MUNGU ANAKUPELEKA SEHEMU NZURI ZAIDI - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Friday, September 21, 2018

MUNGU ANAKUPELEKA SEHEMU NZURI ZAIDI


Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, hili ni Jina lililopewa mamlaka duniani na hata mbinguni naam Jina la Yesu Kristo, ninatumaini umeamka salama na unaendelea vyema na kazi zako, hii ni siku njema sana na Mungu ameifanya ili tuweze kumsifu na kumtukuza katika maisha yetu
Leo tena tunaendelea na kujifunza Neno la Mungu kwa pamoja, nilichelewa kuandaa somo hivyo nimelazimika kutafuta moja ya masomo yetu ya kipindi cha nyuma na nikaliweka vizuri zaidi kwa ajili ya wakati huu, tunakua kutoka kiwango hata kiwango katika utumishi

Tulipoishia jana....
Neno hili linakupa uhakika wa kusamehewa dhambi zako zote na kwa asilimia mia, ni maombi yangu kwamba kabla ile siku haijafika uwe umetubu dhambi zako na Mungu akukumbuke kwenye ufalme wake katika Jina la Yesu Kristo aliye hai
Ninaamini somo la jana lilikuwa somo zuri sana kama hukupata nafasi ya kulisoma tafadhali hakikisha unalisoma hapa kwa ⇒⇒⇒kubofya hapa katika maandishi

Tunaendelea...
Kuna wakati huwa ninakaa na kufikiria nilikotoka ninabaki namshukuru Mungu kwa sababu amenitoa mbali sana, zipo nyakati mbaya nilipitia kwenye maisha yangu ambazo ninajua kama siyo mkono wa Bwana nisingevuka salama, baada ya kupitia nyakati zile sasa nikikaa ndio naweza kutambua nguvu na ukuu wa Mungu, ninaweza kuunganisha nukta moja hata nyingine

Mtu mmoja aliwahi kusema huwezi kuunganisha nukta kwa kwenda mbele sasa ninaelewa maana yake, nyakati mbaya zinamtengeneza sana mtu kwa ajili ya kazi ambayo Mungu amemuandalia mbeleni, Yusufu alipouzwa kama mtumwa Misri na ndugu zake na hata baadae kufungwa jela zile zilikuwa nyakati ngumu sana kwake lakini ndizo zilizomuandaa kuwa waziri mkuu

Sio kwa uwezo wangu bali ni kwa uweza wake yeye ambaye hunitia nguvu kila wakati, kuna kipindi mtu unapitia changamoto nyingi na pengine unaona huenda hata watu wamekutenga au Mungu kakusahau, lakini baada ya kufanikiwa kutoka katika changamoto ndio unaelewa Yakobo 1:2 "Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkianguka katika majaribu mbalimbali, mkifahamu ya kuwa majaribu kwa imani yenu huleta saburi

Hauwezi kuinuliwa bila majaribu, huwezi kufanikiwa katika huduma bila majaribu, Mungu ameruhusu mlango wa majaribu kuwa njia ya kutuinua ili tuende katika viwango vingine, anayeweza kuvumilia majaribu ndiye anayeinuliwa Ayubu 1:22 "Katika mambo yote hayo Ayubu hakufanya dhambi, wala kumwazia Mungu kwa upumbavu"

Hata uwe kwenye changamoto kubwa kiasi gani Mimi ninakuhakikishia kupitia Neno la Mungu kuna njia ya kutoka, leo ninakuomba ujiweke kwenye nafasi ya Ayubu ambaye alikuwa tajiri kuliko watu wate wa mashariki, mke, watoto, mali na afya yake vilijaribiwa na Adui mbaya zaidi alipoteza familia yake yote akabaki peke yake lakini hakumwazia Mungu upumbavu

Ukitaka kuamini kwamba unachokiona ni changamoto kwako siyo kitu jilinganishe hali yako na ya Ayubu, kama unataka kuinuliwa usiyakimbie majaribu au changamoto zinapokuja, simama na mshukuru Mungu mwambie asante kwa kuniamini naweza kuitatua hii changamoto kisha ishughulikie kisawasawa akiona akiwa mbinguni atakuinua lazima

Tunafahamu baada ya majaribu Ayubu alirudishiwa kila kitu mara mbili Ayubu 42:10 "Kisha BWANA akamrejeshea Ayubu mali yake, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo mwanzo"

Jaribu halimaanishi unaacha kuwasaidia wengine na kuangalia mambo yako tuu au changamoto yako tuu hapana! unaweza kuwa kwenye jaribu na ukawaombea wengine na kutatua changamoto za wengine na Mungu akakuinua zaidi kama alivyofanya kwa Ayubu

Kwa nini?
Kwa sababu atakaye kuiokoa nafsi yake ataipoteza bali atakaye kuipoteza nafsi yake kwa ajili ya Yesu ataiokoa, unapowatanguliza wengine, unapotanguliza nafsi zingine unakuwa umetanguliza ufalme wa Mungu kwanza, uwe unajua au haujui na kama unafanya hivyo Mungu ni lazima akushughulikie kwa sababu akikuacha ina maana utaangamia

Ninatamani ufahamu leo kwamba Mungu anatenda kazi siku zote na wale wanaomwamini asilimia zote na hawana tegemeo lingine lolote ispokuwa Mungu pekee, maana nzuri ya Imani kwa Mungu ni hii "Kama ni kuangamia na niangamie pamoja na Mungu"


Katika kipindi cha majaribu kama uliwahi kuwa na vitu vizuri kipindi cha nyuma mfano kazi au biashara halafu ikafa ndipo Shetani anapoanza kukukumbusha furaha uliyokuwa nayo kipindi kile na kukuambia ya kwamba Mungu amekuacha, ila wakati wazo la namna hii linakujia unapaswa kufahamu kwamba Mungu siyo wa mambo ya kale tuu bali ni wa sasa na milele

Ninataka kukuambia kwamba yaliyopita achana nayo weka tumaini lako kwa Mungu na mambo yajayo, hii ni kwa sababu hauendi nyuma kwenye maisha bali unaenda mbele na ili kuweza kwenda mbele ni lazima usahau maumivu ya nyuma

Mtu mmoja akasema akikumbuka changamoto aliyopitia kipindi cha nyuma ni kwa lengo la kujifunza tuu na si vinginevyo, inawezekana umeumizwa sana katika ndoa, mahusiano, kazi, biashara haziendi au pengine watu wanakudharau

Mungu leo anakuambia Jeremia 29:11 "Maana nayajua mawazao ninayowawazia ninyi, asema BWANA; ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za baadaye" Mungu anao mpango na maisha ya kila mmoja na mpango wake ni kutupa tumaini jema na kunyoosha kusudi letu

Huenda wewe ni mtumishi mzuri, lakini thamini sehemu uliyopo sasa ndipo Mungu atakuinua na kukupandisha sehemu nyingine, kumbuka aliye mwaminifu katika vitu vidogo Mungu humuongezea na vikubwa kwa sababu mambo makubwa ni matokeo ya mafanikio ya mambo madogo

Usidharau kabisa sehemu uliyopo mshukuru sana Mungu kwa sababu ni sehemu njema na ya kupendeza, kila asubuhi unapoamka mpe shukrani kwa jinsi ulivyo, mwembie kwa tabasamu pana kwamba ninajua hapa nilipo nipo kwa neema yako na hata ninakoenda nitafika kwa neema yako, muoneshe Mungu kwamba unathamini anachokuwazia na upo tayari kukifanya

Mungu kakuumba kwa namna ya ajabu sana unapendeza, unavutia na ni wa pekee ndio maana upo hivyo ulivyo, ambacho watu wanakiona cha ajabu kwako ndio uzuri ambao Mungu kakuwekea, hivyo jiamini na mtumainie Mungu pekee achana kabisa na maneno ya wanadamu Mwanzo 1:27 "Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba

Siku zote kumbuka mtu anayekudharau anamdharau Mungu na siyo wewe kwa sababu wewe ni mfano wa Mungu, sikio la Mungu siyo zito kiasi hicho asisikie wanayokusema, macho ya Mungu hayajajifunga asione wanaokung'ong'a, jambo la msingi ni wewe kusimama katika nafasi yako na kumwamini Mungu asilimia zote

Mungu ni wa pekee na wa ajabu kila amtumainiye na kuliamini neno lake huthibitika kwake, amini naye atafanya, chunguza utagundua Mungu hupenda kuwainua wanyonge na kuwaketisha na wafalme kwa ajili ya utukufu wake

Ni furaha zaidi masikini akibarikiwa kuliko tajiri akizidi kujiongezea mali na ndio maana Mungu hupenda kuwainua wanyonge, na tambua ya kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya kubarikiwa na kuwa tajiri, nenda kwa Mungu kutafuta baraka ndiyo utakavyothibitika waachie watu wa dunia watafute utajiri kwa sababu kwenye baraka kuna utajiri

Tutaendelea tena wakati mwingine....

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana