KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 15 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, September 3, 2018

KWA NINI MUNGU HABADILIKI- SEHEMU YA 15

Ev.Tedy Stephen
Ninakusalimu katika Jina lenye uweza la Yesu Kristo, sina shaka moyoni mwangu kwamba wewe ni mzima wa afya na unaendelea vizuri na shughuli zako,  leo tena ni siku njema ya ambayo Mungu ameiandaa kwa ajili yetu ili tumtumikie na kumtukuza


Tumekuwa na kichwa cha somo kubali kubadilika ambacho tumeenda nacho kwa muda wa takribani majuma mawili sasa na bado ninashhudiwa ndani ya moyo wangu kuendelea na somo hili japo kidogo kwa sababu tupo mwishoni mwa somo hili, usichanganywe na kichwa cha habari kwa nini Mungu habadiliki hii ni sehemu iliyopo ndani ya kubali kubadilika 

Tunajiandaa na somo jingine jipya ambalo litaanza karibuni, ni kawaida yangu kwamba huwa sifahamu somo jipya linalofuata mpaka inapofika muda wa kuliandaa hivyo siwezi kukuambia moja kwa moja tutakuwa na somo gani lakini tambua litakuwepo somo jipya katika mtandao huu

Leo nina taarifa muhimu ninayotaka kujadiliana na wewe ambayo ni kuhakikisha unashea neno hili la Mungu, kuvuna nafsi ni kwa namna nyingi kuna watu wengi wameokoka kwa neno wanalolipata katika mtandao huu, wengine wamefunguliwa hivyo usione shida kushea neno hili kwa watu angalu ishirini kwa siku, tizama takwimu za mtandao huu ninakuonesha ili uwe mmoja wa watu wa kusukuma Injili ya Yesu Kristo

Tambua ya kwamba unaposhea neno la Mungu hunifaidishi mimi bali Mungu mwenyewe kwa sababu unamvunia nafsi kama unabarikiwa basi kuwa baraka kwa wengine pia tizama picha hii


Takwimu za jana
Tanzania 737, USA 36, India 31, Sehemu zisizojulikana 19, Kenya 8, Germany 6, France 4 Netherlands 4 and UAE 2  kwa pamoja kama kila mtu anayetembea katika mtandao huu atashea neno linalotoka hapa tutafikia wengi zaidi ya hapa tulipo, sababu malengo ni kufikia watu 40, 000 kabla ya mwaka huu kuisha na ndio tunakaribia 23,000 sasa, hivyo tuna watu 17, 000 zaidi wa kufikia, kuwa balozi mwema wa Yesu katika hili

Siri ni hii siku hizi huhitaji kutengeneza magrupu watu wengi hawapendi kuwa kwenye magrupu ila unaweza kutengeneza broadcast group kila mtu akapata Neno kwa wakati wake ndiyo siri inayotumika sasa, huo ulikuwa mwanzo sasa tuendelee na somo......

Tuliposhia....

Ngoja nikudokeze kitu binadamu anabadilika kwa sababu hajakamilika, tutaendelea kubadilika maadamu tupo kwenye mwili huu wa udongo ambao unabomoka na kumomonyoka, hata siku ya kiama bado tutabadilika lakini badiliko hili litakuwa ni la kuvishwa mwili mpya wa mbinguni 1Kor 15:53-54 "Maana sharti huu uharibikao uvae kutoharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa,.... hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa katika ushindi

Tunaendelea....

Jana tuliona sababu mbili kubwa japokuwa moja niliielezea sana zaidi ya nyingine ni kutokana na muda lakini pia sikutaka kuelezea sana maana ungelichoka kusoma na jana tulikuwa na wakati mzuri sana wa kutizama sababu hizo, kama ulisoma somo la jana asubuhi au hukulisoma tambua ya kwamba lilibadilika mchana hivyo lisome tena upya utaona mabadiliko makubwa ⇒⇒⇒BOFYA HAPA

Sababu ya tatu kwa nini Mungu habadilki..,

Mungu ni Mtakatifu, utakatifu kwangu mimi ninaona ndiyo sifa kuu kuliko zote ya Mungu, Ufunuo 4:8 ".......Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuweko, aliyeko na atakayekuja maana yake ni kwamba hakuna aliye Mtakatifu kama Mungu tangu uasili wake yaani aliyekuweko kwa sababu twafahamu ya kwamba Mungu hana chanzo, lakini pia hakuna atakayekuja tokea kuwa Mtakatifu kama Yeye ndiyo maana ya atakayekuja

Mungu ni msafi na mkamilifu na hachangamani na kitu kingine chochote kile, ukitaka kuufahamu utakatifu wa Mungu tizama katika kitabu cha Mwanzo baada tu ya Adamu na Hawa kutenda dhambi hakuwavumilia aliwaadhibu kwa sababu walikuwa wachafu mbele zake na hakuona sababu ya kuendelea kua karibu nao akauondoa uwepo wake mbele zao

Ndio maana njia rahisi sana na ya haraka ya kuupata uwepo wa Mungu katika maisha yetu ni kujitakasa na dhambi zetu, Mungu kwa ajili ya utakatifu wake pia aliangamiza dunia mbili zilizopita kabla ya dunia tuliyopo sasa zilitenda dhambi na zikawa chukizo kwa Mungu

Hata sisi tungeshaangamizwa kama siyo Yesu Kristo kuja kutukomboa kutoka kwenye dhambi yetu ya asili na matendo yetu maovu, ndiyo maana moja ya zawadi kubwa kupita zote ya Mungu kwenye maisha yetu ni wokovu, mkumbatie sana rafiki yako anayekusisitiza kwenda Sayuni

Vitu ambavyo siyo vitakatifu pekee ndiyo vinabadilika baada ya muda fulani kwa sababu ya kukosa ukamilifu, binadamu baada ya muda anaweza kuwa siyo Mtakatifu kwa sababu ya dhambi, ila ana nafasi ya kutubu na kuwa mtakatifu tena Mithali 28:13 "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema

Hivyo utakatifu ni kuwa halisi, ni kile ambacho umesema lazima utakifanya, ni kutokuwa na uchafu mawaa wala kosa lolote ndani yako, utakatifu wa Mungu ndio unaomfanya asibadilike kwa sababu umemkamilisha katika kila idara

Ayabu alifahamu siri ya utakatifu wa Mungu hata kipindi alichokuwa katika majaribu hakuthubutu kuunyanyua mdomo wala ulimi wake kuongea neno lolote la kumuudhi Mungu Ayubu 6:10 "Hapo ndiyo ningefarijika hata sasa; Naam ningejikuza katika maumivu yasiyoniacha; Kwa kuwa sikuyakana maneno yake Mtakatifu

Tambua ya kwamba tunasujudu na kumtukuza Mungu kwa sababu ni Mtakatifu, siku Mungu akibadilika tuu ina maana anapoteza sifa ya kupata mambo haya kutoka kwa binadamu na kamwe usikae utarajie Mungu atapingana na neno lake, kwa sababu ni Mtakatifu sana na hauwezi kamwe kuuelezea utakatifu wake

Zaburi ya 99 kaisome nanukuu mstari wa 9 "Mtukuzeni BWANA, Mungu wetu; sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana BWANA, Mungu wetu ni mtakatifu

Sababu ya nne kwa nini Mungu habadiliki..,

Watu wasingemuamini, hii inajumuisha Mimi Humphrey Makundi ningeongoza maandamano haya ila ya kisiasa tusitafutane, ninaandika hivi sababu ninajua Mungu wangu hawezi kubadilika, Mungu siyo mwanasiasa Mungu wangu ni Mfalme anasema anachomaanisha, ngojea nikueleze kitu hapa kuhusu Mungu hata ukatae kumuabudu bado ataendelea kuwa Mungu huifanyi nafasi yake kubadilika na ninaandika hivi baada ya kujifunza ni kuelewa vitu kwa upana na marefu 

Elewa hivi kama binadamu mwenzako akiwa na tabia ya kuenda kinyume na makubaliano mnayofikia tayari unaanza kumuona muongo na unaenda mbali na kusema ni msanii au unasema ana maneno mengi au kageuka mwanasiasa unafikiri hali ingekuwaje kwa Mungu ambaye haumuoni si ndiyo ungemkashifu na kumtukana kabisa? Ndiyo maana nakuambia kamwe Mungu hawezi kubadilika

1Yoh 4:20 "Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake anayemuona; hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumona soma tena hili neno lirudie mara tatu, kisha litafakari linamaanisha nini

Fahamu ya kwamba ukiweza kuwa na uelewa mpana wa neno la Mungu inakuwia rahisi sana kumwamini Mungu na unakuwa na uhakika wa kumkamata kwa nguvu mpaka akupatie baraka zako, Yakobo alilifahamu hili alimfahamu Mungu wake hata alipopigana mieleka na malaika hakumwacha aondoke kizembe alimkamata mpaka akambariki, ndiyo ufahamu ninaotamani kila mtu aupate ndiyo maana ninasisitiza kushea kila neno la Mungu unalosoma

Maana yake ni kwamba Mungu ni mwaminifu na anakuamini wewe mungu ili uweze kumpenda Yeye ni lazima umpende ndugu yako unaemuona kumbuka Mungu ni Roho na hatumuoni kwa macho ya mwili ila tunaona nguvu na matendo yake maishani mwetu, kama anaweza kusema maneno makali kiasi hiki kamwe hawezi kubadilika

Usishangae nimesema wewe ni mungu ndiyo wewe ni mungu kwani mfano wa meza si meza, mfano wa gari si gari na mfano wa Mungu si mungu au umesahau neno hili Mwanzo 1:26 "Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale...... maana yake ni kwamba wewe ni mungu mdogo tafadhali tizama matumizi ya herufi kuna M kubwa na m ndogo 

Tizama tena Zaburi ya 82:6 "Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye Juu, enyi nyote wakati mwingine ili kulielewa neno tizama matumizi ya herufi kubwa na ndogo katika sentensi maana ndiyo yanatafasiri na kuweka mkazo juu ya neno husika, ukitizama hapo Aliye Juu zote zina herufi kubwa inamaanisha ni nje ya dunia, jambo jingine kuna matumizi ya neno Ndiyi inamaanisha wingi lakini miungu ni herufi ndogo hivyo kila mtu ni mungu 

Kudadavua zaidi imeandikwa miungu kwa sababu ni wa aina mbalimbali, tumepewa karama tofauti na Mungu unakuwa mungu kwenye eneo ulilopewa ila kwa sababu ni maeneo tofauti ndiyo maana limetumika neno miungu kujumuisha mungu katika maeneo mbalimbali

Warumi 12:6-8 "Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa ni nabii tutoe unabii kwa kadiri ya imani, ikiwa ni huduma tuwepo katika huduma yetu; mwenye kufundisha katika kufundisha kwake, mwenye kuonya katika kuonya kwake; mwenye kukirimu kwa moyo mweupe; msimamizi na asimamie kwa bidii; aliyerehemu na arehemu kwa furaha

Ninatumaini hata wewe upo kwenye moja ya karama hizo, na umeshaifahamu sehemu yako na unaifanyia kazi kwa bidii na nguvu zako zote, maisha ni mabaya sana kama unafanya kitu nje ya kusudi la kuumbwa kwako, usitumie nguvu nyingi kutafuta hela, tumia nguvu na akili kutafuta kusudi, kisha songa mbele na kusudi hilo mwishoni lazima litaongea cha muhimu usiache kulifanyia kazi na mwamini Mungu

Tuishie hapa leo tutaendelea kesho....

Rafiki katika Kristo Yesu umejionea mwenyewe leo sababu mbili muhimu ukijumlisha na za jana zinafika nne za kwa nini Mungu habadiliki, kumbuka Mungu ndiye aliyekuumba anakujua kuliko unavyojijua kwa nini unaufanya moyo wako kuwa mgumu hivyo kumpoke Yesu Kristo? Kama uanaisikia sauti yake pokea neema hii ya wokovu 

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana