MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA TANO - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, October 2, 2018

MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA TANO


Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu, nina imani ndani ya moyo wangu kwamba wewe ni mzima wa afya na unaendelea vyema na kazi zako, hata mimi pia ninaendelea vyema kwenye kazi ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazarethi

Tumekuwa na kichwa kizuri sana cha somo la "Mungu anayejificha" jana pia tuliona mfano wa hakimu na mama mjane, namna ambavyo mama mjane alivyopigania haki yake mpaka hakimu akakasirika na kumpatia, lakini pia tuliona ni kwa imani tunaweza kupokea haki zetu kutoka kwa Mungu kama hukujifunza somo la jana tafadhali unaweza ⇒⇒⇒KUBOFYA HAPA KUJIFUNZA LOTE

Tulipoishia...

Mtu mwenye hekima hapaswi kuogopa kabisa dhambi alizozifanya kama ataelewa hiyo mistari miwili bali kama alianguka atajua ni Shetani anamfanya asimrudie tena Mungu, hivyo simama na jioneshe kwamba unalifahamu neno tubu ana anza maisha mapya tena ndani ya Kristo Yesu

Tunaendelea...

Mungu ni wa ajabu ndiyo maana hatuwezi kumaliza mizungu yake, japokuwa kuna wakati Mungu hujificha kwetu lakini pia hata sisi tunaweza kujificha ndani yake na adui kamwe asiweze kutudhuru, kama umewahi kuomba maombi ya vita nina uhakika utakuwa unafahamu siri ya kujificha ndani ya damu ya Yesu Kristo haswa pale unaposhambulia kambi ya adui

Nakumbuka kuna siku tulisali maombi haya pamoja na Mchungaji na rafiki yangu lakini yeye hakujifunika na damu ya Yesu, yaliyompata anayajua mwenyewe nilimsikia akilalama nikamuuliza swali moja tu jee ulijifunika na damu ya Yesu akasema hapana nikamwambia ulikuwa unategemea nini? Hivyo kuna siri kubwa sana katika damu ya Yesu Kristo 

Kama unataka kujifunza zaidi juu ya damu ya Yesu kuna somo maalumu nililoliandaa kipindi cha nyuma unaweza kulisoma kwa ⇒⇒⇒⇒Kubofya katika linki hii

Unapojificha kwa Mungu hakikisha ya kwamba unaamini Mungu aweza kukuficha kwa sababu Mungu hapendi watu wanaomwendea kwa mawazo ya kusitasita bali wanaojiamini ndiyo maana anasema katika Zaburi 119:113 "Watu wa kusitasita nawachukia, mstari wa 117 "Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima"

Tunamwita Mungu Baba yetu kwa sababu anaweza kutupatia kila tunachohitaji, anaweza kutulinda, anaweza kutuponya na kutukomboa, mtoto mdogo huamini kwamba wazazi wake waweza kufanya jambo lolote kwa ajili yake ndiyo maana watoto huomba wazazi wao kitu chochote hata kama ni ndege wakiamini wazazi wao wanaweza kuwapatia

Hivi ndivyo tunavyopaswa kuwa kwa Mungu, tena hata zaidi ya watoto kwa sababu wazazi wa duniani kuna mambo mengi hawawezi kuwapatia watoto wao lakini Mungu kila tunachomuomba kama ni kitu sahihi kwa ajili yetu aweza kutupatia, ni suala la kuimarisha imani zetu tuu ndio linatakiwa ndipo tutakapoweza kupokea kila tunachotaka kutoka kwa Mungu

Tunajificha kwa Mungu kwa sababu anaweza kutuokoa na mitego mbalimbali pamoja na hila la adui Ibilisi, mara nyingi watu huanguka kwa sababu hawajajificha kwa Mungu hivyo adui huwatega nao hushindwa kustahimili mitego yake, dawa ya mtego ni kuutegua Mungu pekee ndiye anayetuwezesha kutegua mitego ya adui ambayo hutupeleka kwenye mauti Zaburi 69:20 "Mungu wetu ni Mungu wa wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana"

Kipindi cha nyuma kidogo kama miezi miwili iliyopita niliota ndoto fulani ya ajabu, lakini baada ya kutafuta sana maana ya ndoto ile kwenye vitabu na kuchunguza sana nikapata maana yake, ambapo kulikuwa na jaribu linalonijia na katika jaribu hilo Mungu atanipa hekima ya kutoka, ni kweli mwezi uliopita mwanzoni jaribu likaanza nikiwa napambana nalo nikakumbuka ile ndoto

Kufupisha habari ni kwamba hili jaribu lilikuwa limelenga kuniondoa kwenye ninachofanya niende kufanya kitu kingine, kuna siku nikiwa nimekaa natafakari ghafla Roho wa Mungu akanipa Idea nikaandaa waraka kwa ajili ya jaribu hilo mpaka sasa njia ambayo Shetani alikuwa anaitumia kaona haina tija kaamua kunyamaza ndiyo nikafahamu ile hekima ya kutoka niliyoambiwa ni huo waraka nilioandaa

Mungu wetu ndiye anayetuponya na adui zetu, wote tunafahamu kwamba tunaye adui mmoja ambaye ni Shetani lakini changamoto iliyopo anatumia watu wengi kukudhuru, hatumi kibaraka mmoja wanakuja wengi kwa pamoja ndiyo maana kuna haja kubwa ya kujificha kwa Mungu Zaburi 143:9 "Ee BWANA, uniponye na adui zangu; Nimekukimbilia Wewe, unifiche

Watu wengi hufikiri utumishi ni jambo rahisi kweli nakuambia siyo rahisi, nimesikia maneno mengi sana ni neema ya Mungu tuu inanifanya ninawaombea hata wanaonisema vibaya, na usifikiri wanaokusema ni watu wa mbali ni wa karibu yako sana, tena unaokaa nao na kujadiliana nao mambo mbalimbali leo utaletewa hili kesho lile kama haujajificha kwa Mungu mambo hayataenda

Jaribu kufikiri katika maisha ya kawaida unasemwa jee ukiwa unahudumia watu hali itakuwaje, kifupi Shetani hufanya kila mbinu kukurudisha nyuma, jamani kuwa mwalimu, mchungaji, mtume, nabii, mwinjilisti unahitaji moyo wa jiwe kinyume na hapo hautaweza ndiyo maana Daudi akasema Zaburi 31:20 "Utawasitiri kutoka kwenye fitina za watu, Katika maficho ya kuwapo kwako; Utawaficha katika hema Na ushindani wa ndimi

Kufichwa katika hema ni kufichwa nyumbani mwa Mungu, hivyo watu watakuwa wanakufanyia fitina lakini wewe upo nyumbani kwa Mungu unahudumia watu, nyumbani kwa Mungu ni Sayuni mji wake mtakatifu, watu wanapokutupia maneno wewe unakwenda zako Sayuni mjini kwa Mungu huna habari nao nabii Isaya aliliona hili Isaya 4:6 "Kisha kutakuwa na hema kuwa uvuli wakati wa mchana kwa sababu ya joto, na kuwa mahali pa kukimbilia na kujificha wakati wa tufani na mvua"

Hata kama mtu siyo mtumishi unapopigwa na maneno ya watu yakakukosesha amani hakuna sehemu nzuri ya kukimbilia na kuisalimisha nafsi yako kama Sayuni, jenga mazoea hayo itakusaidia sana, kuna mambo huondoka yenyewe unapokuwa Sayuni kwa Mungu Baba 

Ushindani wa ndimi, hii huwezi kushinda sasa naelewa kwa nini unaweza kusikia mtumishi mkubwa kasemwa kwa jambo fulani na akanyamaza kimya ni kwa sababu anapojibu anatengeneza nafasi ya kushambuliwa zaidi, wakati mmoja walimwandika vibaya mtumishi wa Mungu Dr. David Oyedepo na alipopelekewa gazeti lile akakataa kabisa kulisoma, walipomlazimisha akawaambia wakaliweke mapokezi wageni wakija wasome yeye hana muda wa kusoma ujinga

Hivyo njia nzuri ya kuwashinda wanaotaka kuleta majibizano ya ndimi ni kunyamaza, ni mara nyingi watu humsema mtumishi fulani vibaya ili tuu aongee ila unapokuwa kwenye maficho ya Mungu anakuepusha na kujibizana nao unakaa kimya na huduma inasonga mbele zaidi kwa utukufu wa Mungu Baba

Itaendelea tena kesho.....


Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana