JIFUNZE KUSHUKURU - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, January 25, 2018

JIFUNZE KUSHUKURU


Katika maisha yetu siku zote mambo madogo ndio ambayo hukua, hukomaa na kuzaa mambo makubwa. Waswahili wakasema "hata mbuyu ulianza kama mchicha" 

Watu hufikiri ni mpaka mambo yawe makubwa au biashara ikue au wapandishwe cheo na kuwa wakugenzi ndipo wanapopaswa kumshukuru Mungu

Kama unashindwa kumshukuru Mungu kwa faida ya shilingi elfu kumi uliyopata huwezi kumshukuru akikupatia laki moja au milioni

1Wathesonike 5:8  inasema shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu, maana yake ni kwamba haijalishi ni jambo kubwa au dogo, zuri au baya wewe unapaswa kumshukuru Mungu

Kama hukusoma makala ya jana ya tenda wema kwa kila mtu unaweza Kugusa hapa

Hata kama ingekuwa ni majambazi wamevamia nyumbani kwako na wakaiba kila kitu lakini hawakumuuwa mtu hata mmoja wa nyumba yako bado una sababu ya kumshukuru Mungu kwa sababu amekuepusha na kifo wangeliweza kuiba na kukuuwa pia, kuwa na uhai ni sababu kubwa sana ya kumshukuru Mungu

Kila jambo kubwa unaloliona leo hii mwanzo wake ulikuwa mdogo sana, tukienda mbali zaidi ni kwamba lilianza kama dhana fulani kwenye akili ya mtu kisha akalitendea kazi na kadiri siku zinavyozidi kwenda likapanuka na kuwa kubwa

Luka 16:120 "Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia"

Kamwe usikudharau hata faida ya shilingi mia tano unayopata kwenye biashara yako mshukuru Mungu na kesho atakuongezea zaidi sababu yeye ni mwaminifu na wa haki

Lakini pia usidharau mambo ambayo umepewa  na Mungu bure mfano Idea zetu, akili zetu, marafiki zetu, viungo vya miili yetu kwa sababu haya ndiyo chimbuko la kufanikiwa hapa duniani

Ukitaka kuishi maisha mazuri zaidi usipime mafanikio yako kwa kuangalia kiasi cha fedha ulicho nacho, wala usipime kwa kujilinganisha na watu wengine

Jaribu kuangalia una furaha? Je una afya njema na husumbuliwi na maradhi, unapata mahitaji yako yote muhimu, mahusiano yako na Mungu na watu wengine yameimarika?

Ukiyapima mafanikio yako kwa nyanja ya fedha pekee utajikosea kwa sababu upende usipende kwenye maisha ni lazima kuna watu watakuwa na mafanikio zaidi yako na kuna watu watakuwa wapo nyuma yako kimafanikio

Myles Munroe akasema "Tunapaswa kupima mafanikio kwa kuangalia kusudi la mtu hapa duniani" 

Wakati unalalama kwamba kiasi fulani cha fedha hakikutoshi kuna mwingine anatamani angekipata

Wakati unalalama mwanao ni mkorofi na anakuwa wa mwisho darasani kuna mwingine anatamani angepata mtoto n.k

Jambo nalotaka kusema hapa ni kwamba tunapaswa kuwa na shukrani kwa vitu ambavyo Mungu ametupatia bure kabisa. Unapokuwa na shukrani katika kile kidogo ulichokuwa nacho unaongezewa zaidi

Kama Mungu leo angesema kila mtu alipie kila kiungo alichompa bure ni hakika kwamba watu wengi wasingeweza, hivyo jifunze kuwa na shukrani kwa kile ulichokuwa nacho

Umefanya biashara umepata faida mshukuru Mungu, umeamka una pumzi na afya tele mshukuru Mungu, kuna mtu yupo mahali anatamani tuu angekuwa anaona,anatembea, anaongea kama wewe lakini hawezi

Siku zote kumbuka kilicho kidogo kwako wewe ni kikubwa sana kwa mwenzio hivyo kuwa mwaminifu kukifanyia kazi, kukitunza na kukikuza ili kesho uwe na cha kusema.

Shukrani kwa Mungu na binadamu wenzetu ni chanzo cha kufanikiwa zaidi, ni chanzo cha kupewa baraka na waliokuzidi umri na ni chanzo cha kupendwa.

Mwanamke Thamani!

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana