Ninakusalimu katika Jina la Yesu Kristo, Bwana wetu na mwokozi wetu, hili ni juma jipya kumbuka kila juma lina baraka zake na Juma hili utakutana na baraka zako zote katika Jina la Yesu, ninamshukuru Mungu kwa ajili yako na nina imani wewe ni mzima wa afya hata mimi pia
Tulikuwa na majuma mazuri ya kujifunza mada ya kubali kubailika na ninamshukuru sana Mungu kwa kutuwezesha kuweza kujifunza mada ile mwanzo mpaka tulipofikia tamati ijumaa iliyopita kama hukusoma ⇛⇛BOFYA HAPA KUSOMA
Hiki ni kichwa kingine cha neno chunga sana ulimi wako lakini nikutaarifu kwamba hiki siyo kichwa cha somo kinachoendelea kwa sababu nimechelea kuandaa somo ndiyo maana nilichukua somo hili la nyuma kwa msaada wa Roho Mtakatifu nikalijaza nyama sababu lilikuwa halijitoshelezi
Tafadhali kesho ukiona kichwa kingine cha neno usishangae wala usighadhabike ndiyo maana nimetoa taarifa mapema, lakini pia kama ukiona hiki kinaendelea ni heri pia na yote yatakuwa ni mema mbele za Mungu
Tuanze neno la leo....
Matumizi ya ulimi wako yanaweza kukuletea faida au madhara, ulimi ni kiungo kidogo sana lakini kinasababisha kila kitu kwenye maisha ya binadamu kutokea, usipotamka na kukiri hakuna kinachotokea maishani mwako hii haijalishi ni baraka au laana
Wengine wamekuwa wanatumia ndimi zao kulaani wengine na kujitamkia laana na maneno ya kukatisha tamaa, lakini wapo ambao wanatumia ndimi kubariki na kujitamkia maneno ya baraka, mstari wa mafanikio na umasikini ni mwembamba sana kiasi ambacho unaweza kuathiriwa na ulimi
Wengi wanadanganywa na manabii wa uwongo kwa sababu wanafikiri wao sio manabii, Biblia haikuandikwa kwa ajili ya watu maalumu, kumbuka kila mtu ameitwa kumtumikia Mungu ila ni wale ambao wanaomtumikia zaidi wanatofautishwa na wengine, kiwango cha mtembeo wako kinaendana na utumishi wako
Nabii wa kwanza wa maisha yako ni wewe mwenyewe, kwani nabii anatamka nini si maneno? Na hayo maneno si ni lazima yawe neno la Mungu? Hivyo kama umetambua hili ukatafuta kile ambacho neno la Mungu linasema kuhusu maisha yako ukajitamkia asubuhi, mchana na jioni kwa imani unafikiri hakitatimia? Ni suala la Imani tuu asikudanganye mtu
Sasa kuiamuru siku yako si ndio unabii? utaiamuru vipi kama hakuna maneno ambayo utatamka na kama hakuna vitu ambavyo unataka kuviona? hiki siyo kipindi cha kukariri mistari ya Biblia ni kipindi cha kupata maarifa na kuyaishi
Hakuna anayejua maisha yako kuliko wewe mwenyewe, kumbuka kama umempokea Yesu yupo ndani yako sasa amua ni kipi rahisi kuzungumza na Yesu aliye ndani mwako au kwenda kutabiriwa? Usiseme ninacheza na maneno ila ndio ukweli lakini ili haya kutimia ni lazima ukue kiwango chako cha imani, ni lazima utoke kwenye utoto uende kwenye wana kwa sababu mtoto siyo mrithi bali mwana
Nilisema kwamba sifundishi watu kuwa watoto wala sina mpango wa kutengeneza watu tegemezi Mungu ameniambia nitengeneze wanafunzi, watu watakaoweza kujisimamia wenyewe, watu wataoanzisha mambo mengine, waalimu wengine, wachungaji na wainjilisti wengine ndiyo maana mafunzo yangu yote yanalenga mtu kujua kujitegemea
Mmekuwa watumwa wa watu inatosha sasa, soma neno jifunze neno, elewa neno na liishi neno ule muda wa kutegemea watumishi uishe ukija kwangu ni kwa maelekezo maalumu, ni kwa ajili ya kuchochea imani yako
Hivyo asikudanganye mtu kuanzia sasa tamka maneno matamu na mazuri unayotaka kwenye maisha yako kwa ulimi wako, hizi habari za Magufuli amebana, sijui hela haionekani, maisha magumu achana nazo waache watamke wao, kumbuka utakula maneno ya kinywa chako kama kitu hukitaki unatamka cha nini?
Ulimi ni kiungo muhimu sana na ndio unaoleta ladha ya kila mahali, ladha ya chakula inaletwa na ulimi, Iadha ya mahusiano inaletwa na ulimi hali kadhalika na ladha ya maisha yetu 1Petro 3:10 "Kwa maana, atakaye kupenda maisha, na kuona siku njema, auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila"
Kila kitu kina uzuri wake lakini ukikaa kutafuta ubaya badala ya wema na kutumia ulimi na mdomo wako kuongelea hayo basi hata siku yako itakuwa mbaya na iliyokosa baraka
Biashara, kazi, mahusiano, udugu hujengwa kwa ulimi, namna ambayo unaongea na wateja wako, unavyoongea na familia yako, mkuu wako wa kazi na watendakazi wenzio ndio itaamua ufanikiwe au ubomoe unachokifanya
Binadamu tumekuwa tunaongea maneno mabaya, maovu ya kukatishana tamaa na kujiambia kwamba hatuwezi kufika sehemu fulani au hatuwezi kufanikisha suala fulani lakini tunasahau kwamba kile ambacho tunakikiri kwa ulimi na midomo yetu ndicho ambacho hutokea
Neno ni sawa na kiapo, ndiyo maana viongozi huapizwa kwa maneno na kwa mujibu wa dini zao, Amini Amini nakuambia hakuna sababu yeyote ya kusema jambo ambalo haulitaki maishani mwako
Isitoshe hata suala zima la imani yetu na suala la kwenda mbinguni lipo kwenye ulimi na kwenye moyo Warumi 10:9 "Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu utaokoka
Kama unataka utajiri usikae ukae chini na kukiri wewe ni masikini na huwezi kufanikiwa, kama unataka kuwa na mahusiano mazuri na watu usikae useme fulani anaringa na hataki kushirikiana na watu, kama unataka mafanikio kielimu usikae useme nitafeli somo fulani au mimi ni dhaifu sehemu fulani, kiri na tamka tena kwa ujasiri kitu ambacho unakihitaji pekee
Hii ndiyo maana Biblia ikasema katika Waefeso 4:29 "Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia"
Una kila sababu ya kutamkia watu habari njema na za kufurahisha, una kila sababu za kuwabariki watu kwa kile ambacho Mungu amekupa, kiuhalisia hakuna mtu mbaya hata mmoja duniani kila mtu ana uzuri wake kabla ya kuangalia ubaya tafuta uzuri na utamke
Itaendelea.....
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;
SALA YA TOBA
Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa
Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani
Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.
Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu
Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana
Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana