MUNGU NI WA LEO- SEHEMU YA KWANZA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, September 26, 2018

MUNGU NI WA LEO- SEHEMU YA KWANZA


Bwana Yesu asifiwe, ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote la Yesu Kristo, leo tena ni siku nzuri inayopendeza Mungu ameifanya kwa utukufu wake ili tumsifu na kusimulia tena matendo yake makuu maishani mwetu

Tulipoishia jana...

Hitilafu ya kiungo kimoja mfano figo inaonekana mpaka kwenye ini na mapafu hivyo kila kiungo kina umuhimu wake, usikae ujidanganye na kujiambia kwamba unaweza kufanya kila kitu peke yako Mith 28:26 “Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa kila wazo tulilonalo hatuwezi kulimaliza peke yetu kuna ladha ya mtu fulani itahitajika kiutendaji, kuna ushauri utahitajika, kuna fedha zitahitajika n.k

Tunaendeleaa....
 Jana tulikuwa na somo zuri sana la "Kipindi cha kupanda mbegu" lilielezea kiundani mambo  ambayo mtu anayafanya kabla ya kufikia baraka ambazo Mungu amemuandalia kama  hukujifunza nasi unaweza ⇒⇒⇒Kubofya hapa kujifunza nasi

 Leo kipekee tujifunze somo jingine la Mungu ni wa leo .....twende nasi sasa..

Mungu anatenda mambo sasa na siyo kesho hii ndio maana anaitwa Bwana wa Mabwana Yeye asiyeshindwa, ukiambiwa na Mungu kwamba mwakani muda kama huu utakuwa na mtoto kama Elisha alivyomwambia yule mwanamke Mshunami haimaanishi Mungu atafanya mwakani hapana, katika ulimwengu wa kiroho jambo hilo limeshafanyika

Waebrania 13:8 " Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Hii inamaanisha namna ambavyo Yesu alifanya jana ndivyo atakavyofanya leo na hata milele, hii ndiyo maana tunamwamini Mungu, kama Mungu angekuwa hawezi kufanya leo zaidi ya jana tusingemuamini ndiyo maana ni Mungu wa leo

Hivyo haumuombi Mungu kitu leo akakuambia atakujibu kesho au baada ya wiki hukujibu hapo hapo kama haujajibiwa huenda haujaomba ipasavyo au kakujibu lakini haujafahamu ila ni hakika hujibu wakati huo 

Kuna nyakati ambazo Mungu huuficha uso wake kwa watu kwa sababu maalumu kwa mfano kipindi cha Ayubu, lakini Mungu alivyofanya vile kulikuwa na sababu maalumu ambayo ilikuwa ni kumdhihirishia Shetani kwamba bado anao watu wanaomtumikia duniani, Ayubu alifikia sehemu ya kukata tamaa ndiyo maana akasema hivi Ayubu 13:24 "Mbona umeuficha uso wako, Na kunihesabu kuwa ni adui yako

Kesho tutajifunza pamoja somo maalumu nitalipa jina la "Mungu Anayejificha" hili litakupa maana halisi ya kwa nini Mungu alimruhusu Ayubu kujaribiwa na Shetani lakini pia litakupanua uelewa kwa nini kuna wakati Mungu hujificha tunapomuita

Ninaposema kujibiwa hata Hapana ni jibu, hivyo unaweza kumuomba Mungu jambo fulani na akakujibu hapana na amini nakuambia Mungu anakujua kuliko unavyojijua hivyo anaposema hapana katika suala fulani inakuwa ni kwa kusudi la kukuokoa na jambo fulani

Kuna kipindi fulani nilimuomba sana Mungu juu ya suala fulani lakini kila nilipokuwa ninaendelea na yale maombi nilikuwa nasikia moyo kuwa mzito, baadaye kabisa nilikuja kuelewa kwa nini Roho Mtakatifu alifanya vile na kitu nilichokuwa nakiomba hamu ya kuwa nacho ikaisha nikakuta moyo wangu unafanya jambo jingine ambalo hata sasa limegeuka furaha ya moyo wangu

Unapoisikia sauti ya Mungu katika siku husika hauna sababu ya kusema nitaifuata kesho hapana unakata shauri hapo hapo na kufanya kile ulichoambiwa, hii ndiyo njia pekee inayoimarisha ushirika wetu na Roho Mtakatifu

Waebrania 4:7 "Aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu

Lakini pia Mungu ni wa leo na siyo kesho ndio maana kila siku anataka tutubu na tuwe wapya Waebrania 3:13 "Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi, toba inatufanya tuwe wapi na wasafi kila siku mbele za Mungu 

Hivyo hatufanyi dhambi leo kisha tukasema tutatubu kesho au mwakani ila leo leo lazima tutubu na kuomba rehema kwa Mungu ndipo anapotusamehe na kuturejesha kuwa wapya kwa sababu Mungu ni mpya kila siku, fadhili zake na uaminifu wake katika maisha yetu hazielezeki kamwe

Mambo aliyoyafanya kwa Watumishi wake ikiwemo Musa, Elia, Elisha na wengineo bado anayafanya hata leo kwa kiwango kikubwa na cha ajabu sana na bado anaudhihirisha ukuu wake katikati yetu kama wana wake

Mungu hataki kuwa wa historia ndio maana ni Mungu wa leo anafanya matendo mapya kila leo hii inatufanya sisi wana wake tuzidi kumuamini na kulishika neno lake zaidi angekuwa wa historia hata mimi nisingemuamini

Kama ningeliweza kujua namna Mungu anavyotenda mambo yake basi hata kiu ya kujifunza kwake ingeisha lakini kwa sababu ana mizungu mingi na anafanya mambo kwa namna ya ajabu zisizoelezeka ndio maana anakuwa mpya kila leo

Ukisikia mtu anakuambia anamjua Mungu huyo ni muongo na hata hajui nukta ya Mungu jamani Mungu hachunguziki wala haelezeki Daudi rafiki wa Mungu alishindwa kabisa kuelewa Mungu alivyo na namna anavyotenda mambo yake

Mungu ni wa ajabu na anatenda mambo ya ajabu njia zake hazichunguziki akili yake haielezeki ndio maana ni wa leo kila siku anatenda mambo mapya na ya ajabu, 

Eliya alisema 1Wafalme 18:15 Eliya akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo ambaye ninasimama mbele zake, hakika nitajionyesha kwake leo. Hajasema atajionesha kesho bali leo sababu alijua fika Mungu ni wa leo siyo kesho

Unapomuendea Mungu muendee kwa akili ya leo, kwamba atakupatia kila unachohitaji kwa muda huo na hii ndiyo imani, unapoomba amini ya kwamba umepokea wakati huo huo ni kama maandiko matakatifu yanavyosema Warumi 1:17 "Mwenye haki ataishi kwa imani"

Kwa nini usiungane nami leo kama umeisikia sauti yake utubu dhambi zako na kumpokea Yeye awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako?


Itaendelea tena kesho........

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana