CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA PILI - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, September 10, 2018

CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA PILI


Ninakusalimu kwa Jina la Yesu Kristo, Jina lipitalo majina yote mbinguni hata duniani, nimejawa na nguvu na amani tele siku hii ya leo nina imani mambo ni mazuri sana kwako pia, kumbuka tupo hivi tulivyo kwa neema ya Mungu pekee na asubuhi ya leo kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuna neno kwa ajili yako

Niliomba udhuru jana nikasema sikuwa nimejiandaa kwa ajili ya kichwa hiki cha neno lakini nilichelea kuandaa somo ikanibidi nitafute somo la nyuma nilijaze nyama na kuliweka hapa ila leo tena nimepata kibali cha kuliendeleza sehemu ya pili, karibu tuendelee kujifunza kwa pamoja kama hukusoma sehemu ya kwanza ⇒⇒⇒Bofya hapa kulisoma neno lote

Tulipoishia...
Hii ndiyo maana Biblia ikasema katika Waefeso 4:29 "Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia"
Una kila sababu ya kutamkia watu habari njema na za kufurahisha, una kila sababu za kuwabariki watu kwa kile ambacho Mungu amekupa, kiuhalisia hakuna mtu mbaya hata mmoja duniani kila mtu ana uzuri wake kabla ya kuangalia ubaya tafuta uzuri na utamke

Tunaendelea....
Ulimi ndio unasababisha mambo mengi sana kutukia hata Adamu wa kwanza aliponzwa na ulimi wake, dhambi amefanya kwa kumsikiliza mkewe lakini hataki kutubu bali anamtupia mpira mkewe Mwanzo 3:12 "Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa  awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala

Kusudi la Mungu tokea awali wakati ameumba ulimwengu ilikuwa ni kumpatia kila mtu mke wake, suala la kutafuta mke halikuwepo Adamu ndiyo aliharibu kila kitu, ukisoma maneno hayo vizuri utaona kwamba Adamu alikuwa anamwambia Mungu amekosea kumpatia mke, na ndipo Mungu alibadilika akasema kila mtu na atafute mke wake mwenyewe Mithali 18:22 "Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana

Ni lazima uwe makini na maneno unayotamka hata katika sala zako la sivyo Mungu atajiondoa katika kukufanyia vitu ambavyo alikuwa anakufanyia, hautamki tuu kwa sababu una ulimi bali unafikiri kwa kina kabla ya kutamka, Adamu angefikiri asingalisema maneno hayo angaliomba msamaha au angesema kitu kingine Mithali 15:28 "Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu: Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya

Katika hali ya kawaida watu hufikiri unapomuona mke wa mtu anafanya kitu fulani cha ajabu ukienda kuripoti kwa mumewe unamsaidia hapana, huko ni kumwaga maneno mabaya unachopaswa kufanya ni kumfuata hapo alipo na kumweleza namna mmewe anavyompenda na aache hicho anachokifanya, ukifanya hivi unahesabika kuwa na hekima

Hakuna haja ya kufunga safari na kuenda kumwambia mumewe, tambua ya kwamba mtu yeyote anayekuletea taarifa mbaya isiyokujenga kwa mujibu wa neno hilo siyo mtu mwema, kwani utakapomwambia mmewe kitakachotokea si ugomvi? Je utakuwa umetatua tatizo au umelikuza? Maneno ya watu mara nyingi sana yameharibu ndoa na urafiki baina ya ndugu

Ni vyema kuanzia leo ukajifunza kuchagua maneno ya kusema na ya kutokusema, lakini pia ni vyema zaidi kuchagua maneno ya kusikiliza na ya kutokusikiliza, mimi ukiniletea taarifa yoyote mbaya inayohusu mtu kunisema kabla hujamaliza kuongea utajikuta mwenyewe kwa sababu sina muda wa kusikiliza ujinga

Hivyo hatuongei tuu hovyo kwa sababu tuna ulimi hapana! Tunaongea kwa wakati sahihi na ni lazima tuhakikishe tunaongea vitu sahihi ili kuweza kuyafanya maisha yawe na ladha na yakuvutia Mithali 15:23 "Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini! Tujifunze leo kuanza kunena maneno ya heri kwa wengine acha kuwa kibaraka wa kusambaza habari mbaya za watu wengine

Binadamu hujichimbia shimo kwa maneno yake yeye mwenyewe, kiuhalisia hakuna mchawi mkubwa wa maisha yako kama wewe mwenyewe, leo umefika hapo ulipo kwa maneno yako, yaani unaishi kile ulichokuwa unakikiri siku za nyuma na maisha yanayoendelea baada ya haya ni kile unachokikiri sasa

Haiwezekani kabisa kama ulikuwa unakiri huwezi kubarikiwa itokee Mungu amekubariki kamwe haiwezekani, kama ulikuwa unakiri kwamba hauwezi kuanzisha biashara yako tambua ya kwamba hautakaa uweze kuanzisha, kama ulikuwa unakiri ndoa ni mbaya na zina changamoto elewa mapema hicho ndicho utakachokikuta kwenye ndoa yako

Umeshajichoma moto wa kutosha, umeshajimaliza peke yako ni wakati sasa wa kutafuta zima moto lije likusaidie kuzima moto uliouanzisha mwenyewe kwenye nyumba yako pasipo kufahamu, ni wakati wa kukaa na kuyatafakari maisha yako vyema ili usiendelee kuwa jinsi ulivyo bali ubadilike kwa wema tizama Mithali 16:28 "Mtu asiyefaa kitu huchimba shimo la madhara; Katika midomo yake mna moto uteketezao

Labda haujafahamu nguvu uliyonayo katika kinywa chako, lakini mimi ninaomba nikukumbushe leo kwamba wewe siyo wa kawaida kama unavyodhani au unavyojiona ni kwa sababu tuu ulikuwa hufahamu ila umefahamu sasa, huwezi tena kukiri kushindwa wala kukiri udhaifu linapokuja suala linalokutatiza usiwe mwepesi kusema siwezi kwa nini usiseme Wafilipi 4:13 "Ninayaweza mambo yote katika Yesu Kristo anitiaye nguvu"

Umetumainia nguvu zako vya kutosha hazijakusaidia, huu ni wakati wa kumruhusu Mungu achukue nafasi katika maisha yako na kuanza kutenda kazi yake njema aliyoiweka tangia awali kwako lakini hukuwahi kumruhusu kufanya hivyo, ngoja nikuambie Mungu akiongea na wewe dakika mbili amebadilisha maisha yako kwa miaka ishirini

Watu wote wenye akili sahihi hawaangaiki kufanya mambo yao wenyewe, wanajua kuna aliyewaumba anawajua kuliko wanavyojijua, wanajua hawawezi kufika wenyewe, wanautafuta uso wake kwa nguvu zote na wanataka kusikia kile Mungu alichokiandaa kwa ajili ya maisha yao, jifunze kumsikiliza Mungu utaepuka mambo mengi

Kumbuka ya kwamba hauwezi kamwe kupata haki maishani mwako kama usipokiri kwa kinywa chako na moyo wako uamini kile unachokisema Warumi 10:10 "Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu

Wokovu ni stahiki zako ni haki zako unazopaswa kuzipata, wengi hufikiri wokovu ni kwa watu wa kiroho pekee hapana wokovu ni kwa kila mtu ni yale mambo ya msingi ambayo unapaswa kuyapata katika maisha yako ambayo ulikuwa umeyaoteza baada ya Adamu wa kwanza kutenda dhambi

Itaendelea tena.......

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote

Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana