KWA NINI MUNGU HABADILIKI?- SEHEMU 14 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Sunday, September 2, 2018

KWA NINI MUNGU HABADILIKI?- SEHEMU 14

Co-Founder at MT Pendo Wisso 
Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu, nina imani ndani ya moyo wangu kwamba wewe ni mzima wa afya na unaendelea vyema na kazi zako, hata mimi pia ninaendelea vyema kwenye kazi ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazarethi

Huu ni mwanzo wa juma jipya la mwezi wa tisa na ni kawaida Mungu kuwa na baraka mpya kwa kila mwezi kwa sababu Mungu ni wa mabadiliko japokuwa yeye habadiliki, leo kipekee kabisa tunajifunza somo muhimu kwa pamoja ambalo litakupatia mwanga kwa nini Mungu habadiliki

Kama hukusoma neno la Mungu lililopita la kubali kubadilika sehemu ya kumi na tatu ⇒⇒BOFYA HAPA KULISOMA

Tulipoishia.....

Sehemu yoyote ambayo hakuna maarifa kuna giza, ndiyo maana kutafuta maarifa ya neno la Mungu kwa nguvu zako zote katika kipindi hiki ndiyo jambo jema zaidi unaloweza kulifanya kuliko kitu kingine chochote kile kwenye maisha yako

Tunaendelea.....

Katika masomo yaliyopita nimekuwa nikifundisha mara kadhaa kwamba Mungu ni wa mabadiliko lakini Yeye habadiliki, kama anayapenda mabadiliko na habadiliki ni lazima kutakuwa na siri kubwa kwa nini habadiliki, katika somo la leo nilipata ufunuo wa baadhi ya sababu kwa nini habadiliki na ndio nitakaojadiliana nawe katika mtandao huu

Mungu katika Biblia amejitambulisha kama mfalme, kama ulikuwa hufahamu ni kwamba neno la mfalme ni sheria wakati Bwana Yesu alipoianza Injili maneno yake ya kwanza yalikuwa ni haya Mathayo 4:17 "Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia; unayapata maneno haya pia katika Marko 1:15 " akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni, na kuiamini Injili

Utawala wa kifalme upo tofauti kabisa na utawala wa kidemokrasia na ndiyo maana nilifundisha siku moja na kusema dini siyo demokrasia unapoona watu wanapiga kura kuhusiana na masuala ya kiroho kuna matatizo makubwa, neno la mfalme ni sheria hata mfalme mwenyewe hawezi kulipinga kwa sababu mfalme haongei hovyo anachoongea ni uhai

Biblia imeweka wazi ya kwamba neno la Mungu ni kama upanga ukatao kuwili, maana yake ni kwamba linafanya mambo makuu mawili kwa wakati mmoja, yaani linabariki na kulaani, linatoa uhai na kuuwa na pia linamhukumu aliyelitamka na aliyelipokea, Mungu anahukumiwa kwa neno lake mwenyewe

Hapa sichezi na maneno ila ninakufundisha kitu ambacho Roho Mtakatifu alinifundisha peke yake tizama Waebrania 4:12 " Maana neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyoko ndani yake; tena ni jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo

Hivyo neno la Mungu linamuwajibisha Mungu mwenyewe na linamuwajibisha mwanadamu kama kiumbe chake, tizama tena upanga ukatao kuwili yaani kwake na kwetu ni lazima Mungu awajibike kwa neno lake Malaki 3:6 "Kwa kuwa mimi BWANA sina kigeugeu ndiyo maana ninyi hamkuangamizwa enyi wana wa Yakobo

Maana yake ni nini? Mungu asingeliweza kuacha kuwafikisha wana wa Israeli nchi ya Ahadi japokuwa walikuwa wamemuudhi kwa kuabudu miungu mingine na kukosa imani kwake, hii ni kwa sababu maneno yake yalimhukumu, kumbuka alimuahidi Abrahamu kwamba uzao wake utairithi nchi ile hivyo alifungwa na maneno yake mwenyewe kama mfalme

Mwanzo 17:7-8 "Agano langu nitalifanya imara kati yangu na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kuwa nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako, Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayokaa kama mgeni, nchi yote ya Kaanani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao

Mungu anajua ya kwamba kwa maneno yake mwenyewe anahesabiwa haki Mathayo 12:37" Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa; siku Mungu akibadilisha neno lake ni lazima tutamhukumu, hivyo kamwe hawezi kubadilika atakuwa anajipinga mwenyewe

Hii ndiyo maana Mungu pia anajifunua kwetu kama Mungu mwenye haki Zaburi 11:7 "Kwa kuwa BWANA ni mwenye haki, Apenda matendo ya haki, wanyofu wa moyo watauona uso wake, tizama tena Zaburi 145:17 "BWANA ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye huruma katika matendo yake yote

Haki ya Mungu ipo kwenye nini? Ipo katika Neno lake mwenyewe ndiyo maana kila ukitubu kuna msamaha wa dhambi, anatimiza ahadi zake, wanaomtafuta kwa moyo wao wote wanamuona, anawafundisha watumishi wake neno lake, anaonesha haki yake kwa namna anavyoongoza lakini ukumbuke mwenye haki anaishi kwa Imani katika Yesu Kristo

Mfalme yeyote akiwemo Mungu mwenyewe ambaye ndiye Mfalme wa wafalme huwa analiangalia neno lake linasemaje, ndiyo maana ni hatari sana kuwa na maombi ambayo hayana neno la Mungu kwa sababu kamwe hawezi kukujibu kitu kilicho nje ya neno lake Yeremia 1:12 "Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vyema, kwa maana naliangalia neno langu, ili nilitimize

Mtakumbuka habari za Danieli na Mfalme Dario, wakati washauri wa mfalme Dario walipomuonea wivu Danieli kwa hekima na namna ambavyo Mfalme alivyokuwa anampenda waliamua kula njama ya kwenda kumshawishi mfalme apitishe sheria ya kila mtu kutoabudu Mungu wa kweli bali waabudu mungu wa Dario na atakayekutwa anafanya kinyume na hilo atastahili kuuwawa

Danieli 6:4 "Basi mawaziri na viongozi wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu; wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake

Tizama tena kwa makini neno lililotumika katika mstari huo la kumshitaki Danieli kwa habari za ufalme, hivyo kuna namna maalumu ya kumshitaki mtu linapokuja suala la kifalme, haushitaki kizembe zembe tuu kuna utaratibu ambao ni kupitia neno la mfalme

Ninapenda zaidi  Danieli 6:5  unaelezea zaidi juu ya Danieli "Ndipo wale watu wakasema hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake, sheria ya Mungu ni neno lake

Walifanikiwa katika suala lao hili na mfalme Dario alipitisha sheria, kumbuka Danieli alikuwa muaminifu kwa Mungu kaasi ambacho hakuacha kuomba mara tatu kwa siku akigeukia Yerusalemu na walijua ya kwamba watamnasa katika neno hili na walifanikiwa kufanya hivyo, kwa sababu neno la mfalme ni sheria na hakuna wa kulibadilisha Danieli aliandaliwa kuwa kitoweo cha Simba

Mfalme Dario alikuwa anampenda Danieli kwa sababu ya hekima na busara zake alianza kutafuta namna mbalimbali za kupindisha sheria lakini ilishindikana kabisa kwa sababu neno la mfalme ni sheria hata baada ya kukusanya timu nzima ya washauri wake na mwishoni aliandaliwa kuwa kitoweo maalumu kwa ajili simba

Danieli 6:14 "Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli, akajitaabisha kumuokoa hata jua likachwa, hakufanikiwa katika hili

Siku ambayo Mungu atabadilika ndiyo siku ambayo mtaanza kumshitaki kwa kukiuka neno lake kwa sababu neno la Mungu ndiyo Mungu mwenyewe na kamwe hawezi kuenda kinyume na neno lake kwa sababu ndiyo sheria

Pia mshitaki wa kwanza wa wanadamu ni Shetani Ufunuo 12:10 "Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, sasa kumekuwa wokovu, na nguvu na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele ya Mungu wetu, mchana na usiku

Swali la kujiuliza ni kwamba Shetani anatushitaki namna gani kwa Mungu? jibu ni hili ni kupitia neno la Mungu ambalo ndiyo sheria ya Mungu kwa sababu Mungu hawezi kwenda kinyume na neno lake, tizama hapo neno linasema mshitaki wa ndugu zetu ndugu za Mungu ni wewe na mimi kwa sababu Mungu ametuumba kwa sura na mfano wake

Luka 8:20-21 "Akaletewa habari akaambiwa, mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe, Akajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ni hao walisikiao Neno la Mungu na kulifanya, kwenye kulishika neno hatua ya kwanza ni kuokoka, hivyo kama hujaokoka kuna nyimbo hupaswi kabisa kuziimba kama ile ya Yesu ni rafiki yangu, sio dhihaka ila ni kwa sababu huna sifa kulingana na neno

Hatari ni kwa watu wote ambao bado wanaishi katika nchi hii, na kama hufahamu ni kwamba mtu yeyote ambaye hajaokoka anaishi duniani wengine wote waliookoka wanaishi katika ulimwengu mwingine wa kiroho juu kabisa ya kila ufalme, mamlaka, na nguvu na utawala siyo maneno yangu bali ya Mungu mwenyewe Waefeso 1:20-22 "alilolitenda katika Kristo alipomfufua katika wafu akamweka katika upande wake wa kulia katika ulimwengu wa roho, juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka na nguvu na utawala, na kila jina litajwalo, wali si ulimwenguni humu tuu, bali katika ule ujao

Unapookoka maana yake ni kwamba unaamishwa katika ulimwengu huu na kupelekwa katika ulimwengu mwingine juu zaidi ya huu ndiyo maana katika wokovu tunamkiri Yesu Kristo ili sehemu alipo na sisi tuwepo naye na tunakuwa katika kiwango sawa na Yesu tunaweza kutenda neno lake na kushinda mambo yanayowaogopesha wengine

Tizama ambao hawajaokoka neno linavyosema ufunuo 12:12 "Kwa hiyo shangilieni enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu akiwa na ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tuu, unashangaa kwa nini unaogopa wachawi, unashangaa kwa nini baharini kuna majini na pepo wachafu jibu umelipata leo, ni mpaka uhame katika ulimwengu huu ndiyo utakapoweza kumshinda Shetani

Sababu ya pili ya kwa nini Mungu habadiliki ni;

Mungu amekamilika haitaji chochote, yeye ndiyo kila kitu na kila kitu kimeumbwa naye, kitabu cha Injili ya Yohana mlango wa kwanza kimefunua siri hii ya ajabu kuanzia mstari wa kwanza mpaka wa tano kwa faida yetu nitakukuu maneno yote

Yohana 1:1-5 "Hapo mwanzo kulikuwako na Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu, Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika, Ndani yake ndimo ulikuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu, Nayo nuru iling'aa gizani, wala giza halikuiweza

Hivyo fika unaona hapo kila kitu ni Mungu alikiumba na pasipo yeye kuwepo hakuna kitu kilichofanyika, tunamlilia Mungu katika shida zetu kwa sababu ni yeye pekee anayeweza kutuokoa Zaburi 107:6,13,19,26 "Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, akawaponya na shida zao, ni Mungu pekee ndiyo mwenye uzima, ina maana nje ya Mungu hakuna uzima wala hakuna mwanga 

Ngoja nikudokeze kitu binadamu anabadilika kwa sababu hajakamilika, tutaendelea kubadilika maadamu tupo kwenye mwili huu wa udongo ambao unabomoka na kumomonyoka, hata siku ya kiama bado tutabadilika lakini badiliko hili litakuwa ni la kuvishwa mwili mpya wa mbinguni 1Kor 15:53-54 "Maana sharti huu uharibikao uvae kutoharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa,.... hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa katika ushindi

Ninatamani kuendelea lakini leo tuishie hapa, kesho tutaangalia sababu zingine kwa nini Mungu habadiliki........

Rafiki katika Kristo Yesu umejionea mwenyewe leo sababu mbili muhimu kwa nini Mungu habadiliki, kumbuka Mungu ndiye aliyekuumba anakujua kuliko unavyojijua kwa nini unaufanya moyo wako kuwa mgumu hivyo kumpoke Yesu Kristo? Kama uanaisikia sauti yake pokea neema hii ya wokovu 

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636




No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana