MTUMWA NI NANI?- SEHEMU YA SABA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, November 14, 2018

MTUMWA NI NANI?- SEHEMU YA SABA


Bwana Yesu asifiwe? Ninakusalimu katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareti nina amini kwamba ni mzima wa afya na unaendelea vyema na kazi uliyopewa na Mungu, ninazidi kumshukuru Mungu kwa ajili yako na kwa kila hatua ambayo unapiga kwenye maisha, kwa sababu siyo kwa uwezo wetu bali kwa uweza wake Bwana Yesu tunaweza kutoka kiwango hata kiwango, Mungu azidi kukubariki!

Ninakukaribisha tena kipekee katika mtandao huu kujifunza Neno la Mungu pamoja nasi, nikuhakikishie upo sehemu sahihi na haujapotea, na kwa sababu una kiu ya Neno la Mungu basi Yesu Kristo mwenyewe aliye maji ya uzima na akuhudumie katika Jina la Yesu Kristo kupitia Roho wake wa mafunuo

Tulipoishia...

Nihitimishe siku hii ya leo kwa kusema kwamba kuna mambo makuu matatu yanayomfanya Yesu Kristo aishi ndani yetu na sisi ndani yake na siku ya jana tuliangalia jambo la kwanza ambalo ni wokovu na leo tumeangalia meza ya Bwana na kesho tutaangalia neno la Mungu, afya ya kiungu ni haki yako kama umeokoka na ninakuona ukiwa na uzima katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareti, Amen!

Tambua kwamba masomo haya yako katika mtiririko unaofuatana, uanapokosa kujifunza somo moja huenda usielewe vizuri somo jingine ndiyo maana nakushauri kama hukutengeneza muda wa kujifunza nasi somo la jana la mtumwa ni nani- sehemu ya sita unaweza kuungana nasi kwa kujifunza kwa ⇒⇒⇒Kubofya hapa kusoma mwanzo hata mwisho

Tunaendelea..
Kabla sijaendelea ninaomba nikufahamishe kwamba tunabadilika viwango kupitia ufunuo wa tunaoupata kwenye Neno la Mungu, usishangae kabisa ukiwa unajifunza nasi mtumwa ni nani Roho Mtakatifu akakupatia ufunuo juu ya mafanikio kiungu, haya ni mambo ya kiroho bora niweke wazi mapema na tambua unachojifunza hapa kinakupa mwanga lakini mwanga mkubwa usiotikisika upo kwenye ufunuo utakaopewa

Hakuna mwanafunzi mbaya kama anayeelezea kila kitu kama mwalimu wake pasipo kusema alichokielewa yeye, namba moja wengi darasani huishia kufanya kazi za wengine kwa sababu hii, huwa hawana cha kuongeza baada ya kujifunza kaa chini peke yako andika ni nini spesho nilichokielewa kutoka katika hili

Kumbuka siku zote unachoongezea ndiyo chako, na ndiyo maana ni rahisi mwanafunzi kuenda mbali zaidi ya mwalimu wake, kile ulichoongezea ndicho ulichokielewa, maisha ya kiroho hakuna kukariri kuna kufunuliwa, ninachofunuliwa mimi siyo utakachofunuliwa wewe, ila utofauti wa mafunuo ulio na udhihirisho wa Neno la Mungu wafaa kwa ajili ya kujenga mwili wa Kristo 1Kor 12:7 "Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana"

Kumbuka tunaendelea na tabia ya pili ya mtumwa inayosema kama umeokoka na bado unasumbuliwa na magonjwa wewe ni mtumwa, tuliangalia siku ya kwanza kwa nini ukiokoka haupaswi kuumwa, jana tukaona kwa nini ukishiriki meza ya Bwana hupaswi kuumwa na leo tunaangalia kwa nini ukisoma Neno la Mungu hupaswi kuumwa

Kumbuka kwamba mambo haya yote matatu yanakaa ndani yetu na ndio maana tuliyaweka katika kundi moja Yohana 15:7 "Nanyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo nanyi mtatendewa" maneno ya Yesu Kristo yanapaswa kukaa ndani yetu ndipo tunapoweza kupatiwa chochote tunachotaka

Kuna tofauti ya ndani na mdomoni, wengi yamekaa mdomoni siyo ndani (moyoni) ndio maana hayana faida kwao kwa sababu hayajachanganyika na imani, pale tuu kitu kinapoingia moyoni ndipo imani huzaliwa, Injili tunayohubiriwa ni ya Yesu Kristo ila kama haijachanganywa na Imani haina faida Waebrania 4:2 "Maana ni kweli sisi nasi tumehubiriwa Habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliolisikia"

Kufaa au kutokufaa kwa neno kunatokana na imani, ninasema kwa kujiamini kwamba siwezi kamwe kuumwa kwa sababu ya neno la Imani nililojifunza, kama huamini neno kamwe haliwezi kukuletea mabadiliko yeyote yale na unapoteza muda wako, faida ya neno la Mungu ni likae ndani yetu na sio tuu kulisikia au kulisoma ukaishia hapo

Neno ni nini? 

Sehemu ya kwanza, Neno ni Yesu mwenyewe, wengi hawafahamu hili kama umeokoka halafu huamini neno jua kiufupi humwamini Yesu Kristo uliyempokea au huenda ulikuwa haujui na jua sasa, kama Neno linasema Kwa kupigwa kwake sisi tumepona, ndivyo ilivyo amini utaona likidhihirika  Yohana 1:1 "Hapo mwanzo kulikuwa na Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu, tizama tena Ufunuo 19:13 "Naye amevikwa vazi lililoloweshwa katika damu, na jina lake anaitwa, Neno la Mungu"

Kama hiyo haitoshi nikuongezee zaidi Yohana 1:14 "Naye Neno akafanyika mwili (yaani Yesu), akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, na utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli" Hata sisi ni lazima tufanyike kuwa Neno kupitia wokovu kisha Neno linatubadilisha kuwa jinsi lilivyo 

Neno la Mungu tunalila kama chakula linatutia nguvu na kutuimarisha katika kila eneo la maisha yetu, ili ubadilike zaidi hauna budi kutoka kwenye kusoma Neno uhamie kwenye kulila, ifikie sehemu unakaa unacheuwa Neno hii ndio kutafakari kwa lugha ya kiroho, unapolila Neno linageuka linakuwa ufunuo kwako Yeremia 15:16 "Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA Mungu wa majeshi"

Unapokula Neno linakuwa baraka kwako, kumbuka ya kwamba chanzo cha baraka zote ni Mungu mwenyewe yaani Neno, na magonjwa siyo baraka ndio maana hakuna mtu anayeweza kutoa ushuhuda wa magonjwa, Mithali 10:22 inasema Baraka ya BWANA hutajirisha, Wala haichanganyi huzuni nayo" hii ndio maana Neno linaleta furaha kwa sababu lina baraka

Na shangwe ya moyo wangu!

Niliwashirikisha ushuhuda wa ufunuo niliopatiwa na Roho Mtakatifu baada ya kusumbuliwa na ndoto mbaya sana na nikaomba pasipo majibu baada ya kupata ule ufunuo nilisema niligeuka nikawa "naongea kama kichaa" ule ukichaa wa kuongea pasipo kujali watu barabarani na kucheka mwenyewe ulikuwa ndio shangwe ya moyo wangu, moyo ukiwa unaongea haujali akili inasemaje, kwa sababu akili huangalia watu na mazingira, ila moyo huangalia ukweli na siri iliyofunuliwa

Maana nimeitwa kwa Jina lako!

Kila aliyeokoka ni mtoto halisi wa Mungu, kumbuka mtoto anapatiwa kila anachohitaji na mzazi wake Yohana 1:12 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio Jina lake" Ukimpokea Yesu Kristo kila kitu chako hubadilika hata sehemu unayoishi kiroho unahamishwa unaenda kukaa naye juu kabisa kwenye mawingu, huwezi kuona kwa macho ila kiroho ndivyo ilivyo

Mwaka jana niliposoma Neno likaniingia haswaa nikamwambia Anti yangu nimehama ukoo akamwambia Baba nilichokuwa nacho ni huu ufunuo, ila wao hawakuelewa ilikuwa bonge la msala, ukiokoka unaingia kiroho katika ukoo wa Yesu Kristo, ndio maana anasema amekuita kwa Jina lake

Sisi ni mungu kupitia Neno kwa sababu aliyetuita ametupatia Jina lake kama Yeye ni Mungu sisi tuliopewa hati miliki ya Jina ni mungu, Zaburi 82:6 "Mimi nasema, Ndinyi Miungu, Na wana wa Aliye juu, enyi nyote" hivyo kwa sababu tuna hata miliki ya Jina la Yesu Kristo kila alichokifanya tunaweza kufanya na zaidi kwa sharti moja tu la kumuamini Yesu Kristo, hii ni kwa sababu Jina halikuja lenyewe bali na nguvu yake, mamlaka yake na uweza wake Luka 10:19 "Tazama, nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na n'ge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru"

Sasa wewe umeokoka halafu bado unasumbuliwa na mambo ya kichawi jua bado hujaamua kusimama kwenye Neno la Mungu, ninamaanisha hili nimeshachoma moto nyumba ya mchawi ninaposhi na jioni baada ya siku moja akanitumia majeshi ya paka akidhani ataniweza nikayafurumsha na damu ya Yesu usiku wa manane

Ukweli ukijua nafasi yako hakuna kitu kitakutishia katika hii dunia kinachohusiana na uchawi, ushirikina, magonjwa, kulogwa n.k omba tuu ufunuo usiende kichwa kichwa maana utapigwa vizuri tuu na utaomba poo!

            YESU NI BWANA!
Tutaendelea tena kesho.......!
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636


No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana