SITABAKI KAMA NILIVYO! - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, September 19, 2018

SITABAKI KAMA NILIVYO!


Ninakusalimu kwa Jina lipitalo majina yote, hili ndilo Jina la Yesu Kristo Bwana na mwokozi wa maisha yetu, pekee linalostahili kuinuliwa na kupewa sifa, hii ni siku njema sana kwangu inapendeza mno na nina furaha ndani ya Bwana sijui kuhusu wewe
Kama ilivyo kawaida ya mtandao huu tunakuandalia neno la Mungu kila siku kasoro jumamosi na jumapili hata leo kuna neno kwa ajili yako, swali ni jee upo tayari kuhudumiwa? Kama upo tayari Roho Mtakatifu naye yupo tayari ndiyo maana Vodacom wanakuambia kazi ni kwako
Mambo ya kiroho hulazimishi unafanya uchaguzi kama upo tayari basi ungana nasi na kaa mkao wa kupokea Neno la uzima na Mungu akubariki sana katika Jina la Yesu Kristo

Tulipoishia......
Uwongo utakufukuza nyumbani kwa Mungu, kwa sababu Mungu siyo muongo hawezi kamwe kukaa na muongo hata kwa dakika moja ni lazima atamfukuza, kwa maana nyingine hutasitawi wala kupata kibali kwa Mungu, tambua maisha yetu tunatafuta kibali kwa Mungu, unapokuwa na kibali hakuna kitu ambacho hakifanikiwi, kumbuka ukifukuzwa nyumbani kwa BWANA utakwenda jehanamu ya moto Zaburi 101:7 "Hatakaa ndani ya nyumba yangu Mtu atendaye hila. Asemaye uwongo hatathibitika Mbele ya macho yangu
Kama hukujifunza nasi somo la jana ambalo ni moja kati ya masomo mazuri sana tuliyowahi kuyaandaa la kwa nini watu wanasema uwongo unaweza ⇒⇒⇒kubofya hapa kulisoma lote!

Tunaendelea.....
Leo sitaendelea na mada ya chunga sana ulimi wako kwa sababu maalumu labda kesho tutaendelea leo nimekumbuka moja ya somo tulilowahi kuliandaa kipindi cha nyuma sana lililokuwa na kichwa cha habari "Sitabaki kama nilivyo"

Lilikuwa na sehemu tatu na hata leo hii ukilisoma utaona namna ya uandishi ya kipindi hicho na sasa ulivyo tofauti kabisa, Mungu ni mwema sana kama angekuwa hatutoi kutoka kiwango hata kiwango kwa kweli tusingemuamini

Kinachonifanya niweke somo hili ni kwamba lilikuwa na ushuhuda mkubwa sana, kuna watu watatu katika kampuni moja walifanya makosa yanayostahili kufukuzwa kazi na walishaandikiwa barua za kufukuzwa kazi na zimeshasainiwa kabisa, bosi wao jioni alikuwa anasubiri wakiwa wanatoka wapatiwe barua zao na kibarua chao kiishie hapo

Shuhuda zinatujenga sana ndio maana leo nashea hii, zipo nyingine ila nimeanza na hii leo, tuendelee jioni ilipofika karibia wanatoka kazini bosi wao akaingia facebook na somo la kwanza kabisa lilikuwa ni hili la "Sitabaki kama nilivyo" akalisoma lote likaingia kwenye moyo wake sana kisha ndani yake akasikia sauti inamwambia piga hiyo namba ya simu hapo chini

Alitii akanipigia simu na bahati ofisini kwao na kwangu haikuwa mbali akaniomba sana niende ikabidi niache shughuli zangu nikaenda, ndipo aliponielezea huo mkasa baada ya hapo wakaitwa wale watu watatu, walipokuja niliwahoji wakakubali wametenda kosa mmoja wao alikuwa ni Mwislamu cha kushangaza ni hiki;

Wote waliokoka na kumkiri Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao pamoja na yule bosi wao, pale pale bosi wao aliwasamehe na hawakufukuzwa tena kazi, wakaambiwa wasirudie tena kampuni yenyewe ni ya Vodacom makao makuu

Hivi ndivyo Mungu anavyofanya kazi na masomo haya tunayoyaandaa, yamegeuka baraka kwa watu wengi sana, kumbuka hawa waliokuwa wanafukuzwa kazi wana familia zao jee zingeishije, wangekula nini? Ndiyo maana nazidi kumshukuru Mungu kwa kila hatua tunayopiga
Mwisho wa shuhuda....!

Ni vitu ambavyo hatuna vinatufanya tuweze kufahamu vile ambavyo tunavyo, kila hatua ambayo tunapitia inatuandaa kwa ajili ya hatua nyingine ambayo hatukuifahamu awali, ni hofu ya kuendea vitu vipya inayotunyima baraka zetu maishani


Huwezi kufahamu kama kuna uwezekano wa kupona mpaka utakapokuwa mgonjwa, huwezi kujua kama kuna uwezekano wa kuwa tajiri mpaka utakapokuwa masikini, huwezi kujua kama kuna imani mpaka utakapokuwa na woga

Maisha hayana maana kama hatupandi kutoka ngazi moja kuelekea ngazi nyingine, njia za kuendea kile ambacho Mungu ametuandalia ndio zinafanya maisha kuwa na maana, Jaribu kufikiri umeamka asubuhi na kukuta kila kitu ambacho uliwahi kuhitaji maishani mwako unacho pasipo kufanya kazi, kumuomba Mungu, Je utafurahia? Jibu la haraka ni HAPANA!

Kwa nini?
Ni kwa sababu hakuna utukufu kwenye kula, kunywa, au kufurahia kitu chochote ambacho hujakilipia kwa muda, nguvu, fedha, kufikiri n.k

Kinachofanya mbinguni kuwe na sherehe mtu mmoja anapotubu ni kwa sababu Yesu alilipa gharama ya dhambi zetu msalabani Luka 15:7 ``Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

Ukisoma Biblia sana utagundua kuna vitu ambavyo vinakutokea na Mungu ameviruhusu kwa sababu maalumu, inaweza kuwa ni kukufundisha kitu fulani, kuchochea imani yako au kuandaa ushuhuda

Ni mpaka ujue unapokwenda, ndio utafahamu ulipo, wakati mwingine tunabakia sehemu moja kwa muda mrefu siyo kwa sababu Mungu anataka tuwepo sehemu hiyo ila ni sisi hatujaona tunapopaswa kuelekea

Ndio maana ni muhimu kumshukuru sana Mungu katika kila hatua tunayopitia kwa sababu tunapomshukuru na kumsifu anatuonesha njia nyingine ambayo hatukuwa tunaifahamu 1Thel 5:18 Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.

Unapokutana na mguso wa NENO yaani YESU unagundua kwamba kuna baadhi ya vitu ambavyo haviko kwenye agano baina yako na YEYE, ghafla mwanga unawaka maishani mwako na unaanza kujiona katika kiwango kingine Kiroho

Hili linatokea tuu pale unapomtaka Yesu kuliko kitu kingine chochote maishani mwako, pale ambapo upo tayari kufanya lolote kwa ajili yake

Ndipo unapoweza kujiamini na kusema SITABAKI KAMA NILIVYO hata kama unapitia hali ngumu kiasi gani, unaamini kwamba unapita tuu, mambo yatabadilika, hali uliyonayo ni ya muda tuu utafika sehemu nyingine nzuri zaidi

Kinachofanya Ukristo kuwa na matumaini ni Yesu Kristo ambaye alituahidi kwamba atarudi kulichukua kanisa lake, jaribu kufikiri Yesu angekuwa harudi imani yako ingekuwaje?

SITABAKI KAMA NILIVYO -2
Ni uhakika siyo kitu cha kubuni au kujipa moyo ni kwa sababu ndio ukweli na ukweli hujitenga na uwongo, Ameniahidi kwamba kama nikimtumikia sitabaki kama nilivyo kwa sababu atanipatia na kunijazia kila nachohitaji Wafilipi 4:19 "Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu

Nikikumbuka nilivyokuwa mtoto sikuweza kutembea, nilianguka mara nyingi niliinuka, nikaanguka tena na tena na kadiri ninavyoanguka wazazi wangu waliniangalia, siyo kwamba hawakuwa wananipenda, ila ili niweze kutembea ni lazima nianguke kisha niinuke, niyumbe, nishindwe kusimama na baada ya kuanguka mara kadhaa naliinuka tena

Sasa nimekuwa ninatembea, sifikirii kuanguka tena, sipo kama nilivyokuwa ningali mchanga ninakwenda ninapotaka, silindwi tena nina uhuru wangu, kama sikubaki kama nilivyokuwa mchanga nina uhakika kabisa hali hii ni ya muda tuu na ninavuka kuelekea sehemu nyingine nzuri, inayometatameta

Siyo kwa nguvu zangu pekee ila ninayaweza yote katika Yesu Kristo anitiaye nguvu (Wafilipi 4:4) ninatengenezwa kiimani kwa ajili ya ushuhuda ujao, ninakumbuka msemo wa wahenga hakuna marefu yasiyo na ncha, giza linapozidi inamaanisha karibia kunakucha, karibia Mungu anamuaibisha Shetani na hila zake

Mtetezi wangu yu hai, ningali nimelala ananiandalia njia na kunilinda, ananiandalia meza mbele za watesi wangu sawa na Zab 23 na kama aishivyo ataniketisha na wafalme, Alisema kwamba hakuja kwa ajili ya matajiri au wanaomjua ila waliopigika na waliokosa matumaini, sina haja ya kulalamika wala kukufuru, nilipo pananiandaa kwa ajili ya wakati ujao

Hali kama hii ndio inanifanya nizidi kuamini kwamba yupo kwa sababu ningeonaje thamani ya maji kama nisingelisikia kiu, kama koo langu lisingekauka na midomo yangu kupauka?Ni nyakati ngumu zinatupatia mafunzo muhimu zaidi maishani, kila kipindi huja na kuondoka, nyakati ngumu hazidumu maishani, ila watu wanaomshika Mungu vizuri ndio wanaodumu

Ni lazima nitoke hapa nielekee juu kwa sababu vitu vyote vizuri huanzia chini kwenda juu, siyo juu kwenda chini na anayecheka mwishoni hucheka daima, Waache wanaocheka, wanaonibeza lakini kiukweli Sitabaki kama nilivyo ndio ninavuka kuelekea yale mema ambayo Mungu ameniandalia naam yale mambo ambayo jicho halikuyaona wala masikio kuyasikia (1Kor 2:9-10)

Laiti wangalijua kile ambacho Mungu amewaandalia wampendao wangalifumba vinywa vyao, lakini watajuaje kuna wakati wa kustareheshwa pande zote kama wasipoona nyakati za kupigika na kutoa jasho kila mahali

SITABAKI KAMA NILIVYO--3

Hakuna sababu ya kulalama kwa ajili ya wakati unaopitia, upo kwa ajili ya kukuandaa kwa kile ambacho Mungu kakiweka ndani yako, majaribu unayoyapitia sasa unapaswa kuyafurahia kwa sababu Yak 1:2 inasema " Ndugu zangu hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali"

Hauwezi kuinuliwa na kwenda sehemu nyingine bila majaribu, huwa tunafanya mitihani tukifaulu tunaenda darasa linalofuata mitihani ya maisha ni majaribu Yak 1:3 "Mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi"

Unakuwa mkamilifu na mtimilifu baada ya kushinda majaribu kwa hiyo kila jaribu lipo kwa ajili ya kukuinua na kukupeleka sehemu nyingine nzuri ambayo haukuifahamu mwanzo, tunapovuka katika majaribu ndipo tunapozidi kuuona utukufu wa Mungu na kuutambua uweza wake katika maisha yetu, tutamwabudu vipi kama asipotutendea matendo makuu na ya ajabu?

Mimi ninapita hapa duniani kile ambacho nitakiacha ni cha maana zaidi kwangu kuliko nitakachokipata, idadi ya watu nitakaosaidia, tabasamu nitakazotengeneza machoni pa watu, watumishi nitakaotengeneza hivi vitaongea zaidi kuliko mimi

Mambo mengi yatakuja na yatapita Lakini Mungu atabakia kuwa yule yule asiyebadilika na anayetenda matendo makuu, unapokuwa unajifunza na unatambua ya kwamba kati ya kitu muhimu sana unachopaswa kukifanya kama binadamu hapa duniani ni kufanya uchaguzi

Kama mkristo una chaguzi mbili mbele yako ni kumtumikia Mungu au kumtumikia Shetani, hakuna kukaa katikati ni lazima kuchagua mmoja, wengi kwa kutokufahamu wanamtumikia Shetani japokuwa hawajauza nafsi zao kwa damu lakini matendo yao yanaonesha imani waliyonayo

Kuna vitu vingi sana watu wanavyo lakini havimaanishi chochote kwa sababu hawamtumikii Mungu na wala hawana hofu ya Mungu

Jesus yuko hai hata sasa na anarekebisha kila kitu pale unapomtumikia Yeye na kuupeleka ufalme wake mbele sawa na Math 6:33 kwa kuhudumia wengine na kufuata amri za Mungu

Waendelee kukuona wanavyokuona lakini sehemu ambayo Mungu anakupeleka ni mbali zaidi ya unavyofikiri na wanavyodhani, giza linavyozidi kutanda jua pambazuko limekaribia naam asubuhi yako yaja, wingu linapojikusanya na kuwa zito jua mvua imekaribia kunyesha

Sitamani kuwa kama baadhi ya watu, sitamani nisichokifahamu kimepatikanaje ninatamani vitu vyenye misingi imara, iliyojengwa juu ya mwamba ambao ni Yesu Kristo

Mungu pekee ndiye anayefanya mambo mazuri kwenye mambo mabaya, anamtoa mtu kwenye ulevi na uasherati na kumfanya kuwa mtumishi, anamtoa mtu kwenye uuwaji na kuwa mtumishi, anamgeuza masikini kuwa tajiri

Unapoijenga imani yako zaidi kwa Mungu anaanza kukuinua kutoka kiwango hata kiwango na kutoka utukufu hata utukufu na anafanya suala lako kuwa la tofauti, hapo ndipo maneno haya SITABAKI KAMA NILIVYO yanakuwa na maana kwako
Mwisho wake....!
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote

Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana