KUTEMBEA KATIKA MUDA ULIOAMRIWA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, September 24, 2018

KUTEMBEA KATIKA MUDA ULIOAMRIWA


Ninakusalimu katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, ninatumaini ni mzima wa afya na unaendelea vyema, nimekuwa na juma jema sana ambalo lina baraka na mafunuo mengi, ninamuomba Baba katika Jina la Yesu Kristo aendelee kubariki kazi ya mikono yako

Jana hatukuweza kuwa na somo katika mtandao huu ni kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu lakini ninamshkuru Mungu kwamba kuna masomo mengi sana katika huu mtandao hata kwa bahati mbaya tusipoweka bado una masomo zaidi ya 90 ya kujifunza na pia ukitembelea kwenye page yetu ya facebook yapo zaidi ya 110 tofauti ya kujifunza

Tulipoishia.....

Ni furaha zaidi masikini akibarikiwa kuliko tajiri akizidi kujiongezea mali na ndio maana Mungu hupenda kuwainua wanyonge, na tambua ya kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya kubarikiwa na kuwa tajiri, nenda kwa Mungu kutafuta baraka ndiyo utakavyothibitika waachie watu wa dunia watafute utajiri kwa sababu kwenye baraka kuna utajiri

Kama hukujifunza nasi somo lililopita la "Mungu anakupeleka sehemu nzuri zaidi" unaweza ⇒⇒⇒kubofya hapa kujifunza nasi

Tunaendelea.....

Leo pia hatutaendelea na mada ya chunga sana ulimi wako bado sijapata kibali cha kuendeleza mada ile leo kipekee tuna somo zuri sana na watu wengi wanapaswa kulielewa somo hili la "Kutembea katika Muda Ulioamriwa"

Kila neno la Mungu unalolisoma lipo kwa ajili ya leo na siyo kesho, hausomi neno na kupata ufunuo ukasema huu ni wa kesho bali ni wa siku hiyo na wakati huo, ila linapokuja suala la kufanya maamuzi makubwa yanayohusiana na maisha yako unapaswa kusubiri mpaka usikie sauti, Yesu alimwambia Mama yake sentensi hii Yohana 2:4 "Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.

Leo tambua kwamba upo muda maalumu ambao Mungu ameuandaa kwa kila mtu kwa ajili ya kufanya kusudi lake, Yesu alikuwa mwana wa Mungu lakini kama anasema saa yake haijawadia ina maana kuna saa kwa ajili ya kila mtu na kwa ajili ya kila kitu

Mfalme Suleimani na hekima zake alifahamu siri hii hata akasema maneno haya Mhu 3:1 "Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu. Hili hata Shetani analifahamu sikiliza alichomwambia Yesu Mathayo 8:29 "Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe Mwana wa Mungu? Je umekuja kututesa kabla ya wakati wetu?

Kama mpaka Shetani anajua kuna wakati wa kila jambo na kila kusudi jee wewe Mkristo kwa nini unafanya vitu kwa kulazimisha, kabla ya kuanza kufanya jambo lolote hakikisha unasikia sauti kwanza, ndipo unapoanza usikurupuke tuu na kurukia mambo yatakushinda kama Yesu ilimbidi asubirie muda wewe ni nani ukurupuke?

Hata kumsulubisha Yesu haikutokea tuu ndiyo maana mara nyingi walitaka kumpiga mawe na alitoweka mbele yao hata alipokuwa hekaluni siyo kwa sababu alikuwa anaogopa kifo hapana ni kwa sababu muda ulikuwa bado Yohana 8:59 "Basi, wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni
Naomba niandike sentensi hii itakushangaza lakini ndio ukweli wenyewe "Unapotoka kufanya kitu nje ya muda Mungu aliokupangia mkono wa Mungu hauwi pamoja nawe" hivyo itakubidi utumie nguvu zako mwenyewe, utumainie akili zako mwenyewe na ukomae hapo mpaka wakati ulioamriwa utakapofika

Hakuna mtu ambaye alikuwa anaweza kumuuwa Yesu, usishangae kauli hii rudia tena kuisoma Yesu aliamua mwenyewe kuutoa uhai wake wangeweza kumsulubisha mpaka wachoke na asife kama angetaka hivyo, ila aliutoa uhai wake mwenyewe Yoh 10:18 "Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nilipokea kwa Baba yangu

Hii ni kwa sababu Yesu alikuwa anafanya huduma yake kwa wakati ambao ulikuwa umekusudia na Mungu, ukijidai unaenda mwenyewe yatakayokupata huko ni shauri yako usije kusema hukuwahi kujifunza juu ya hili, kumkamata Yesu ilishindikana ni mpaka muda wake ulioamriwa ulipofika ndipo walimpata Yohana 7:30 "Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika 

Watu wengi wameanza vitu vikaishia njiani siyo kwa sababu Mungu hakuwapangia kufanya vitu hivyo ila kwa sababu walifuata muda wao wenyewe na siyo muda aliowapangia Mungu kufanya mambo hayo

Mungu ametupatia karama mbalimbali kupitia Roho Mtakatifu lakini ukweli ninaokuhakikishia ni kwamba utakapotoka kwenda kufanyia kazi karama yako nje ya muda ambao Mungu ameuandaa kwa ajili yako utakutana na changamoto nyingi sana ambazo pengine zitakurudisha nyuma

Hii ni kwa sababu Shetani anajua namna ya kukuharibu na kukutega pale unapokuwa nje ya muda wa Mungu, kwanza mazingira yanakuwa hayajaandaliwa kwa ajili yako, hivyo utapaswa kuandaa mwenyewe na pia itakubidi utumie nguvu nyingi sana kufanya kitu kidogo au uingie gharama kubwa kufanya kitu ambacho ungekifanya bure kwa wakati ulioamriwa

Waebrania 3:7 "Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake, pale unapopewa ufunuo wa kitu fulani au unapofundishwa suala fulani unapaswa kulifanyia kazi haraka kama umeambiwa ufanye hivyo unaposema hili nitalifanya kesho au juma lijalo unamzimisha Roho wa Mungu
Ni lazima tufikie kwenye kiwango cha juu kabisa cha kuelewa neno siyo kila ufunuo unaopewa ni wa kuutimiza wakati huo, kuna maagizo mengine yatakupelekea kusubiria wakati fulani ili uanze kuyatimiza, lakini wakati haujatoka nje kuyafanyia kazi unakuwa unajiandaa ndani

Tunaposoma neno la Mungu anaetufundisha na kutupa maarifa ni Roho Mtakatifu na kumbuka yupo mahali pote kwa wakati mmoja hivyo anapokupa mafunuo ya kitu fulani kwa wakati huna budi kuutumia ili kupata matokeo wakati huo 

Neno la Mungu ni jipya masikioni petu pale tunapolisikia hata kama ni la miaka mingi iliyopita lakini utendaji kazi wake upo kwa wakati ule unapolisikia, kuna vitu vya kupokea hapo hapo hauna haja ya kusubiria muda kama una imani, isitoshe tunapokea katika ulimwengu wa roho kwanza siyo mwili

Kila kitu tunachokisoma kwenye Biblia kipo kwa ajili ya leo na siyo kesho, uponyaji, kazi, neema, imani, mafanikio, baraka n.k katika Math 6:11 "Utupe leo riziki zetu hivyo hata riziki ni suala la leo siyo miaka ijayo

Mungu anasema katika Zaburi ya 95:7 " ....Sisi ni kondoo wa mikono yake ingekuwa heri leo tusikie sauti yake" Hatusemi tutaokoka kesho wala wiki ijayo tunaokoka leo sasa hivi na ndio maana anasema usiufanye wako kuwa mgumu

Hatusubiri tufikie umri fulani au tuwe na vitu fulani ndio tumtumikie Mungu bali tunamtumikia Mungu leo tena sasa hivi kwa sababu Mungu wetu ni Mungu anayetenda sasa, kama muujiza wako upo leo usitake upokee kesho ndio maana Biblia imeweka wazi kwamba tusisumbukie kesho bali tuiache itajitegemea yenyewe

Mungu ni Mungu wa leo kwa sababu Yeye ni Mungu wa muda kuna mtembeo unapaswa kuwa nao leo na siyo kesho, baraka zako za leo na za kesho hazifanani, ndio maana kuna siku unapata zaidi ya siku nyingine na ukichunguza vema utagundua siku ulizopata ulimtumaini Mungu zaidi hii ndio maana ni muhimu sana kuanza siku yako na Mungu

Hii ni siku ambayo Mungu ameifanya nitaifurahia na kuishangilia ukimuamini Mungu wa sasa kila siku unakuwa mtu wa kufurahia kwa sababu kila siku ni Mungu mwenyewe anaifanya

Hatusubiri kuwa mabilionea ndio tufurahie maisha ila tunaanza kuyafurahia maisha kwa ubilionea ambao tunauona katika Mungu wetu na tunaanza kuyafurahia maisha hata kama tunalala kwenye mikeka, Ukristo una maana tu pale unapokuwa na imani ndani ya Kristo Yesu, kama hauamini na hausadiki maneno yake basi itakuwa ni vigumu kuelewa na kukiona kile ambacho Mungu amekiandaa katika maisha yako

Mimi ninaamini sipo hapa duniani kwa sababu nilitaka kuwepo! Hapana ni kwa sababu alitaka niwepo na kama ni hivyo ninavyoamini basi ana kusudi aliloliweka ndani yangu, kiuhalisia hatuuoni utukufu wa Mungu kipindi tuu pale ambapo tumepigika, tumefungwa, tunaumwa au tumefilisika Hapana bali ni hata kipindi tuna mafanikio makubwa kiroho na kimwili

Ni lazima tuhakikishe tunaona afya yetu leo katika ugonjwa wetu wa leo, ni lazima tuone mafanikio yetu leo katika umasikini wetu wa leo hii ndio inayobadilisha mienendo yetu na matendo yetu, kama huwezi kujiona upo sehemu fulani kesho kama leo basi jua sehemu hiyo kamwe Hutaweza kuifikia kwa sababu mambo ya kesho yanaonekana katika roho leo

Hii ndio maana Mungu hutujuza mambo yote yajayo kabla ya hayo kutukia kwa sababu Mungu ni wa sasa na siyo wa kesho anakuonesha habari za kesho leo ili uiishi kesho leo, ukweli ni kwamba kama Mungu angekuwa siyo wa leo hakuna mtu angemwamini ndio maana anakuonesha kesho yako leo ili ujue ulipo na kule unakokupeleka na unaanza kuishi kile alichokuonesha leo katika roho

Itaendelea tena wakati mwingine.....!

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana