KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 17 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, September 5, 2018

KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 17

Humphrey Makundi MD at MT 
Nina furaha na amani tele, ninatumaini na kwako mambo ni shwari na matamu sana kama ilivyo kwangu, ninakusalimu katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, Jina lipitalo majina yote katika ulimwengu huu na hata ule ujao, leo tena ninapenda kukukaribisha tujifunze neno la Mungu kwa pamoja na kwa nia ya dhati kutoka katika kilindi cha moyo wangu ninamuomba Roho Mtakatifu akufunulie na wewe kile ambacho amekusudia kwa ajili yako leo

Mimi ni Mtumishi wa Mungu tuu, sina nguvu wala uwezo wa kuingiza maarifa akilini mwako, lakini yupo ambaye mwenye uweza wa kufanya hivyo huyu ndiye Roho Mtakatifu, ndiye mwalimu mwema ananitumia mimi kama chombo chake kuwasilisha kile anachotaka kifundishwe ila ndiye anayepigilia msumari neno lake katika mioyo ya watu

Hivyo kamwe usikae unione kwamba ni wa tofauti sana na kunisifia hapana, tambua ninafanya hivi kwa neema ya Mungu pekee aliyonikirimia ndiyo inayonifanya kuwa hivi nilivyo, ndiyo inayonifanya nijisifu kwake, ndiyo inayonipa kujiamini na kufundisha kwa madaha, nje ya Yesu mimi siyo kitu ni bure na hovyo kabisa

Leo tutaendelea na somo letu la kubali kubadilika sehemu ya kumi na saba kama hujasoma mfululizo huu wa masomo haya mpaka tulipofikia unaweza kuyasoma yote kwa njia rahisi ambayo ni⇒⇒⇒ KUBOFYA HAPA

Tulipoishia.....
Hivyo haina shaka kwamba kama Mungu angekuwa katika hali ya miili kama yetu angebadilika kwa sababu naye angekuwa anafikiria mambo ya kimwili, na kama ni angekuwa na mwili kama wetu angekuwa mzazi na siyo Mungu, ndiyo maana yeyote anayeufuata mwili kamwe hawezi kumpendeza Mungu Warumi 8:6 "Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani

Tunaendelea...
Jana tuliona sababu nyingine moja ya kwa nini Mungu habadiliki ambayo ni Mungu ni Roho na tunafahamu ya kwamba Roho haiwezi kupoteza uhai na Roho ndiyo inayotoa uhuru ni vitu ambavyo vina nafsi ndivyo vinaweza kubadilika, binadamu ni nafsi hai ndiyo sababu anabadilika kama hukujifunza somo la jana tafadhali bofya linki hapo juu kujifunza lilikuwa somo zuri sana

Sababu ya sita kwa nini Mungu habadliki ni;

Ili mabadiliko yaweze kutokea ni lazima kuwe na mfumo maalumu/ mpangilio maalumu yawe ndani ya muda, Mungu ametengeneza muda na wakati kwa ajili ya kuwezesha mabadiliko kutokea kwa mwanadamu lakini siyo kwake, ukisema kwamba Mungu abadilike ni sawa na kusema Mungu ni duni kwa sababu mabadilko hutoa kitu kutoka kwenye hali ya uduni na kukipeleka katika hali ya uimara/ ubora

Jambo la msingi ninaloomba uelewe hapa ni kwamba ili kitu kitokee kwenye maisha yako muda wa kuanza ni Mungu anayeamua siyo wewe, kwa sababu mazingira ya kufanya kusudi lako ni Mungu anayatengeneza kwa ajili yako, lakini ufanisi wake na uharaka wake ni jukumu lako kujituma na kuhakikisha unafanya kwa wakati, Mungu amejifunua kwetu kama Mungu wa muda na wakati lakini kwa Mungu binafsi muda haumuendeshi kwenye kufanya kazi zake ila muda upo kwa ajili ya binadamu kuweza kufanya kazi zake

Hivyo kama huwezi kutambua muda ambao Mungu ameukusudia kwa ajili yako basi jua ya kwamba hata Mungu mwenyewe hawezi kukusaidia atakuacha hapo uteseke mpaka uchoke siku akili yako ikifunguka utaondoka, hii ndiyo maana hata wana wa Israeli safari iliyowapasa kutumia siku arubaini iliwagharimu miaka 40

Tizama tena kipindi cha Daniel walipokuwa utumwani Mungu hakuwa na muda wa kuja kuwakumbusha muda wao wa utumwa umeisha ni mpaka Danieli alipovisoma vitabu na kugundua mwenyewe ndipo walipoanza mikakati ya kujiondoa katika nchi ya utumwa

Mungu akianza kufanya kazi zake kwa muda anakuwa siyo wa milele tena bali wa wakati fulani na kumbuka Mungu wetu ni wa milele Mithali 33:11 "Shauri la BWANA litasimama milele, Makusudi ya moyo wake milele hata milele, hivyo kama Mungu ni wa milele ina maana Yeye hatendi mambo yake binafsi ndani ya muda ila viumbe vyake vyote vipo ndani ya muda na wakati

Ukisema kwamba Mungu anajitendea mambo yake binafsi ndani ya muda ina maana muda unamfunga Mungu, kumbuka Mungu ndiye aliyeumba kila kitu hivyo hata muda na majira ni yeye alivitengeneza kwa hiyo kama ikiwa hivyo itakuwa Mungu anatawaliwa na muda kitu ambacho siyo kweli

Kitabu cha Mhubiri 3:1 "Kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu, soma tena mstari huo kwa makini, tizama inasema chini ya mbingu siyo mbinguni kwa Mungu ni lazima uelewe jambo hili ili kuweza kumfahamu Mungu wako alivyokuwa wa ajabu na alivyo na mizungu mingi

Hivyo tunavyokuwa tunaongelea masuala ya muda na wakati ni hapa duniani na siyo mbinguni, Mungu ni wa ajabu kiasi ambacho hata siku ya mwisho wa dunia hakuna anayeifahamu isipokuwa yeye pekee Yesu mwenyewe alikiri haifahamu Mathayo 24:36 " Lakini kuhusu ile siku na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake

Kuwa makini siku inayoongelewa ni mwisho wa dunia siyo mwisho wa mbinguni, kwa sababu ukisema mwisho wa mbinguni na Mungu naye anajumuishwa katika mwisho hivyo atakuwa amebadilika siyo tena wa milele kumbuka Mungu ni wa milele ndiyo maana suala la muda kwake siyo kigezo cha kutenda matendo makuu

Tambua kwamba muda upo kwa ajili ya viumbe ili kukua na kuweza kufikia hatua nyingine lakini siyo kwa ajili ya Mungu, kwa sababu siku ambayo Mungu atakayoanza kuendeshwa na muda ina maana muda utakuwa mkubwa zaidi yake na atakuwa na kikomo katika utendaji kazi, lakini pia hatakuwa wa milele kwa sababu neno milele ndiyo linaondoa muda kwa Mungu, ndiyo maana Mungu hawezi kubadilika kwa sababu ni wa milele

Huu ufunuo ni mgumu kwangu lakini Mimi ni Mtumwa wa Bwana nakubali kila ninachosikia na ninaandika, Zaburi 41:13 "Na atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina, hivyo tunamtukuza Mungu kwa sababu ni wa milele ina maana tukiuondoa umilele wa Mungu hatuwezi kamwe kumtukuza katika maisha yetu, kumbuka umilele wa kitu unaweza kuondolewa kwa muda

Muda ni kikomo cha kitu fulani kufanyika au kutendeka, hivyo ukiuweka muda kwa Mungu mwenyewe kama kigezo cha kufanya mambo yake mbinguni ina maana Mungu ana ukomo na hivyo umilele unaondoka na moja kwa moja atakuwa ameshabadilika, hivyo tambua ya kwamba umilele wa Mungu ndiyo unaomfanya asibadilike

Tizama tena Zaburi 90:2-4 "Kabla haijazaliwa milima, wala haujaiumba dunia, na tangu milele hata milele wewe ndiwe Mungu, Wamrudisha mtu mavumbini usemapo rudini enyi wanadamu, Maana miaka elfu machoni pako, Ni kama siku ya jana ikisha kupita, na kama kesha la usiku

Neno hilo linaonesha dhahiri kwamba kitu kinachoitwa muda kwa Mungu hakifanyi kazi bali kwa wanadamu na viumbe alivyoumba, jaribu kutafakari kwa namna ya Mungu tangu Yesu Kristo aje duniani ina maana ni siku mbili zimepita, pengine hata hazijaisha maana tizama anasema ni kama kesha la usiku

Hii inakupa picha kubwa ya hiki nilichokuwa ninakielezea tangia mwanzoni kwamba machoni kwa Mungu muda siyo kigezo na Mungu haendeshwi na muda kwa sababu yeye ndiye aliyetengeneza muda na wakati kwa ajili ya binadamu na siyo kwa ajili yake, na kumbuka muda ni kwa ajili ya mabadiliko Mungu hawezi kamwe kuwa chini ya muda kwa sababu akifanya hivyo atakuwa anabadilika na Mungu wetu habadiliki

Ukitizama tena mstari huo unasema tangu milele hata milele, Mungu alikuwa ni Mungu maana yake hata uwepo wa Mungu au asili ya Mungu haina muda, haijulikani ni lini Mungu alitokea, haijulikani pia Mungu ataendelea kuongoza mpaka lini ni kwa nini ni kwa sababu Mungu hayupo chini ya muda naam haendeshwi na muda na ndiyo maana Mungu habadiliki

Unajua hii ndio inazidi kutoa mwanga zaidi kwa nini kuokoka ni suala la ghafla na siyo la muda, kwa sababu wakati mtu anapomkiri tuu Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake wakati huo huo anahamishwa kutoka katika ulimwengu huu anapelekwa katika ulimwengu mwingine anakaa na Yesu katika ulimwengu wa kiroho 

Ninaomba uelewe kuna tofauti kati ya kuokoka na wokovu na ninaweza kukueleza kwa kifupi namna hii kwamba kuokoka ni kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako, lakini wokovu ni kuishi maisha ya Kristo yaani kuenenda katika roho, wokovu ni wa muda ndiyo maana wokovu unafanyiwa kazi ila siyo kuokoka

Hivyo usijidanganye kwamba ukiokoka kila kitu kitabadilika hapo hapo kwenye maisha yako, hapana kitabadilika kwenye ulimwengu wa kiroho sasa kwa sababu bado hujaanza kuuishi wokovu itakubidi uchukue muda ili kuweza kuona matokeo ya kile ambacho Mungu ana makusudi nacho katika maisha yako, ndiyo maana binadamu anabadilika 

2Tim 1:9 inagongelea msumari hili "ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye mwenyewe na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele"

Wote tumeokolewa ila hatujapewa wokovu, wokovu ni kazi yako kwa maana nyingine ni kwamba wokovu unaufanyia kazi wewe binafsi ili uweze kudhihirika katika maisha yako, wengi wanaishia kwenye kuokolewa chukua hatua zaidi nenda kwenye wokovu tendea kazi kuokolewa kwako

Hii ndiyo sababu Mtume Paulo aliwaambia Wafilipi 2:12 "Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii siku zote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka

Nikuelezee namna hii kwa mfano kama ulikuwa unasafiri na meli kisha mkafika katikati ya bahari meli ikaanza kuzama, nahodha akagawa maboya bahati mbaya ukakosa akasema mliokosa maboya kuna njia mbili ya kwanza ni kubakila kwenye meli mpaka izame kabisa au kujitosa baharini, ukaamua kujitosa baharini kwa bahati zuri Mungu akakuonesha mkungu wa ndizi ukielea ukapata ufahamu kwamba ule hauzami ukaupigia mbizi ukaufuata ukautumia mkungu ule kuelekea pwani na ukafika salama

Mkungu wa ndizi ni kuokoka na jitihada za kupiga mbizi mpaka kufika pwani kwa kutumia huo mkungu wa ndizi ndio wokovu wenyewe, hivyo kuokoka pekee haitoshi unapaswa kuenenda katika wokovu ndipo unapopata udhihirisho wa nguvu na uweza wa Mungu katika maisha yako

Ninatamani kuendelea lakini kwa sababu ya muda leo naomba niishie hapa Mungu akubariki sana, tutaendelea tena kesho;

Rafiki katika Kristo Yesu umejionea mwenyewe leo sababu moja muhimu ukijumlisha na za jana zinafika sita za kwa nini Mungu habadiliki, kumbuka Mungu ndiye aliyekuumba anakujua kuliko unavyojijua kwa nini unaufanya moyo wako kuwa mgumu hivyo kumpoke Yesu Kristo? Kama uanaisikia sauti yake pokea neema hii ya wokovu 

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana