KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 16 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, September 4, 2018

KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 16

Co-Founder at MT Sialove Lukumay
Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo Bwana wetu, nina imani kwamba ni mzima wa afya na unaendelea vyema, karibu tena katika wakati mzuri wa kujifunza neno la Mungu lenye nguvu pamoja nasi, Roho Mtakatifu aliye mwalimu mwema akufundishe na kukufunulia ujumbe ambao ameuandaa kwa ajili yako siku ya leo

Leo tutaendelea na somo letu la kubali kubadilika sehemu ya kumi na sita kama hujasoma mfululizo huu wa masomo haya mpaka tulipofikia unaweza kuyasoma yote kwa njia rahisi ambayo ni ⇉⇉⇉KUGUSA HAPA

Tulipoishia.....

Ninatumaini hata wewe upo kwenye moja ya karama hizo, na umeshaifahamu sehemu yako na unaifanyia kazi kwa bidii na nguvu zako zote, maisha ni mabaya sana kama unafanya kitu nje ya kusudi la kuumbwa kwako, usitumie nguvu nyingi kutafuta hela, tumia nguvu na akili kutafuta kusudi, kisha songa mbele na kusudi hilo mwishoni lazima litaongea cha muhimu usiache kulifanyia kazi na mwamini Mungu

Tunaendelea...

Jana tuliona sababu zingine kuu mbili za kwa nini Mungu habadiliki ambazo ni utakatifu wa Mungu ambao  unamuweka mbali na dhambi, ni vitu ambavyo siyo vitakatifu ndio vinavyobadilika katika maisha, lakini pia tuliona ni kwa sababu watu hawatamuamini kama akibadilika, tunamwamini kama Mungu wetu kwa sababu anachosema ndiyo anachofanya na hiyo ndiyo sifa ya Mfalme

Sababu ya tano ya kwa nini Mungu habadiliki ni;
Mungu ni Roho, na tunajua ya kwamba alipo Roho kuna uhuru 2Kor 3:17 "Basi "Bwana" ndiye Roho; lakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru, maana ya uhuru ni kuwa na kila kitu na kuweza kufanya kila kitu, ukweli ni huu hakuna nchi yeyote duniani au mtu yeyote duniani ambaye amewahi kufikia hali hii pasipo msaada wa Yesu Kristo

Kuwa huru maana yake hakuna kinachokusumbua, hakuna shida ya aina yoyote, huna madeni, husumbuliwi na maisha au kazi au watoto au taaluma yako au nguvu za giza ndiyo maana Neno la Mungu linasema katika Yohana 8:36 "Basi mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli

Nimekuwa ninaangalia watu wanaohudhuria huduma za kufunguliwa (deliverence) cha kushangaza ni kwamba mtu anakwenda leo anafunguliwa juu ya suala fulani na mtumishi wa Mungu lakini baada ya muda anarudi pale alipokuwepo mwanzoni, siri ni kwamba anapaswa kuenenda katika hatua nyingine ya pili ya kuweza kujifungua mwenyewe 

Ninasema hivi kwa sababu siyo Mtumishi wa Mungu anafungua watu bali ni Yesu Kristo na kama umeokoka maana yake umempokea Yesu Kristo, yupo ndani yako na wewe unapaswa kukua kiroho uwe ndani yake hapo ndipo unapoweza kuwa huru hili siyo suala la kunywa maziwa bali kula chakula ndiyo maana Neno likasema Yohana 8:36 "Basi mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli

Hautafuti kuwekwa huru na mtumishi fulani wa Mungu bali na Yesu Kristo, niliteseka nilivyokuwa sifahamu leo na wewe fahamu hili litakusaidia sana, hivyo kama Mungu ndiye anayeweka watu huru kweli kweli ina maana hawezi kamwe kubadilika, tizama tena kuna kweli mbili kweli ya kwanza ya kuombewa ya pili ni ya Yesu, maana yake unawekwa kweli na mtumishi ila unakuwa kweli kweli na Yesu Kristo pekee

Kama unafuatilia kwa makini kile ambacho ninafundisha hapa utagundua kitu kimoja, mafunzo yangu yote hayalengi kukuambia ukaombewe au ukasaidiwe na mtumishi fulani, yamelenga kukufungua na kukuonesha nini unachoweza kufanya mwenyewe kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu na kupokea muujiza unaotamani maishani mwako

Mungu karama aliyonipatia siyo tuu kufundisha na kufurahia kuwa na waumini wengi bali ni kutengeneza watu wanaoelewa Neno la Mungu kama mimi ninavyofundishwa na watu hao kuweza kusimama na kulitumia neno hilo kwenda kinyume na kila hila za mwovu katika maisha yao, hivyo unapokuwa unapata neno hapa kuwa makini tambua sitengenezi tegemezi bali tegemeo

Lakini pia kumbuka kwamba ili kuweza kumwabudu au kuwasiliana na Mungu ni lazima tuwe katika Roho, Yohana 4:24 "Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli, roho ndiyo uhai wa kitu na damu imebeba uhai wa kitu, wote tunafahamu ya kwamba kuna miili maalumu ya mbinguni kwa sababu miili tuliyonayo inaharibika

Hivyo kwa sababu Mungu ni Roho, na Roho ya Mungu ndiyo yenye uweza wa kufanya kila kitu, kamwe hatokaa aweze kubadilika, isitoshe roho tulizonazo sisi ni matokeo ya pumzi aliyotupulizia kipindi tunaumbwa Mwanzo 2:7 "......, akampulizia puani pumzi ya uhai; akawa nafsi hai, mwili unapotengana na roho ndiyo tunaita kifo, hivyo kwangu mimi mtu anapofariki halafu watu wanasema amekata roho au Mungu aipumzishe roho ya marehemu sielewi maana yake  

Kinachotokea mtu anapofariki ni roho yake inarudi kwa Mungu aliyeiumba na ndiyo maana huwezi kusema kila roho itaonja mauti bali unasema kila nafsi itaonja mauti, hivyo suala la kupumzisha roho ya marehemu halipo ila tuna kupumzisha nafsi ya marehemu, siyo kila unachofundishwa au ulichozoea ni sahihi chunguza na kuwa na hamu ya kujifunza vitu utafahamu

Hivyo haina shaka kwamba kama Mungu angekuwa katika hali ya miili kama yetu angebadilika kwa sababu naye angekuwa anafikiria mambo ya kimwili, na kama ni angekuwa na mwili kama wetu angekuwa mzazi na siyo Mungu, ndiyo maana yeyote anayeufuata mwili kamwe hawezi kumpendeza Mungu Warumi 8:6 "Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani

Leo tuishie hapa kesho tutamalizia neno hili la Mungu...

Rafiki katika Kristo Yesu umejionea mwenyewe leo sababu moja muhimu ukijumlisha na za jana zinafika tano za kwa nini Mungu habadiliki, kumbuka Mungu ndiye aliyekuumba anakujua kuliko unavyojijua kwa nini unaufanya moyo wako kuwa mgumu hivyo kumpoke Yesu Kristo? Kama uanaisikia sauti yake pokea neema hii ya wokovu 

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636


No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana