MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA NNE - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, October 1, 2018

MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA NNE


Ninakusalimu katika Jina la Yesu Kristo, ninatumaini unaendelea vizuri, mimi pia ninaendelea vyema mkono wa Bwana umeendelea kunizunguka pande zote na kila mahali, hii ni siku njema ambayo Mungu ameifanya tena kwa utukufu wake mwenyewe ili tumsifu na kumtukuza

Tunaendelea na kichwa cha habari cha "Mungu anayejificha" jana tuliendelea kuona madhara ya Mungu kujificha kwenye maisha yetu kwa zaidi ya dakika moja na pia tulisema unapoona Mungu kajificha endelea kukomaa naye mpaka upate tena uso wake kama Ayubu

Kama hukupata nafasi ya kujifunza nasi somo la jana bado unayo muda wa kujifunza kwa ⇒⇒⇒Kubofya hapa kujifunza mwanzo hata mwisho

Tulipoishia....

Mungu akikuficha uso wake unakuwa mtu asie na makao duniani, watu wote wanaotangatanga na maisha yanaonekana kupishana nao ni kwa sababu Mungu amewaficha uso wake Mwanzo 4:14 " Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na makao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniuwa"

Tunaendelea...

Jana wakati ninatafakari juu ya somo hili nilikumbuka moja ya mfano wa Yesu aliowapa wanafunzi wake unajulikana kama "Mfano wa mjane na hakimu" mfano huu unaelezea kabisa juu ya somo hili kama hujawahi kuusoma au umeusahau waweza kufungua kitabu cha Luka 18:1-8 na ukausoma wote, japokuwa katika mfano huu Yesu alitumia "mungu mtu" ila mwishoni aliishia kulinganisha na Mungu Baba wa mbinguni namna anavyotujali

Katika mfano huu nimejifunza baadhi ya mambo ambayo ninafikiri ni muhimu tukashea kwa pamoja leo hii na kuweza kuelewa zaidi juu ya Mungu anayejificha na ni nini kinahitajika kufanya unapokuwa huoni uso wa Mungu kwa wakati fulani

Katika mfano huu hakimu alikuwa na sifa zifuatazo;

Luka 18:2 "Akasema, Palikuwa na hakimu katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu na mstari wa 5 "Lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima

Hamchi Mungu, maana yake alikuwa ni mtu mwenye dhambi na asiyetaka kulishika neno la Mungu, lakini pia neno la Mungu kwake lilikuwa ni upuuzi, hii ndiyo maana ya mtu ambaye hamchi Mungu na kama mtu hamchi Mungu hatakuwa na upendo ndani yake kwa sababu Mungu ni pendo, neno la Mungu na ile hofu ya Mungu ndiyo inayotengeneza pendo la Mungu ndani ya mioyo yetu

1Yoh 4:7-8 "Wapenzi, mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo

Hakimu huyu pia alikuwa hajali watu, hii ni kwa sababu hakuwa na upendo unapokosa upendo wa Mungu binadamu mwenzako waweza kumuona takataka na hapaswi hata kukusogelea, kutokujali kunamfanya mtu asitake kusikiliza shida au haja za mwenzake kwa sababu anaona hana thamani, ndiyo maana huyu hakimu hakutaka hata kumsikiliza huyu mama mjane

Jambo la tatu huyu hakimu alikataa kumpatia huyu mjane haki yake, kwa sababu tuu hajali kama unafuatilia namna mambo haya yalivyopangiliwa ni kwamba jambo moja linazaa jambo jingine lakini kikubwa kilichosababisha haya yote ni kukosa upendo wa Mungu hii ndiyo maana amri mpya Yesu aliyotuletea ni upendo tupendane sisi kwa sisi

Yohana 13:34-35 "Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi

Unapaswa kuelewa mambo haya katika mfano huo wa mama mjane na hakimu ambayo ndiyo yalimfanya Yesu atoe mfano huo kwa wanafunzi wake, ili nao wapate kuelewa kwamba kuna nyakati Mungu hukificha hivyo haupaswi hata kidogo kukata tamaa na imani yako ni lazima ipimwe ili uweze kukua viwango

Mungu hapendi uangaike kwa suala moja kwa muda mrefu, Mungu ni mpaji hutupatia kila tunachotaka na hataki kuona kamwe mtu anamwendea kwa kitu kimoja kwa muda mrefu ndiyo maana ukikomaa vya kutosha ni lazima atakujibu, wengi hawamuoni Mungu kwa sababu wanaombea suala lao siku moja wanaliacha na kukata tamaa, inakupasa kuomba bila kukoma kwa suala hilo hilo ndipo Mungu anaingilia kati

Huyu mama mjane alimuendea hakimu kwa jambo moja mara nyingi, jambo la kushangaza japokuwa huyu hakimu hakuwa hakuwa anamcha Mungu, wala anajali na alishakataa kumpa haki yake lakini bado alishawishika kumpatia kwa sababu hakukata tamaa kudai haki yake

Leo hii umeokoka kuna haki zako kwa nini unaomba mara moja na kukata tamaa, kwa nini unaumwa na unakubali, kwa nini unateswa na wachawi na unakubali? Ni muda wa kusema imetosha sasa ni lazima kila kilichopo kwenye maisha yako kisichofanana na wokovu kiondoke ili watu wamjue Mungu unayemtumikia

Jambo la pili ni kwamba upo uhakika wa kupata kila kitu unachotaka kama ukikomaa/ukipambana vya kutosha, huyu mama mjane alipata haki yake si tuu kwa imani bali kwa imani yenye fujo naam imani ya kupambana hata tone la mwisho mpaka kipatikane kinachohitajika ndio unaacha, maisha ya wokovu ni ya Imani kama huwezi kupigana vita vya imani yatakushinda na utaomba poo mapema sana kabla hata ya mchezo kufika katikati

Mwenye imani zaidi ndiyo anashinda ndiyo maana Mtume Paulo anasema katika Warumi 1:12 "Mwenye haki ataishi kwa imani" kama hakuna imani hakuna kitu utapata kwenye wokovu utaishia kuwa mshabiki wa shuhuda za watu, jamboa ambalo halipaswi kabisa kuwa fungu lako katika jina la Yesu Kristo ndiyo maana katika mfano huu tizama Yesu alichowaambia wanafunzi wake;

Luka 18:8 "Nawaambia, atawapatia haki upesi; lakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataona imani duniani? maana yake ni kwamba tunaweza kupata haki zetu zote kwa imani kama hakuna imani hata Mungu hawezi kukusaidia, unahitaji kukua kiimani ndugu yangu tena sana

Somo lingine katika mfano huu ni uvumilivu wa Mungu kwetu, utaniuliza kwa nini Yesu alisema kwamba Mungu anatuvumilia? Ni kwa sababu tunafanya dhambi kila wakati lakini changanya na dhambi hizi bado Mungu anavumilia anasema moyoni mwake nimewapa nafasi ya kutubu na kurekebisha watanirudi

Luka 18:7 "Na Mungu, Je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

 Lakini pia Mungu  ameachilia neema kubwa duniani kuliko dhambi ambazo wateule wake wanazifanya ndiyo maana anaweza kuwavumilia
Warumi 5:20-21 "Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi, ili kwamba, kama vile dhambi inavyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu

Nilipokutana na hiyo mistari miwili akili yangu ilipata chaji, maana yake ni kwamba hata ufanye dhambi kiasi gani neema ya kuokolewa bado ni kubwa kuliko dhambi ulizozifanya, hivyo ukimjia Mungu kutubu bado unasamehewa na hii ndiyo inamfanya Mungu kutuvumilia ile neema aliyoiachilia

Mtu mwenye hekima hapaswi kuogopa kabisa dhambi alizozifanya kama ataelewa hiyo mistari miwili bali kama alianguka atajua ni Shetani anamfanya asimrudie tena Mungu, hivyo simama na jioneshe kwamba unalifahamu neno tubu ana anza maisha mapya tena ndani ya Kristo Yesu

Tutaendelea tena kesho....

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

1 comment:

  1. Amina sana Dada Ubarikiwe, kama nilivyosema katika comment ya Facebook ya kwamba nabarikiwa sana na ninajifunza na kupata hamasa zaidi katika moyo Wangu.

    Nitazidi kifuatilia zaidi ili nizidi kuelewa vitu kwa njia na lugha nyepesi uitumiayo. Hakika wewe ni MWANAMKE WA THAMANI, MUNGU AKUBARIKI SANA.

    Ni Mimi Mwl. George John

    ReplyDelete

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana