KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA 12 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, August 30, 2018

KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA 12

Humphrey Makundi MD at MT
Bwana Yesu asifiwe! Namshukuru Mungu kwa ajili ya muda huu ambao ametupatia mimi na wewe kuweza kujifunza neno lake, tunaendelea na neno tuliloliendeleza juma hili la kubali kubadilika na leo tunaangalia sehemu ya kumi na mbili ya somo hili

Ninaomba Roho Mtakatifu aliye mwalimu mwema akakufundishe muda huu kile ambacho amekusudia kukufundisha, na Mungu akupatie hekima ya kuweza kukifanyia kazi ili uweze kupata matunda yake katika Jina la Yesu Kristo, Amen

Tulipoishia....

Nimalizie leo kwa kusema kwamba njia rahisi sana ya kutaka kubadilika ni kuanza kujifunza na kujijaza na maarifa ya eneo ambalo unataka kubadilika, ukiwa na maarifa ya kutosha una uhakika wa kubadilika katika eneo hilo, sehemu yoyote unayoteseka ni kwa sababu hauna maarifa


Kama hukusoma somo la jana la kubali kubadilika sehemu ya kumi na moja unaweza ⇉⇉⇉KUBOFYA HAPA KUISOMA

Tunaendelea...

Ninaomba ufahamu kwamba hakuna Neno linaloandaliwa katika mtandao huu kwa bahati mbaya, chochote unachokisoma hapa kina pumzi ya  Roho Mtakatifu, unahitaji kuwa makini sana ili kupata neno lako na lifanyie kazi, utageuka mpumbavu kama unafurahishwa na huduma hii lakini haufanyii kazi Neno la uzima linalotolewa

Jana nilisema kwamba mimi nina ukichaa wa Imani, ninamuamini Mungu na neno lake nilikuwa ninamaanisha sikuwa najisifu peke yangu la hasha! Ninamsifu Yesu wangu, huu uchizi wangu kwa Yesu ndiyo unaonifanya ninaandaa masomo haya mara tano kwa juma unapata maziwa na chakula  katika mtandao huu

Ni mimi na wewe tusababishe mabadiliko au mabadiliko yatusababishe, binadamu hapelekwi na upepo bali matawi ya mti na vitu, hatusubiri mpaka tsunami ipige ndio tufahamu kuna upepo mkubwa na wa ajabu bali tunajifunza na kufahamu namna ya kujikinga utakapotokea ili tuweze kuenenda nao


Tumeachiwa jukumu la kuamua ni nini kitatokea kwenye maisha yetu, ninakupasha habari hili siyo jukumu la Mungu, ndiyo maana una utashi na akili ya kutambua mema na mabaya katika maisha yako, ni mpumbavu ambaye anajifunza halafu hafanyii kazi anayojifunza, unahesabiwa kuwa mwerevu ukitafuta maarifa na kuyafanyia kazi


Hatubadiliki ili kuwafurahisha watu au jamii yetu, tunabadilika ili kuweza kuwa chanzo cha matokeo makubwa yanayohitajika katika maisha yetu, na pia sababu tumetambua kwamba mlima wa maisha ya mtu ni ujinga wake 


Marko 11:23 "Amin, nawaambia, yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake


Hauwezi kuyakimbia mabadiliko, kama haujafahamu siri ni hii hata unaposoma hapa unabadilika lakini itakuchukua muda kuona hili likidhihirika katika maisha yako rudia tena na tena masomo haya utasadiki ninachokuambia


Mabadiliko hayatokei kwa kujifunza kitu mara moja, unajifunza tena na tena, hivyo usiridhike kusoma neno la Mungu mara moja bali kula neno la Mungu kabisa kwa sababu neno la Mungu ni chakula cha uzima 


Yeremia 15:16 "Maneno yako yalionekana, nami nikayala, na maneno yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe moyoni mwangu; maana nimeitwa kwa jina lako Ee BWANA, Mungu wa majeshi


Unapofikia hatua ya kula neno la Mungu na siyo kulisoma tuu neno unageuka kuwa muujiza unaoishi, anza kuhama kutoka kwenye kusoma neno tuu na kuishia hapo nenda hatua nyingine ya kulitafakari neno na hatua ya juu kabisa ni kulila neno


Daudi aliweza kupigana vita vingi na kuleta mabadiliko mengi kuliko mfalme yeyote yule katika Israeli, Mungu alifikia hatua ya kumuita rafiki yake akaona haitoshi akaamua kumleta Yesu Kristo mwana wake wa pekee kupitia ukoo wake kwa sababu Daudi alikuwa amebadilika na alikuwa na ukichaa kwa Mungu, upendo wake haukupimika


Mwanaume ambaye ndoa inamshinda ni kwa sababu hajataka kubadilika na kumpenda Mungu kwa sababu upendo ulionao kwa Mungu ni sawa na upendo ulionao kwa mke wako chunguza hili utafahamu hili


Waefeso 5:25" Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake; unashangaa kwa nini hupendwi jibu hili hapa mama, kama anampenda Kristo hawezi kuacha kukujali na kukutunza


Mabadiliko yanamfanya mtu aweze kukabili hali itakayojitokeza katika maisha, kumbuka kwamba nilikuambia jana mabadiliko ni kuichungulia baadaye sasa, kisha unaanza kuiishi na kuifanyia kazi kwa kumwamini Mungu na neno lake


Wazee wote wanaolalamika na kusingizia watoto wao hawawajali ni wale ambao walikataa kubadilika, waliishi kwa kula na kuvaa na hawakufikiria la zaidi ya hapo, walihubiriwa habari za Yesu wakapuuzia waliikataa kweli na sasa katika uzee wamekosa uhuru


Mimi nimeshafanya uamuzi wa kubadilika na nitake au nisitake maadamu nimebadilika ni lazima nitapata kila kitu ninachokihitaji, lazima nitaenda kila ninapopaswa kuenda, lazima ninayemtangaza atajulikana, kwa sababu nimeamua kubadilika na ameahidi kuwa pamoja na mimi


Sikushikiwa fimbo na mzazi, hakuna aliyenishauri bali niliamua mwenyewe ogopa sana nguvu ya mtu aliyenuia kufanya kazi ya Adamu wa pili, atatoboza kila mahali hata katikati ya mwamba nitapita na hakuna atakayenizuia, sijui unapitia hali gani lakini ninachokifahamu kuna ufumbuzi wa kila jambo swali ni Jee upo tayari?

Tambua ya kwamba mazoea na tabia uliyojitengenezea yalikufikisha hapo, ukitaka kwenda mbali zaidi ya hapo badili tabia na mazoea uliyokuwa nayo, mtu mmoja akasema ukitaka kuwa masikini ambatana na masikini na ukitaka kuwa tajiri ambatana na matajiri Wakati mwingine kuacha njia za zamani huwa ni kitu kugumu zaidi kufanya na hii ni sababu huwa tunahofia vitu vilivyo mbeleni, lakini kwa kuacha mazoea na tabia za awali ndio njia ya kufungua njia mpya na kukupeleka sehemu nyingine yenye milango ya utele na baraka kwenye maisha kwa ajili yako. Vitu ambavyo huvifahamu ndio vina nguvu ya kukubadilisha, umefika ulipo kwa sababu ya taarifa unazozifahamu ukipata taarifa nyingine mpya za kuushibisha ubongo wako una uhakika wa kufungua mlango wa utele na kupata vitu vya thamani maishani mwako
Hili ni moja ya jambo rahisi na lepesi sana lakini wengi hawathubutu kufanya hivyo kwa sababu wameridhika na hali walizonazo na pia wametawaliwa na hofu ya sehemu ambayo wanayotaka kuiendea, tunaweza kuishinda hofu kwa kuwa na maarifa na ufahamu
Hali hii imezuia watu wengi kupata mabadiliko wanayoyataka pamoja na kufikia hatma ya utukufu Mungu aliyowaandalia lakini mwisho wa siku swali la kujiuliza ni nani wa kumlaumu katika kila kitu maishani mwangu? Bila shaka NI mimi peke yangu, siyo mzazi wangu, wala rafiki zangu wala ndugu zangu Hakika sasa nimepata ufahamu mpya na kutambua ya kwamba binadamu wa kwanza ninaepaswa kumteka ni mimi Plato akasema "For a man to concquer himself is the first and nobest of all victories" Ili mambo yabadilike ni lazima nibadilike, mabadiliko yanaanza na mimi na hiki ndicho ninakiita majukumu kwa lugha ya kiutu uzima, naam! ni uwezo wa kubadilika na kukubali kwamba ni jukumu langu kwa asilimia 100% kubadili kila kitu nisichokipenda kwenye maisha yangu, badala ya kulaumu, kuangalia sababu za nje, nachukua hatua na kuongeza bidii zaidi

Itaendelea .......

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana