CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA SABA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Sunday, September 16, 2018

CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA SABA


Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote ulimwenguni na hata mbinguni Jina la Yesu Kristo Bwana wetu, ninatumaini umeamka salama na unaendelea vyema, hili ni juma jipya kabisa na kama Mungu alivyo na mizungu mingi hata juma hili ameandaa baraka mpya tena kwa ajili yako, mwamini lishike neno lake ili uone haya yakitimia katika maisha yako

Karibu tena katika kujifunza neno la Mungu pamoja nasi, tunaendelea na somo la ulimi kwa muda mpaka tutakapoanza somo jingine Mungu atakapopenda tufanye hivyo, Namuomba Mungu ukutane na kile ambacho amekuandalia siku ya leo katka Jina la Yesu Kristo. Kama hukusoma sehemu ya sita ya somo hili ⇒⇒⇒bofya hapa kusoma yote

Tulipoishia.....
Tambua ya kwamba unao ulimi lakini siyo wakwako kila kitu umeazimwa na Mungu ndiyo maana Mungu ni Bwana wako, usifikie hatua ya kuona unaweza kutumia viungo ulivyopewa unavyojisikia, wala kutamka maneno kwa kuzitumainia nguvu zako mwenyewe kumbuka hata unabii unaojifanyia ni kwa kuutafuta kwenye neno la Mungu
Zaburi 12:4 "Waliosema kwa ndimi zetu tutashinda; Na midomo ni yetu wenyewe, ni nani aliye bwana juu yetu? 


Tunaendelea...
Japokuwa mwili wetu ni mkubwa sana lakini unaendeshwa na kiungo kidogo mno ambacho kinaitwa ulimi, mara zote vitu vidogo ndiyo huwa vinafanya mambo makubwa na yenye madhara hata ukipanda merikebu japokuwa ni kubwa sana na inakumbana na gharia nyingi za bahari lakini usukani wake ni mdogo sana na huu ndiyo unaopeleka merikebu uelekeo ambao nahodha anataka

Ukisoma habari ya Daudi na Goliath utashangazwa sana na kitu kimoja, japokuwa watu walikuwa wanaona Goliathi anapigana na mtoto mdogo lakini Daudi hakuwa anajiona hivyo na wote wawili walijua kutumia ndimi zao kuweza kutawala pambano lile, Goliathi alitumia ulimi wake kumlaani Daudi kwa miungu yake 1Sam17:43 "Mfilisti akamwambia Daudi, Je mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake

Daudi naye hakuacha kutumia ulimi wake naye akamlaani kwa Mungu wake 1Sam 17:45 "Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, wewe unanijia mimi na upanga, na fumo na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa Jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana

Wote tunajua kilichotokea baada ya hapa Daudi alishinda vita, kwa namna nyingine ni kwamba Daudi alijua namna ya kutumia ulimi wako kuhamisha vita, hapa ina maana Mungu kama asingejidhihirisha kwa Daudi basi Mungu wa Israeli angeonekana hana nguvu kuliko wa Mfilisti

Huu siyo muda wa kutumia ulimi wako kuelezea shida zako, kwa nini usiutumie kusifia mambo makuu ambayo Mungu wako anaweza kufanya kama Daudi, vitu kama magonjwa vinalaaniwa na vinaondoka vyenyewe ni namna tuu ya kutumia ulimi wako, badala ya kupigia simu kila mtu na kumwambia unaumwa anza kuukemea ugonjwa, badala ya kupiga picha ukiwa umelazwa hospitali anza kumwambia Mungu mimi siwezi kamwe kulazwa hospitali hata siku moja 

Hivi ndivyo tunavyotumia ndimi zetu kutengeneza maisha tunayoyataka, hata sisi walimu tunaaswa sana namna tunavyotumia ndimi zetu maana kuna kujikwaa mara nyingi ndio maana sipendi kuandaa somo hapa lililo na mistari ya neno la Mungu michache ni lazima nitetea kile ninachokisema kwa neno la Mungu linachosema 

Neno la Mungu limeweka wazi hili Yakobo 3:1 "Ndugu zangu msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi, Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi....... hivyo kujikwaa ni suala la ulimi, Mfalme Daudi akasema mwenye haki ataanguka mara saba na atasimama tena, huku kuanguka ni kwa maneno yake mwenyewe

Kama vile tunavyoona njiti ya kiberiti(moto mdogo) inaweza kuteketeza msitu mzima, inaweza kuteketeza soko, inaweza kuteketeza nyumba vivyo hivyo ulimi unaweza kuteketeza mwili wote lakini Mungu anatuambia nao ulimi utateketeza Jehanamu Yak 3:6 "Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, na ndio huo uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfululizo wa maumbile, nao huwashwa moto Jehanamu

Ulimi ni kiungo cha ajabu sana kiasi ambacho hauwezi kufugika, kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi binadamu anaweza kukifuga lakini ulimi haufugiki, ulimi ni uovu uliotulia, ulimi  umejaa sumu iletayo mauti kwa mtu, dakika chache zilizopita tunautumia kumsifu Mungu na matendo yake, baada ya muda kupita tunautumia kulaani watu, kujilaani wenyewe na pengine kulaani uzao wetu wenyewe 

Lakini jambo kubwa la kujiuliza mimi na wewe jee katika ulimi ule ule tunaotumia kumsifu Mungu, tukautumia tena kujilaani wenyewe huoni kwamba kunakuwa na ukakasi wa utendaji hapo? Yawezekanaje katika jito lenye maji matamu pakatoka na maji machungu? Kumbuka kila mzabibu huzaa mzabibu na siyo vinginevyo

Kama umekuwa una ulimi wenye tabia ya ndumilakuwili ni wakati sasa wa kujiangalia upya, ni vitu gani unapaswa kujibadilisha na kujiwekea nidhamu, wokovu ni majukumu na uamuzi ndiyo maana haukushikiwa bunduki kuokoka ni wewe uliamua mwenyewe kukiri, na kila uamuzi una gharama zake za kufuata ni wakati sasa wa kulipa gharama ya ulimi

Itaendelea tena......!


Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote

Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana