"Urejeshewaji utendaji (reciprocity )" ni kanuni inayosema kwamba ukimtendea mtu wema fulani utakuwa umemtwika deni na mbeleni atatafuta namna ya kurejesha fadhila kwa wema uliomtendea
Mwandishi wa Agano jipya Luka aliongelea kanuni hii pale alipomnukuu Yesu akiisema Luka 6:31 "Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo"
Mfano kama unachangia harusi za wenzio uwezekano uliopo ni kwamba na wewe watakuchangia, kama unashiriki matukio ya wengine na ya kwako watashiriki
Lakini utendaji kazi wa kanuni hii huwa una nguvu zaidi pale unapofanya kwa upendo na kutokea moyoni pasipo kutegemea kwamba utarejeshewa mbeleni
Luka 6:32-35 (tafadhali kaisome) "Inaongelea kuwapenda watu wasiotupenda, kuwatendea mema wanaotutendea mabaya, kuwakopesha watu tusiotegemea kitu kutoka kwao, kuwatendea mema adui zetu
Lakini Luka 6:36 inasema "Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma"
Luka 6:37 "Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa"
Kuna vitu vinatuzuia kuchota baraka zetu kwa sababu tuu tumevishika mioyoni mwetu, kuna wema tunaotendea baadhi ya watu kwa kutarajia malipo fulani, Mungu hataki hivyo
Moyoni hukaa vitu viwili tuu cha kwanza ni kumpenda Mungu na cha pili ni kusudi lako vitu vingine vyote hukaa kwenye akili
Ili tuweze kupata kazi mpya au au tufungue biashara mpya ni lazima tuweze kuachilia kazi tulizopoteza au biashara zetu zilizoenda vibaya
Ili kuweza kupata kitu kipya maishani mwako ni lazima uachilie cha zamani ili ipatikane nafasi ya kitu kipya cha aina hiyo au kizuri kupita cha awali
Badala ya kufikiria kusomesha watoto wako na wa ndugu zako fikiria na mtoto wa adui yako aliyekwama kifedha ukamsaidia
Ukiwa ni mtu wa kufanya wema na kufikiri kwamba ni lazima wakati wote na wewe utendewe wema na mtu uliemtendea wema utaumia
Njia za Mungu siyo njia za mwanadamu yeye anataka utende wema kwa kila mtu, kisha ataamua ni mtu gani ambaye atakulipa wema uliomtendea mtu mwingine
Mababu zetu walitambua hili na kusema "Tenda wema nenda zako usisubirie fadhila" sababu saa zingine katika maisha yetu mtu ambaye utamthamini na kumtendea kila lililo jema anaweza kuwa ndiye atakayekuumiza zaidi
Ni vema kufahamu kwamba ukimtendea wema Musa anaweza yeye asirudishe wema uliomtendea bali ukaupata kwa John. Hivi ndivyo jinsi sheria za Mungu zinavyofanya kazi
Mara nyingi sana mtu atakayekusaidia kwenye ndoto yako sio ndugu yako, wala rafiki yako ni mtu mwingine kabisa ambaye hata humfahamu na hii ndio sababu unapaswa kutokumdharau mtu yeyote sababu hujui kabeba nini ndani yake
Baraka na mafanikio tunayoyataka katika maisha yetu zimebebwa na mtu fulani, yaani kuna mtu mmoja tuu akishika simu akiongea na mtu fulani kila mpango wako unakuwa umefanikiwa
Kuna mtu akisema msikilize huyo kijana kipaji chako na ndoto yako inakuwa tayari imepata mwanga mpya
Omba sana Mungu kupata watu wa namna hii, kwa sababu Mungu hutumia mtu kumbariki mtu. Mungu hajawahi kuja duniani kumbariki mtu na haitakaa itokee sababu Mungu ni Roho nao wanaomwabudu yawapasa wamwabudu katika Roho na kweli
Nasisitiza tena usikae ukate tamaa wala kurudi nyuma kwenye kile unachokiamini fanya tuu kuna siku utakutana na mtu mmoja tu na usiku utageuka mchana
Mwanamke Thamani!
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana