CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA TISA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, September 20, 2018

CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA TISA


Ninakusalimu katika Jina la Yesu Kristo, Ninatumaini unaendelea vizuri na shughuli zako, leo tena ni siku njema inayopendeza ambayo Mungu ameifanya kwa utukufu wake ninakukaribisha tujifunze neno la Mungu kwa pamoja

Leo tutaendelea na kichwa chetu cha somo tulichokuwa nacho awali kumbuka jana tulijifunza somo la nyuma linaloitwa "Sitabaki kama nilivyo" kama hukujifunza nasi unaweza ⇒⇒⇒kubofya hapa kujifunza nasi, lilikuwa somo zuri sana na lilikuwa na ushuhuda ndani yake

Tulipoishia...

Juzi katika mada ya Chunga sana ulimi wako sehemu ya nane tuliishia hapa.....
Uwongo utakufukuza nyumbani kwa Mungu, kwa sababu Mungu siyo muongo hawezi kamwe kukaa na muongo hata kwa dakika moja ni lazima atamfukuza, kwa maana nyingine hutasitawi wala kupata kibali kwa Mungu, tambua maisha yetu tunatafuta kibali kwa Mungu, unapokuwa na kibali hakuna kitu ambacho hakifanikiwi, kumbuka ukifukuzwa nyumbani kwa BWANA utakwenda jehanamu ya moto Zaburi 101:7 "Hatakaa ndani ya nyumba yangu Mtu atendaye hila. Asemaye uwongo hatathibitika Mbele ya macho yangu kama hukujifunza somo pili ⇒⇒⇒⇒bofya hapa kujifunza lote

Tunaendelea...
Chunga sana ulimi wako haimaanishi hauongei, naomba nianze hivi ili tuelewane tunakoelekea, inamaanisha unaongea ila kwa ufahamu na hekima siyo kuropoka wala kutamka mambo ambayo haupaswi kutamka kwa ulimi uliopewa na Mungu

Leo katika chunga sana ulimi wako tunaangalia matumizi sahihi ya ulimi kwenye kutubu dhambi zetu kwa Mungu, wote tunajua kwamba kuna tofauti kati ya kutubu na kuomba msamaha, yaani kutubu ni zao la kufanya maamuzi baada ya kufanya tathimini yakinifu juu ya kosa ulilotenda lakini kuomba msamaha ni kusema samahani kwa kuwa nimekukosea inaweza kuwa kwa kulazimishwa au kutolazimishwa

Leo pia nishee nikushirikishe ushuhuda huu ambao ni wangu Mimi binafsi, kuna kipindi fulani cha nyuma niliambiwa taarifa fulani kuhusu watu (niwape jina hili Watumishi) ambao nilikuwa nafanya nao biashara isitoshe hawa ndio wakubwa wangu katika biashara na pia ndio walionialika katika kanisa ninalosali sasa na lililonigeuza kiasi hiki

Neno la Mungu linasema tuishi na Wanawake kwa akili maana ni chombo dhaifu hili mimi lilinitokea kuna dada wawili walinipa taarifa fulani zisizopendeza juu ya watumishi hao ambao nilikuwa nafanya nao biashara nikawauliza mara mbili mna uhakika na mnachoniambia wakasema ndio, kuna siku nikampigia simu mmoja kati ya hao dada maana ni mtu wangu wa karibu sana

Basi alinielezea mambo mengi sana, Mimi kama kawaida nikauliza una uhakika akanihakikishia na maneno mengi sana, huyu dada naye ni mpendwa hivyo nikaamini, tofauti kati ya mwanaume na mwanamke ni kwamba mwanaume hapendi maneno mengi wala hana njia za mkato mimi hiyo siku nikawauliza hao Watumishi maana zilikuwa taarifa mbaya nikaanza kuwawashia moto

Niliandika meseji nyingi kama niandika kitabu na hivi kuna Whatsup kwa kweli nilitiririka sana, kukawa kuna kutokuelewana baina yangu na wao na kukazuka ugomvi kabisa maana hao Wapendwa ni mke na mume jaribu kufikiri nilianzisha vita na taasisi (ndoa)

Baada ya muda kupita na nikakusanya taarifa kutoka kwao nikamrudia yule dada wa awali ambaye niliongea naye nikamwambia mbona huku naambiwa hivi na wewe uliniambia hivi, kufupisha stori niligundua mwenyewe hawa madada walinidanganya

Basi nafsi ikaanza kunisuta, nimelikoroga inabidi nilinywe mwenyewe katika hali ile sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuandika na ushuhuda unaanzia hapa, nikaanza kuandika mada ya "Nguvu ya Msamaha" hii nilifikiri naandikia watoto wa Mungu ila sikujua nini kitatokea mbeleni

Mada ile niliiandika kwa siku sita mfululizo na nilikuwa naandika kitu kinachotoka ndani ya moyo wangu kabisa maana ndicho kiichokuwa kinanitesa, nilipofika siku ya sita tamati kuna mtu mmoja akapiga simu anataka kutuona akaleta fungu la kumi $200 kwamba mada ile imemponya ugonjwa wa mifupa ambao ulimsumbua kwa muda wa zaidi ya miaka 20 ambayo alizunguka katika makanisa mbalimbali pasipo kupona

Hii ni baada ya kujifunza na kugundua tatizo lake ni kutokusamehe aliamua kutoka ndani ya moyo wake kusamehe na akapona hapo hapo, na mimi nilipopata taarifa hii nikapona hapo hapo, ule uzito niliokuwa nausikia ndani ya moyo wangu ukaondoka

Jioni nilijikuta ninatubu kwa ajili ya wale Wapendwa na kwa ajili yangu mwenyewe niliamka usiku wa manane na niliwaombea sana na nakumbuka kabisa niliwaombea mambo mawili tuu la kwanza ni uchumi na la pili ni mtoto wa kiume ninataka nikushudie leo mwezi uliopita walipata mtoto wa kiume

Tambua kwamba wakati mwingine jambo linalokusumbua haupo peke yako wako na wengine, mwalimu mwema siye anayeanza kutatua matatizo yake bali anayeona ya wenzake na kuanza nayo kwenye kusaidia wengine tunajisaidia sisi pasipo kufahamu

Kama na wewe kusamehe au kujisamehe imekuwa ni changamoto kwako, neno hili litakusaidia sana isitoshe zipo shuhuda zingine za neno hili ila hiyo ilinigusa zaidi, kama unataka kujifunza juu ya "Nguvu ya Msamaha" ⇒⇒⇒Gusa hapa kujifunza nasi mada zote sita, itakupeleka ya sita kisha boyfa linki utakazoziona zitakupeleka mpaka ya kwanza

Mwisho wa kushuhudia..

Hilo ni somo pana lakini tambua tuu kwa kifupi kwamba kutubu ni kugeuka kabisa kutoka kwenye dhambi na kufuata uelekeo mpya ila kuomba msamaha siyo lazima mtu abadili uelekeo anaweza kubakia pale pale, pia kutubu ni kukubali kuyavaa majukumu ya dhambi uliyofanya na kunatokea ndani ya kilindi cha moyo wa mtu tofauti na kuomba msamaha

Hivyo kuomba toba ni suala nyeti zaidi ya kusamehe, isitoshe toba ni kwa ajili ya utakaso wa dhambi lakini kusamehewa ni kwa ajili ya kufanya makosa, Yesu alipoanza Injili sentensi yake ya kwanza ilikuwa hii Mathayo 4:17 "Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia" imerudiwa tena Marko 1:15 "Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili

Tunatubu kwa kutumia ulimi ndiyo maana leo nimesema tunaangalia matumizi sahihi ya ndimi zetu, Yesu hakusema watu waombe msamaha kwa sababu ufalme umekaribia hapana ila watubu, watubu kwa sababu walikuwa na dhambi ya asili ambayo ilikuwa inawazuia kuingia katika ufalme wa Mungu, lakini kutubu huku hakuwezi kuwa hivi hivi pasipo sababu ni lazima wafundishwe ndiyo maana alifundisha Injili ili waelewe kwanza kisha watubu

Wakati mwingine watu huweza kuomba msamaha hata kwa vitu ambavyo hawavifahamu lakini toba inakuja kwa ufahamu, kutambua ulipaswa kukaa upande gani na ni nini kilikuondoa na kukunyima baraka zako ambazo Mungu amekupangia 

Mbele za Mungu kile unachofikiri na kile unachosema vyote vinajibiwa, hivyo usikae useme naweza kufikiri kitu kingine na kusema kingine Mungu akanijibu nilichosema akaachana na nilichofikiri hapana, hakikisha unachokisema ndicho ulichokifikiri ili upate majibu sahihi kutoka kwa Mungu 

Waefeso 3:20 "Basi atukuzwe awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu, neno tuyawazayo linamaanisha tunayoyafikiri kuwa makini sana na unachofikiri maana kitajibiwa pia, ndiyo maana kwenye kutubu huwa tunasema ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizozifanya kwa kutenda, kuwaza na kunena

Hii ndiyo maana pia Mungu anatuambia katika Mdo 8:22" Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili ikiwezekana, usamehewe fikira hii ya moyo wako


Tunatubu ili tuweze kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, Mdo 2:38 " Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu

Miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, 1Kor 6:19 "Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;

Biblia inaposema sisi siyo mali yetu wenyewe inamaanisha ya kwamba hakuna kitu tulichonacho na sisi wenyewe hatujimiliki sisi ni mali ya Mungu ni bidhaa ambayo Mungu aliitengeneza kwa ajili yake, kama Jina lake lilivyo Mtakatifu hachangamani na uchafu sababu yeye ni msafi, hivyo wakati wowote tunapokwenda kinyume na neno la Mungu tunamfukuza Roho Mtakatifu ndani yetu

Lakini tunapotubu tunapata tena nafasi ya kuweza kupokea upya kipawa chake na kuweza kuongozwa nae sababu yeye ni wakili mwema, anaweza kutufundisha, na anatupa mafunuo ya mambo yahusuyo maisha yetu na mambo yajayo anatuonesha sasa

Roho Mtakatifu anaishi ndani yetu, Yesu Kristo tulikuwa naye katika hali ya mwili na siyo ndani yetu ilimbidi Yesu atengeneze msingi wa neno kwanza ndipo akaenda kumuomba Baba atupatie Roho Mtakatifu ili agongelee muhuri maneno yake ndani yetu

Kabla ya kuja kwa Yesu Kristo watu walikuwa wanatenda dhambi sana na kwa taarifa yako hakuna dhambi mpya chini ya hili jua Mh 1:9 "Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua, hiivyo vipo vizazi na dunia ambazo zilifanya dhambi na uasi mpaka Mungu mwenyewe akaamua kuziangamiza kwa moto na kwa maji

Unapopata neema ya kutubu dhambi zako usiichezee kwa sababu haufahamu ni nini kitatokea baada ya muda mchache ujao, Mungu akubariki na akusaidie upate kuelewa hili

Hivyo katika kipindi hicho Mungu alikuwa akiangalia duniani na pale anapoona mtu ameupendeza moyo wake kwa matendo yake anaamua kumtumia huyo huyo kwa ajili ya utukufu wake, hii ndio maana ukisoma agano la kale utaona habari zinazosema Roho wa Bwana akamjia/akawa juu ya siyo ndani kuna tofauti kubwa ya kuwa ndani ya na juu yaa ndani yaa ni karibu ni umilele lakini juu ya ni kwa wakati fulani

Zama hizi za zamani zilikuwa ni zama za ujinga na Mungu mwenyewe alikuwa akifunga macho anajifanya kama vile haoni kumbe anaona uchafu na udhalimu wa wanadamu Mdo 17:30 "Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu" na mimi pia "Ninakuambia tubu"

Katika zama hizi hakuna namna ni lazima utubu kwa sababu Mungu ameachilia neema ya toba kwa kila mtu ambaye yuko huku duniani kinyume na hapo utakutana na hukumu, ni muhimu sana kutubu dhambi na usijione una dhambi kuliko wengine kwa sababu neema ambayo Mungu ameachilia ni kubwa kuliko dhambi unazozifanya ndio maana hata ufanye dhambi gani kasoro tuu ya kumkufuru Roho Mtakatifu bado Mungu atakusamehe

Mungu amelithibitisha hili katika Warumi 5:20 "Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi; hivyo neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu ndio maana unapaswa kuwa na ujasiri wa kutubu na kuomba rehema pale unapomkosea Mungu

Huyo anakufanya uone kwamba una dhambi sana kuliko watu wengine ni Shetani na anafanya hivyo ili usitubu aendelee kukutawala na kukutesa, Mungu akisema utubu utasamehewa anamaanisha na ndivyo itakavyokuwa 

Neno hili linakupa uhakika wa kusamehewa dhambi zako zote na kwa asilimia mia, ni maombi yangu kwamba kabla ile siku haijafika uwe umetubu dhambi zako na Mungu akukumbuke kwenye ufalme wake katika Jina la Yesu Kristo aliye hai
Itaendelea tena .....
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote

Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana