KIPINDI CHA KUPANDA MBEGU. - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, September 25, 2018

KIPINDI CHA KUPANDA MBEGU.


Ninakusalimu kwa Jina lipitalo majina yote hili ndilo Jina la Yesu Kristo lina mamlaka mbinguni na hata duniani, katika ulimwengu huu na hata ule ujao, ninatumaini kwamba wewe ni mzima wa afya na unaendelea vyema kabisa

Katika maisha tunayoishi hapa duniani huwa tunapitia vipindi tofauti kwa ajili ya kujifunza, kukua na kutuimarisha, vipindi hivi ni muhimu sana kwa sababu humuandaa mtu kuweza kufikia hatma ambayo Mungu ameiandaa kwa ajili yake

Usitamani kuruka kipindi kama unataka kuenda vyema, hakikisha unapita katika kila kipindi hii itakufanya kujiamini, itakufanya kumpenda Mungu zaidi kwa sababu vipo kwa ajili ya kuimarisha upendo wako na Mungu, ni dhahiri kwamba watu wasingempenda Mungu kama angekuwa hawasaidii katika nyakati ngumu

Isitoshe nyakati ngumu ndio zinaimarisha mahusiano yetu na Mungu zaidi, wale wanaoshindwa kudumisha mahusiano na Mungu baada ya kuwaokoa kwenye majanga Mungu huwakataa na kuwatupilia mbali, hili siyo fungu lako katika Jina la Yesu

Moja ya kipindi tunachopitia kwenye maisha ni kipindi cha kupanda mbegu, leo tuangalie kwa kifupi sana kipindi hiki kinajumuisha mambo gani, kama hukujifunza nasi somo la jana la Kutembea Katika Muda Ulioamriwa  ⇒⇒⇒bofya hapa kujifunza nasi

Ukisoma habari za Adamu na Hawa baada ya kumkosea Mungu utagundua kwamba swali la kwanza ambalo Mungu alimuuliza Adam ni hili Adam upo wapi? Hii haimaanishi Mungu hakufahamu Adamu alipokuwepo wakati ule ila alitaka akiri kwa kinywa chake sehemu ambayo aliyokuwepo.

Ukipigiwa simu na upo katikati ya mji na ukaulizwa uko wapi kama sehemu hiyo haifahamiki lakini mbele yake kuna sehemu maarufu utaitaja hiyo au jengo maarufu kisha utamwambia ulipo.

2Kor 9:10 “Na yeye ampaye mbengu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu katika kipindi hiki cha kupanda mbegu mtizamo unaoingia nao shambani una mchango mkubwa sana katika mavuna utakayoyapata, kama unapanda tuu mbegu alimradi umepanda na hauna matarajio ya ushindi mkubwa basi matokeo yako yatakuwa hafifu

Umeamua kuanzisha biashara amini asilimia mia moja utafanikiwa katika biashara hiyo kuliko watu wengine wote, umeajiriwa katika taasisi fulani amini utakuwa mfanyakazi bora na hakuna atakayefanya vyema kama wewe

Baba yangu mzazi huwa ana Imani yake kwamba kila akienda kupanda mbegu shambani ni lazima usiku wake au siku inayofuata jioni mvua inyeshe, na amekuwa akiamini hivi kwa miaka mingi na ndivyo inavyokuwa kwake, watu walikuwa wakimpigia simu na kumuuliza lini anapanda mbegu ili nao wapande nae sababu ni kitu ambacho wamekuwa wakiona kinatokea kwake miaka kadhaa Math 9:29 “Ndipo alipowagusa macho akisema, Kwa kadiri ya Imani yenu mpate utapata kadiri ya Imani yako siyo kadiri ya machozi na masononeko

Kitu cha msingi hapa ni kwamba kama hujui ulipo huwezi kufahamu unakoelekea, hivyo kwenye maisha utakutana na watu wengi sana ambao wanavutiwa na sehemu uliyopo lakini swali kubwa na la msingi la kujiuliza ni jee hiyo ndiyo sehemu Mungu anataka uwe?

Katika kipindi hiki cha kupanda mbegu unapaswa kuwa mtu wa kuwekeza kila shilingi ambayo unaipata na pia ndio kipindi cha kujitoa sana, ni lazima upande mbegu zako shambani kisha uhakikishe kwamba zinapata mvua/maji, zinapaliliwa na kuondolewa magugu ndipo utakapoweza kuvuna mazao mazuri

Hatuanzishi biashara tukaiacha kwa wafanyakazi kabla haijashamiri na kuhakikisha ina usimamizi uliotukuka, wengi hufikiri wanapaswa tuu kuanzisha biashara wanasahau biashara siyo kuanzisha, biashara ni kuisimamia na kuiwekea misingi mpaka iweze kuleta faida maradufu

Kadhalika na kwenye Idea/wazo letu ni lazima tuhakikishe tunalipangilia vizuri, tunashirikisha watu sahihi ambao wataondoa magugu kisha tunazipanda kwa kuzitendea kazi, kuwa na mbegu ni kitu kingine na kupanda mbegu mpaka imee na kuzaa ni kitu kingine kwa sababu kuna michakato ambayo itapitia mpaka ifikie inapopaswa kufika.

Maisha ni magumu kama kila kitu tutataka kufanya peke yetu bila kutafuta msaada wa kimaarifa, kutengeneza mahusiano na watu fulani na kuwa tayari kujifunza yale ambayo tunaelekezwa na waliotutangulia

Kuna watu ambao wameshafika unakoelekea, ni hekima kuwasikiliza kuliko kuwadharau na kutaka kufanya njia kuwa refu, uzuri wa kujifunza kwa aliyekutangulia ni kwamba unaachana na changamoto alizopitia unachukua vitu alivyovifanya vikamfanikisha tuu

Ni muhimu tukatambua kwamba sisi tulikuwa ni wazo la Mungu kisha tukaumbwa, lakini kwenye kuumbwa kwetu Mungu aliweka viungo mbalimbali katika miili yetu na vinapofanya kazi kwa pamoja ndipo tunapokuwa wazima.


Hitilafu ya kiungo kimoja mfano figo inaonekana mpaka kwenye ini na mapafu hivyo kila kiungo kina umuhimu wake, usikae ujidanganye na kujiambia kwamba unaweza kufanya kila kitu peke yako Mith 28:26 “Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa kila wazo tulilonalo hatuwezi kulimaliza peke yetu kuna ladha ya mtu fulani itahitajika kiutendaji, kuna ushauri utahitajika, kuna fedha zitahitajika n.k

Itaendelea tena .....!


Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana