KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 18 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, September 6, 2018

KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 18

Co-Founder at MT Sialove Lukumay
Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu, nina imani ndani ya moyo wangu kwamba wewe ni mzima wa afya na unaendelea vyema na kazi zako, hata mimi pia ninaendelea vyema kwenye kazi ya Bwana wetu Yesu Kristo

Leo tutaendelea na somo letu la kubali kubadilika sehemu ya kumi na nane kama hujasoma mfululizo huu wa masomo haya mpaka tulipofikia unaweza kuyasoma yote kwa njia rahisi ambayo ni ⇉⇉⇉KUBOFYA HAPA

Tulipoishia....
Mkungu wa ndizi ni kuokoka na jitihada za kupiga mbizi mpaka kufika pwani kwa kutumia huo mkungu wa ndizi ndio wokovu wenyewe, hivyo kuokoka pekee haitoshi unapaswa kuenenda katika wokovu ndipo unapopata udhihirisho wa nguvu na uweza wa Mungu katika maisha yako

Kabla ya kuendelea ninapenda kutumia nafasi hii kukutaarifu kwamba nitakuwepo kwenye Women Summit Jumamosi hii pale Jengo la Golden Jubilee- PSPF Ghorofa ya 6 Posta kama mmoja wa Panelist hivyo ninakukaribisha sana zaidi tizama tangazo hili hapa


Tunaendelea...
Jana tuliona sababu nyingine moja ya kwa nini Mungu habadiliki ambayo ni Ili mabadiliko yaweze kutokea ni lazima kuwe na mfumo maalumu/ mpangilio maalumu yawe ndani ya muda,  kama hukujifunza somo la jana tafadhali bofya linki hapo juu kujifunza lilikuwa somo zuri sana

Sababu nyingine ya kwa nini Mungu habadiliki ni;

Mabadiliko huathiriwa au husababishwa na mbegu ambayo imeingia katika akili ya mtu, ni kweli dhahiri kwamba Mungu ni roho nao wamwabuduo yawapasa kumwabudu katika roho na kweli, Mungu amejifunua kwetu kama mwenye Roho saba Isaya 11:2-3 "Na Roho ya BWANA itakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA, na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA

Hivyo kiuhalisia mtu anayebadilika ni aliyepata maarifa au ufahamu mpya, kama Mungu ndiye mwenye roho za zinazotupatia maarifa na ufahamu kamwe hawezi kubadilika kwa sababu ana maarifa yote na ufahamu wote

Tunaona katika Neno la Mungu kwamba Yeye ndiye aliyempatia Suleimani hekima IWafalme 3:9 "Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana nani awezae kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?

Kama Mungu ndiye anagawia watumishi wake roho hizi ina maana kwamba Mungu hawezi kubadilika kwa sababu yeye ni zaidi, kumbuka hakuwahi kutokea mtu mwenye hekima kuliko nabii Suleimani kwenye Agano la kale, Yesu Kristo ndiye aliyekuja kuvunja rekodi yake na ni Agano jipya

1Wakorintho 1:25 "Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya mwanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya mwanadamu, jaribu kufikiri hekima yote aliyokuwa nayo Suleimani ule ndio upumbavu wa Mungu kwa sababu Mungu alimpa tone la hekima yake

Huwezi kamwe ukasema unaweza kupima akili za Mungu na ndiyo maana kamwe hawezi kubadilika maana akili zake hazina mipaka anafanya kila anachotaka kufanya na hakuna cha kumzuia Zaburi 147:5 "Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mipaka

Kukuonesha kwamba Mungu ndiye mwenye akili zote na maarifa yote na hawezi kubadilika hata hesabu ya nywele zako aweza kukuambia pasipo kukosea (Luka 12:7) hivyo katika hali kama hii huwezi kusema Mungu atabadilika, sasa abadilike aende wapi na kila kitu anacho, kila nguvu na uweza ni wake

Kwa maana nyingine ni sawa kama nikisema ya kwamba akili ya Mungu haimruhusu kubadilika, kwa sababu hakuna kitu kingine chochote kile chaweza kumfundisha Mungu a kumpatia maarifa mapya au hekima mpya ya kufanya mambo yake mwenyewe ndiyo maana kamwe hatoweza kubadilika

Udogo wetu tulionao kuliko Mungu ndiyo unaotufanya tubadilike Mfalme Daudi rafiki wa Mungu wakati fulani alikuwa anatafakari utukufu wa Mungu na alisema maneno mazuri sana ambayo ninatamani nawe ujifunze siku ya leo Zaburi 8: 3-5 "Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha; Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo kuliko Mungu, umemvika taji la utukufu na heshima

Maneno haya ya Mfalme Daudi yanaonesha ukuu wa Mungu na namna ambavyo Mungu yupo bize kiasi ambacho Mfalme alikuwa anaona hana hata haja ya kuangaliwa na Mungu, ndugu mpendwa mambo mengi uliokuwa nayo kwenye maisha yako siyo kwamba unastahili ila ni kwa neema ya Mungu tuu, hivyo kamwe usijisifu kwa lolote lile

Kiuhalisia Mungu hachunguziki hata kidogo mimi ninaamini ninachojua kuhusu Mungu hakijafikia tone la maji, siku nikifanikiwa kufika tone la maji nitafikia mtembeo wa Yesu aliokuwa nao hapa duniani, Ayubu 26:14 "Tazama hivi ni viunga tu vya njia zake; Na jinsi yalivyo madogo manong'ono tusikiayo katika habari zake! Lakini ngurumo za uweza wake ni nani awezaye kuzielewa? kamwe nakiri hakuna ndio maana hawezi kubadilika

Kwani wewe hujui au haujasikia ya kwamba Mungu ni wa milele na ndiye aliyeziumba mbingu na dunia, na kwamba hazimii, wala kamwe hachoki na kamwe akili zake hazichunguziki? tena anasema Isaya 55:8-9 "Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu asema BWANA

Mstari wa 9 "Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, ndivyo njia zangu zilivyo juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu, kama ukuu wa Mungu una utofauti mkubwa hivi na njia ambayo ndio akili zake ipo tofauti nasi kiasi hiki basi kamwe Mungu hawezi kubadilika, sasa abadilike aende wapi?

Leo tuishie hapa tukutane tena wakati mwingine, Mungu akubariki katika Jina la Yesu

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana