CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA TANO - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, September 13, 2018

CHUNGA SANA ULIMI WAKO- SEHEMU YA TANO


Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, ninatumaini unaendelea vyema na ni mzima wa afya, ninamshukuru Mungu kwa ajili yako na kwa ajili ya familia yako

Leo tena ni siku njema inayopendeza na Mungu ameiandaa ili tuweze kuyasimulia matendo yake makuu na ya ajabu katika maisha yetu, tunaendelea na somo letu la chunga sana ulimi wako kama ulisoma au haukusoma somo la jana ⇒⇒⇒ bofya hapa kulisoma sababu limebadilika kuna mambo mapya

Tulipoishia….

 Ninatamani kila mtu anapofikia mwisho wa safari yake atamke maneno hayo, hili linawezekana kwa kila anayeamini, Mungu akulinde na kukuongoza kufikia kile ambacho amekusudia maishani mwako, Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ikae nasi sote. Amen

Tunaendelea…

Ipo siri kubwa katika kutumia ulimi wako vizuri, pale unapoaanza kuutumia vema mambo yanabadilika na kuwa mazuri, Mfalme Daudi aliifahamu siri hii  ndiyo maana akamuomba Mungu aweke mlinzi kinywani mwake, ili asiongee mambo yasiyo na msingi Zaburi 141:3 “Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojenzi mlangoni pa midomo yangu

Mara nyingi sana watu wanaongea mambo ya kijinga kwa sababu ya sehemu wanazokwenda na aina ya watu wanaoshirikiana nao, siku ukibadilisha aina ya sehemu unazoenda na watu wasioelekea unapokwenda hata maneno yako yatabadilika, kila sehemu zina maneno yake mfano bar kuna lugha yake, disko kuna matendo yake Zaburi 39:1 “Nilisema, Nitazitunza njia zangu, Nisije nikakosa njia zangu

Mfalme Daudi anasema mtu mbaya alipokuwa anakuja kwake alikuwa hana muda wa kufungua kinywa chake, kwa maana nyingine ni kwamba alitia gundi mdomo wake, hakuna kuongea na watu wajinga usije ukawa mjinga kama wao kwa sababu mtu ni wastani wa tabia za marafiki zake sita anaokaa na kuongea nao sana, anza kuangalia marafiki zako ondoa wale wasio na sababu Zaburi 39:1b “Nilitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya awapo mbele yangu

Wakati ninamaliza kidato cha sita nilisema sitaki kwenda kusoma elimu ya juu na watu niliosoma nao na nilimaanisha, nilisema maisha ni safari ninataka kukutana na watu wengine sio kama hawa japokuwa tulisoma wote shule moja ila hata sasa nina rafiki wawili tuu kati ya watu zaidi ya 60 tuliosoma pamoja

Nilifanya hivi kwa akili na nilijua ninaelekea sehemu fulani sitaki mtu wa kunikatisha tamaa au kuniambia maneno nisiyoyahitaji, Mungu anaanza kuongea na wewe pele unapojifunza maneno ya kuongea na kuwa na muda wa kutosha kutafakari neno lake, namshukuru Mungu leo kwa sehemu aliyonifikisha na vitu anavyovifanya kupitia mikono yangu na utumishi wangu

Kitu cha kwanza cha mtu anayejua kutumia ulimi wake ukikaa naye hana muda wa kuongelea mambo ya watu, utamsikia akiongea juu ya maono aliyokuwa nayo na jinsi anamwamini Mungu atamfikisha, kama unakaa na mtu dakika thelathini kazi yake ni kuongea habari za wengine jua huyo hajui anakoelekea, kifupi amepotea

Ulimi wetu ni kalamu japokuwa wengi hawafahamu unapoongea unaandika katika ulimwengu wa roho tafadhali fahamu hili, tena ulimi unaandika vizuri kuliko hata mikono yako, hakuna Mtumishi yeyote hata awe na nguvu kiasi gani anaweza kutenda muujiza pasipo kuongea, ni mpaka unapotamka ndio mambo yanatokea Zaburi 45:1 “Moyo wangu umeufinika kwa jambo jema, Mimi nasema nilivyomfanyia Mfalme; Ulimi wangu ni kama kalamu ya mwandishi stadi

Tambua ya kwamba watu wajanja ni wale wanaojua kutumia ndimi zao vyema, sehemu sahihi na anasema neno sahihi, ushindi unaanzia kwenye matamshi unayosema, Shetani hashindwi kwa mdomo uliofungwa bali kwa kumtamkia neno la Mungu, yeyote anayekutakia mabaya mtamkie na wewe kabla hayajafanyika kuwa kweli kwako

Zaburi 71:24 “Ulimi wangu nao utasimulia, Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya

Nilishasema kwamba wokovu siyo ujinga, wokovu ni kujua haki zako ukija kuleta ujinga kwangu ninakuwajibisha na mimi situmii mwili natumia neno ndiyo maana ya kutofautishwa, ndiyo maana ukaitwa siyo mtu wa ulimwenguni humu maana yake hata utendaji wako wa mambo ni tofauti kabisa na wa watu wa ulimwengu huu

Ni jukumu letu kutumia ndimi zetu kunena sifa za Bwana kila wakati, nilisema kwamba kama kila siku wewe ni mtu wa kuomba tuu maana kuna watu hawaoni vitu walivyonavyo kila siku wanajiona wamepungukiwa kama upo hivi jua una matatizo, kumpa Mungu sifa ni sehemu muhimu kuliko zote kwenye maisha yako

Wewe ni mtu wa namna gani huoni zuri hata moja la kumsifu Mungu? Vipi afya, vipi ulinzi, vipi familia yako yaani kweli huoni? Badili huo ulimi sasa tumia muda mwingi kusifu kuliko kuomba, au umesahau ukisifu mambo yanazidishwa?  Kumsifu Mungu ni kutambua uweza wake katika maisha yako Zaburi 35:28 “Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa


Itoshe sasa anza kumuita Mungu kwa kinywa chako, muambie unampenda na unalipenda neno lake, mwambie upo tayari kusikia kutoka kwake na utaona mambo yakibadilika kuwa mazuri kwako, Zaburi 66:17 “Nilimwita  kwa kinywa changu…..

Itaendelea tena.....

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote

Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana