CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA NANE - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, September 18, 2018

CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA NANE


Bwana Yesu asifiwe sana, Ninakusalimu katika Jina la Yesu Kristo, ni matumaini yangu umeamka vyema na una asubuhi tulivu inayokuandaa kwa ajili ya baraka zako za siku hii ya leo, mimi pia siko nyuma nina furaha na amani tele katika kumtumikia Bwana na kila siku Yesu amezidi kuonesha uaminifu wake katika maisha yangu

Nitangulize kuomba uniwie radhi kwa sababu jana hatukuwa na Neno hapa, sihitaji kujitetea kwa hili ila nilipumzika isivyo kawaida jana, ninaamini leo itakuwa siku nzuri ya kujifunza tena pasipo shida wala shaka, kumtumikia Mungu kuna raha na faida ndio maana ninaposhindwa kuandaa Neno ninajisikia vibaya

Tulipoishia....

Kama umekuwa una ulimi wenye tabia ya ndumilakuwili ni wakati sasa wa kujiangalia upya, ni vitu gani unapaswa kujibadilisha na kujiwekea nidhamu, wokovu ni majukumu na uamuzi ndiyo maana haukushikiwa bunduki kuokoka ni wewe uliamua mwenyewe kukiri, na kila uamuzi una gharama zake za kufuata ni wakati sasa wa kulipa gharama ya ulimi
Kama hukujifunza nasi somo hili la chunga sana ulimi wako sehemu ya saba unaweza ⇒⇒⇒kubofya hapa kusoma mtirirriko wote wa somo hili

Tunaendelea....

Japokuwa jana sikuandaa somo lakini nilikuwa na muda mzuri sana wa kutafakari Neno la Mungu na jana kipekee nilipata muda wa kutafakari juu ya ulimi nikajiuliza sana kwa nini watu wanasema uwongo? 

Baada ya kutafakari nilipata baadhi ya sababu, watu wanasema uwongo ili waweze kujinufaisha wenyewe, hakuna uwongo ambao huwa una lengo la kumsaidia anaeusikia hata kama unamficha mtu juu ya msiba wa mtu wake wa karibu bado lengo linakuwa ni hutaki kumuona akilia au akiumia kwa sababu utaingia katika kazi nyingine ya kumbembeleza na kumuonea huruma, mara zote uwongo ni kwa ajili ya kujilinda mtu binafsi

Yohana 8:44b "Asemapo uwongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, baba wa uwongo

Lakini kusema uwongo kuna tabia ya kujizidisha, maana yake kama umesema uwongo fulani leo itakubidi ufikirie kusema uwongo mwingine siku nyingine ili kutetea uwongo wa leo kwa sababu uwongo mmoja huzalisha uwongo mwingine, hii ni sheria ya kiroho kila kitu kinajizalisha kwenye mzizi kilipotokea ndiyo maana mtu hutegwa kwa maneno ya kinywa chake 

Mtu anayesema uwongo bado hajauvua utu wa kale, sababu ya kuokoka ni kuikubali kweli ili kweli itamuweka mtu huru Yohana 8:32 "Tena mtafahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru" maana yake ni kwamba utu wa kale ndiyo unaosababisha watu kusema uwongo ambao tunajua ni ule tuliourithi kutoka kwa Adamu wa kwanza baada ya kutenda dhambi

Wakolosai 3:9-10 "Msiambiane uwongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; Mkivaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu kulingana na mfano wake yeye aliyewaumba

Suala la kusema uwongo ni la ufahamu na tunapookoka tunamkiri Yesu Kristo ili aweze kutuongoza katika kila kitu ambacho tunakifanya, kumkiri Yesu ni kufanana naye na kuwa na ufahamu kama alivyo yeye kama Yesu hawezi kusema uwongo basi na anayeongozwa na Yesu hapaswi kusema uwongo, kusema uwongo ni kiashiria cha mtu asiyeongozwa na Roho Mtakatifu

Jambo la kutafakari hapa watu ambao wanasema uwongo huwa na nia ya kuzilinda nafsi zao, ili wasionekane wabaya au walikosea sehemu fulani au walikwepa majukumu lakini wanasahau kitu kimoja muhimu sana kwamba katika kuilinda nafsi ndiyo wanaipoteza na kuangamia, hii ni kwa sababu mtu anayesema uwongo anafikiri anaweza kujiinda peke yake 

Luka 17:33 "Mtu yeyote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; naye atakayeiangamiza ataiponya, unaingamiza kwa kujitoa kwa ajili ya wengine na kwa kusema ukweli hata kama unakuuma na unakuchoma 

Baba wa uwongo ni Shetani Yohana 8:44b "Asemapo uwongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, baba wa uwongo, Shetani anasema uwongo kwa sababu maalumu ili apate nafsi za kuvuna na kuchomwa naye katika hukumu yake, tunapaswa kufahamu kwamba Shetani ameshaukumiwa ni binadamu pekee hawajahukumiwa

Ndiyo maana hata leo Yesu anakusubiria utubu na urudi kwake, kama umeamka mzima jua umepewa tena neema ya kutubu kama bado haujatubu, siku zote tambua kwamba haustahili bali unastahilishwa na Yesu Kristo, jiulize ni mara ngapi umesema uwongo? Je katika uwongo huo ulinufaika nini?

Dunia tunayoishi sasa ni ya ajabu sana, watu wameshaugeuza uwongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uwongo kiasi ambacho hata ukitafuta mchumba ili uweze kumpata ni lazima umwambie uwongo, ujifanye una vitu fulani ambavyo hauna, umuigizie maisha ya mapicha picha ndiyo anakuelewa na kukukubali, ukisema ukweli unaonekana limbukeni hii ndiyo namna ambavyo Shetani kaharibu dunia

Kafanya viumbe wa Mungu kuigiza maisha fulani ambayo hawayaishi na anatumia mitanao kuharibu watoto wetu, ndugu zetu na hata wadogo wetu kiasi ambacho kuna muda ninaweza kukaa nikaangalia watu wanavyonunua magazeti ya udaku moyo ukaniuma, kama gazeti linaitwa udaku yaani umbea mtu mzima na akili yako unanunua la nini? Haya umeufahamu umbea ambao ni uwongo itakusaidia nini, itabadilisha vipi maisha yako

Zipi ni sifa za uwongo?

Sifa kubwa ya uwongo ni kwamba huwa ni wa muda mchache, haijalishi umedanganya nini lakini baada ya muda ni lazima utajulikana, Mithali 12:19 " Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; bali ulimi wa uwongo ni wa kitambo tuu, usijidanganye kwamba unaweza kuongea uwongo wa milele

Mungu tunaemtumikia ni wa milele kwa sababu anasema ukweli la sivyo kuna siku moja watu wangemkamata katika uwongo na umilele wake ungeondoka, ni ukweli tuu unaodumu milele ndiyo maana Mathayo 24:35"Mbingu na nchi vitapita lakini; maneno yangu hayatapita kamwe"

Uwongo ni baina ya binadamu na binadamu na siyo Mungu, kamwe huwezi kumdanganya Mungu kwa sababu yeye huona sirini unaweza kumdanganya binadamu mwenzio ndiyo maana Luka 8:17 "Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajuikana na kuwekwa wazi, ongea uwongo kama unavyopenda lakini kamwe jua humdanganyi Mungu na kuna siku moja utahukumiwa na uwongo wako

Mungu anasemaje juu ya watu waongo?

Hakuna muongo ambaye hataangamia, hata ukiwa shahidi wa uwongo bado Mungu atakuangamiza kwa sababu umekuwa adui wa haki za mtu mwingine, uwongo ambao Shetani aliufanya kwa Hawa ulitunyima haki zetu kama viumbe wa Mungu awali, namshukuru Yesu Kristo kwa kuturejeshea kila tulichopoteza Mithali 19:9 "Shahidi wa uwongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uwongo ataangamia

Tambua ya kwamba kila unapoongea uwongo unamchiza BWANA, na kama unamchukiza hawezi kukubariki wala huwezi kumfurahisha, unapomfurahisha Mungu ndipo anapokubariki na kila ambacho unakitamani Mithali 12:22 "Midomo ya uwongo ni chukizo kwa BWANA; Bali watendao uaminifu ndiyo furaha yake

Uwongo utakufukuza nyumbani kwa Mungu, kwa sababu Mungu siyo muongo hawezi kamwe kukaa na muongo hata kwa dakika moja ni lazima atamfukuza, kwa maana nyingine hutasitawi wala kupata kibali kwa Mungu, tambua maisha yetu tunatafuta kibali kwa Mungu, unapokuwa na kibali hakuna kitu ambacho hakifanikiwi, kumbuka ukifukuzwa nyumbani kwa BWANA utakwenda jehanamu ya moto Zaburi 101:7 "Hatakaa ndani ya nyumba yangu Mtu atendaye hila. Asemaye uwongo hatathibitika Mbele ya macho yangu

Itaendelea tena ......

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote

Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana