bali ni kufikiri kwa kina na kuja na majibu

                                                   Yesu ni BWANA!


Tutaendelea tena kesho.......!
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana