KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA 11 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, August 29, 2018

KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA 11

Humphrey Makundi MD at MT

Ninatanguliza salamu zangu kwako kwa Jina lipitalo majina yote Jina la Yesu Kristo, ninatumaini unaendelea vyema na ninakulialika tena leo tuweze kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kwa ajili ya utukufu wa Mungu

Nikupongeze unayeendelea na mfungo kama unataka kujumuika nasi ⇒⇒BOFYA HAPA KUPATA MAELEKEZO yote ya mfungo pamoja na sala za mfungo (prayer points),  tulikuwa na somo maalumu la maana ya namba saba kiroho na ninaona katika takwimu lilikuwa na wasomaji wengi sana kama hukulisoma⇒⇒ BOFYA HAPA KUSOMA


Tulipoishia.....

Mabadiliko ni mbegu yanapandwa katika akili, yanakuwa na kuleta ufahamu na maarifa baada ya muda huonekana katika matendo, kisha matokeo hudhihirisha mabadiliko, kitu cha kwanza kabisa kudhihirisha mtu kabadilika ni matendo yake

Jana tuliendeleza somo lenye kichwa cha habari cha kubali kubadilika na tulikuwa sehemu ya kumi kama hukupata fursa ya kujifunza nasi somo hili tafadhali BOFYA HAPA KUJIFUNZA nasi somo hili maalumu

Tunaendelea...

Ukuaji ni mabadiliko, hakuna mtu anayetafuta kurudi nyuma kwenye maisha bali kila mtu anaangalia njia tofauti za kwenda mbele na mabadiliko katika sehemu moja ya maisha yanakuandaa kwa ajili ya mabadiliko katika sehemu nyingine za maisha 

Mungu ameyatengeneza maisha kwa njia maalumu ya kutoka kwenye ubaya kwenda kwenye uzuri na haya ndiyo mabadiliko yenyewe, kama unatoka kwenye uzuri kuelekea ubaya jua uko kinyume na neno la Mungu, kumbuka Siyo sisi tuliomchagua bali ni Yeye aliyetuchangua kwa sababu anatupenda

Tunaitwa kutubu dhambi kwa sababu dhambi hutupeleka kwenye ubaya ambao ni kwenda kinyume na mabadiliko ambayo Mungu anataka yatokee kwenye maisha yetu Mithali 28:13 "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuuziacha atapata rehema

Fahamu ukweli kwamba ni watu ambao wamebadilika ndio wanaoweza kubadilisha wengine,  hivyo usidhubutu kuongelea mabadiliko kama bado hujabadilika, mtu ambaye amerudi kwenye safari ndiye anayeweza kuelezea alikotoka na namna ya kuelekea huko

Yesu mwana wa Mungu aliweza kuhubiri habari njema ya ufalme wa mbinguni kwa sababu ndiko alikotoka Yohana 16:28 "Nilitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; nakwenda kwa Baba

Mbegu ya mabadiliko ndiyo inayochochea na kuhamasisha watu kutengeneza rekodi nyingine katika kazi, taaluma, michezo, biashara, utumishi, fani n.k, ni wale tuu ambao wanaamini wanaweza kutengeneza mambo mapya na kuweka rekodi mpya Yohana 14:12 "Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiaye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba

Suala la kutenda matendo makuu na kubadilisha dunia jukumu umeachiwa wewe na mimi, Yesu alishapanda mbegu zake akaondoka amini nawe uweze kutembea kwenye mtembeo wake na zaidi kwa sababu amesema ukimuamini utafanya na zaidi

Kama umelala huu ni wakati wa kuamka, siyo wakati wa kukubaliana na kila ambacho maisha yanakupatia, umepewa nguvu na mamlaka ya kubadilisha kila hali ambayo hauitaki katika maisha yako na Mungu mwenyewe ni suala la kuamini tuu  na kusonga mbele

Luka 10:19 "Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na n'ge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitakachowadhuru, kila unachohitaji umeshapatiwa ni jukumu lako kukaa chini na kujifunza namna ya kutumia silaha ulizo nazo

Ni mpaka uwe na ukichaa na uchizi wa imani kwa Mungu ndipo unapoweza kuona haya mambo yakitokea, huwezi kufanya kwa sababu hujafikia kiwango hicho, ukifikia utafanya, mimi ni chizi wa imani na ninaliamini Neno, haitachua muda ninachosema kitadhihirika na usiseme sikukuambia

Uchaguzi ni wako ni uamue kuyatengeneza mabadiliko kwa ajili ya kizazi chako na kwa ajili yako, au uwe muhanga wa mabadiliko na uishie kulalamika kila wakati, kwa sababu kuna mambo mawili muhimu ambayo ni wewe kubadilika au ubadilishwe na mabadiliko

Mabadiliko yana chembechembe za imani, yana tabia ya kuvutia wengine kuja kwenye mkondo yanakotokea, unapomuona mtu amebadilika katika suala fulani au amefanikiwa sana katika jambo fulani mara zote ni lazima utataka kuwa kama yeye kinachokuvutia siyo yeye ni yale mabadiliko

Mabadiliko ni lazima yatakuhitaji kuchukua hatua za ziada katika maisha yako, hauwezi kusema umebadilika halafu mwenendo wako ubakie vile vile, ni lazima uchukue hatua ili kuweza kufikia kile ambacho unakihitaji katika maisha yako

Mabadiliko yanahitaji muda ili kuweza kuzaa na kuleta matokeo yanayovutia, siyo suala la kulala na kuamka kila kitu kimekuwa namna unavyotaka, ni suala la mfumo na mchakato katika maisha, unahitaji kubadilisha tabia, kuwa na nidhamu kabla ya kuona mabadiliko

Mabadiliko hayamshangazi mtu aliyejiandaa (it's not a suprise) kwa kuchukua muda wake kuyapangilia na kuyafanyia kazi, ndiyo maana kila mtu aliyefanikiwa kihalali katika eneo fulani anaweza kukuelezea namna alivyofanikiwa

Nimalizie leo kwa kusema kwamba njia rahisi sana ya kutaka kubadilika ni kuanza kujifunza na kujijaza na maarifa ya eneo ambalo unataka kubadilika, ukiwa na maarifa ya kutosha una uhakika wa kubadilika katika eneo hilo, sehemu yoyote unayoteseka ni kwa sababu hauna maarifa

Itaendelea kesho....

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana