KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA 13 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Friday, August 31, 2018

KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA 13

Humphrey Makundi MD at MT

Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo Bwana wetu, nina imani kwamba ni mzima wa afya na unaendelea vyema, karibu tena katika wakati mzuri wa kujifunza neno la Mungu lenye nguvu pamoja nasi, Roho Mtakatifu aliye mwalimu mwema akufundishe na kukufunulia ujumbe ambao ameuandaa kwa ajili yako siku ya leo

Leo tutaendelea na somo letu la kubali kubadilika sehemu ya kumi na tatu kama hukusoma mfululizo huu wa masomo haya mpaka tulipofikia au hukusoma sehemu ya kumi na mbili⇒⇒⇒ BOFYA HAPA KUISOMA


Tulipoishia...

Ili mambo yabadilike ni lazima nibadilike, mabadiliko yanaanza na mimi na hiki ndicho ninakiita majukumu kwa lugha ya kiutu uzima, naam! ni uwezo wa kubadilika na kukubali kwamba ni jukumu langu kwa asilimia 100% kubadili kila kitu nisichokipenda kwenye maisha yangu, badala ya kulaumu, kuangalia sababu za nje, nachukua hatua na kuongeza bidii zaidi

Tunaendelea leo...

Mabadiliko/ kubadilika kunamaanisha kwamba tunaishi na mabadiliko yanayapa maisha uhai, tuliona kwamba Mungu ni wa mabadiliko lakini yeye habadiliki, hivyo hata kama umeoa au kuolewa halafu hamjapata mtoto jua sio mpango wa Mungu, ndoa ni kwa ajili ya uzao na uzao ni mabadiliko na kwamwe huwezi kuniambia unamuamini Mungu halafu ukose uzao haiwezekani, ni haki yako kiungu

Mwanzo 1:29 "Mungu akawabariki, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi

Kubakia sehemu ile ile baada ya kuoa ni sawa na kufa na hii haijalishi kwamba bado unaishi kimwili, kuoa ni mabadiliko kiasi ambacho haupaswi kuoa ukiwa katika nyumba ya Baba yako Mwanzo 2:24 "Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja 

Baba wa Imani Abrahamu hakubarikiwa mpaka alipoondoka kwa Baba yake Mwanzo 12:1 "BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonesha

Kuondoka kwa Abramu sehemu aliyokuwepo ni kubadilika, kuna sehemu ukikaa ni vigumu sana kubadilika, kuna baadhi ya marafiki ukiwa nao ni vigumu sana kubadilika ndiyo maana ni lazima kuwa makini na watu ambao unakuwa nao karibu kwa sababu ndiyo watakaochochea mabadiliko yako au laa

Usitengeneze urafiki na mtu ambaye haamini unachokifanya au anakidharau au kuoa mke asiyeamini maono uliyokuwa nayo sababu atakuzuia kufikia kile unachotamini kukiona katika maisha yako, jiweke karibu na watu wanaokupa hamasa ya kufanya zaidi na wale ambao mnafanya vitu vinavyofanana

Yesu Kristo alilifahamu hili hakutaka mlolongo wa marafiki, alikuwa na wanafunzi kumi na mbili pamoja na mtu mmoja tuu aliyetambulishwa kama rafiki yake ambaye ni Lazaro hivyo kuwa makini sana, alifahamu fika Injili aliyokuja kuihubiri ingefanikiwa kwa watu hao pekee

Yohana 15:14 "Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo, hivyo sasa hivi mtu yeyote anayetenda sawa na Neno la Mungu ndiyo anakuwa rafiki wa Yesu kama wanafunzi wake, na ndiyo mtu aliyebadilika hii inatupa picha ya kutambua kwamba wale wanaoenda tunakoenda ndiyo marafiki zetu wakubwa

Kukubali kubadilika ni kuwa kama mawimbi, kila wakati unajisukuma mbele kuelekea ng'ambo sehemu ambako baraka zako ziko, unapopaswa kubadilika halafu haubadiliki unaenda kinyume na mawimbi, mtumbwi au meli iayoenda sawa na uelekeo wa mawimbi huenda kiurahisi na kiuwepesi kuliko inayoenda kinyume na mawimbi

Kukubali kubadilika ni kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kizazi kijacho, naam ni kujitoa kwa ajili ya wengine kwa mfano watu kama Isaack Newton, Thomas Edson hawa walibadilika walikuwa tayari kutumia muda wao wote kuchunguza vitu mbalimbali vihusuvyo sayansi na leo tunafurahia mbegu ya mabadiliko Mungu aliyoipanda ndani yao

Tambua ya kwamba akili yako siyo kisiwa bali ni bahari, kisiwa kina kikomo lakini akili ya binadamu haina ukomo unaweza kujaza mbegu yoyote ile ndani yake na ikaleta mabadiliko, kwani aliyetengeneza ndege alikuwa anafikiria nini? Hivi umeshawahi kwenda feri na ukaona zile meli za kubeba mizigo zilivyo kubwa? wale waliotengeneza wana akili gani? umeumbwa kwa ajili ya matendo makuu na ya ajabu lakini ni mpaka ubadilike ndiyo utayaona

Ukweli ni kwamba ni mwanaume aliyekataa kubadilika anafikiria kula, kuvaa na kunywa hata anashindwa kuwaachia wana wa wanae urithi, Mithali 13:22 "Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, kama unategemea usomeshe watoto wakusaidie umepotea badilika kuanzia sasa kusomesha mtoto ni jukumu lako ila mtoto wako siyo mtaji wa baadae ndiyo maana akifikia kuoa anaondoka kwako

Muda unathibitisha kwamba mabadiliko ni halisi, pasipo muda hatuwezi kuona udhihirisho wa mabadiliko kwa sababu yanahitaji muda kuweza kuonekana, mabadiliko hupandwa katika akili na huzaa baada ya muda

Mabadiliko siyo maigizo, wala siyo mtindo wa kutafuta aina fulani ya maneno ya kuongea ili kufurahisha watu, kukubali kubadilika ni matendo, katika jamii ya sasa ninaona kumetokea upepo wa watu wanaojiita wahamasishaji wanawaambia watu vitu vya kufanya wakati hao hawafanyi na wengine hata hawavifahamu, kitu unachomwambia mtu halafu hukifanyi hakina nguvu

Huwezi kumlazimisha mtu kubadilika kwa kumpeleka sehemu ambayo mtu hataki kwenda tambua hili mapema, mtoto wako akiwa mvuta bangi kumtafutia chuo cha ujakonia siyo suluhisho la kubadilisha tabia mbaya aliyokuwa nayo baada ya muda atarudia kule alikokuweko, kumbuka nimekuambia mabadiliko ni mbegu yanapandwa kwenye akili, ni mpaka akili ya mtu ikubali ndipo anapobadilika

Huwezi kutumia nguvu kushindana na mtu ambaye ameamua kubadilika kwa sababu nguvu ni zao la mwili na mabadiliko ni zao la akili, ni vitu viwili tofauti, Danieli hakuacha kuomba mara tatu kwa siku hata baada ya sheria ya mfalme kukataza kuacha kumtumikia Mungu wake, na alivyowekwa katikati ya simba Mungu wake aliyemtumainia alimtunza na hakuraruliwa na simba

Danieli 6:22 "Mungu wangu ametuma malaika wake, naye amevifunga vinywa vya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana ya kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno

Hata ujinga unaposhamiri haumzuii mtu anayetaka kubadilika au aliyabadilika, kumbuka ya kwamba kwenye nchi ya vipofu anayefanikiwa kuwa chongo anakuwa mfalme, hivyo usichukulie mabadiliko yatakupata ukiwa katika nchi fulani hapana! Mungu amekuweka hapa kwa sababu unapaswa kuwa hapa toa hizo fikra potofu za mpaka uende ulaya

Sehemu yoyote ambayo hakuna maarifa kuna giza, ndiyo maana kutafuta maarifa ya neno la Mungu kwa nguvu zako zote katika kipindi hiki ndiyo jambo jema zaidi unaloweza kulifanya kuliko kitu kingine chochote kile kwenye maisha yako

Tutaendelea tena week end njema.......


Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana