MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA TISA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, August 16, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA TISA



Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote ulimwenguni, Jina la Yesu Kristo aliye hai, nina imani kwamba wewe ni mzima na unaendelea vyema na shughuli zako za kila siku

Ninamshukuru Mungu kwa ajili yako na leo tena kwa uweza wa Roho Mtakatifu tutaendelea na somo la malango ya kiroho sehemu ya tisa, huu ni mfululizo maalumu ambao tumeendelea nao kwa takribani juma moja sasa

Usisahau kwamba nilikuahidi kwamba tutakuwa na sala maalumu kwa ajili ya kufungua malango yetu ya kiroho yanayotumika na nguvu za giza kuharibu hatma zetu, hivyo endelea kufuatilia  mafunzo haya


Tulipoishia jana…. 

Mpendwa katika Kristo Yesu, mimi ninaomba ufahamu ukweli huu, maadamu upo katika mwili jua ni lazima majaribu yatakujia 1Kor 10:13 " Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo la kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita muwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili muweze kushahimili

Kama hukujifunza neno la Mungu la jana unaweza⇒⇒ KUBOFYA HAPA KUJIFUNZA


Endelea neno la leo..…

Jana tulianza kipengele muhimu cha njia ambazo Shetani anazitumia kama silaha kuvamia malango yetu ya kiroho na tuliona njia moja ambayo ni njia ya vishawishi, leo tuangalie njia nyingine ya pili ambayo ni kugandamizwa au ugandamizaji


Kugandamizwa ni kitendo cha watu kutawaliwa pasipo haki, ni hali ya kutawaliwa mwili pamoja na akili, ni kumnyima mtu haki, ni kuonea pia kugandamizwa ni kuwa chini ya uonevu fulani (wa Shetani)


Kipindi cha ukoloni wakati nchi za Afrika zinatawaliwa zilikuwa zinagandamizwa na watu walikuwa wanakosa haki, stahiki na uhuru wao katika nchi zao ndio maana ilifikia kipindi ikabidi nchi zingine zipigane ili kudai uhuru wao kutoka kwa wakoloni  mfano nchi Kenya, Zimbabwe, Namibia n.k


Tofauti ya kugandamizwa kwa kipindi cha wakoloni na kugandamizwa na Shetani ni hii kipindi cha ukoloni vita havikuwa vya kiroho bali vilikuwa vya kimwili ndiyo maana ili kupata uhuru ilibidi watu wapigane katika mwili kwa kutumia silaha za moto na za kienyeji na aliyeshinda alipatiwa alichokuwa anakitaka


Historia ya wana wa Israeli pia imejawa na kugandamizwa na mataifa yaliyokuwa na nguvu kwa nyakati tofauti na ndiyo maana walimlilia Mungu wao akawasikia na akawajibu na kuwaondoa katika tawala hizo za uonevu


Maisha ya kiroho pia yapo namna hiyo, Shetani anakandamiza watoto wa Mungu  na kuwatesa kwa mbinu mbalimbali Yohana 10:10 “ Mwizi huja tu kuiba, kuuwa na kuharibu; mimi nilikuja ili wawe na uzima, tena wawe nao tele, Shetani amekuja kuiba vitu ambavyo Mungu amewapatia wana wake


Kaja kuiba muda, kuiba heshima, afya na ndoa za watu pia amekuja kuuwa hatma za watoto wa Mungu, amekuja kuuwa biashara, mahusiano, utumishi n.k na hata vile ambavyo mtu ameshatengeneza yeye kazi yake ni kuharibu ndiyo mana mtu anaweza kufanikiwa sana katika eneo fulani lakini baada ya muda anafilisika na kila kitu kinageuka


Luka 8:26-39 kuna habari ya Mgerasi aliyekuwa anagandamizwa na Shetani kwa kutupiwa Jeshi la pepo wabaya mstari wa 30 unasema  “Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia mtu huyu alikuwa na pepo elfu sita


Jambo jingine katika ugandamizaji wa Shetani ni kwamba huwa hamtupii mtu pepo mchafu mmoja bali wengi kwa mfano  pepo la hasira huja na pepo la kiburi, pepo la kuasi, pepo la kutokusamehe na pepo la kisasi hivyo usifikiri linakuja moja bali ni mengi kwa wakati mmoja


Ndio maana natamani sana utengeneze hasira ya kiungu, ninaposema hasira ya kiungu ninamaanisha hasira ya kiroho na siyo ya kimwili, hasira ya kiroho inamwondoa Shetani na anajua mtu akikasirika kiroho ili tutakapoanza maombi haya maalumu uweze kumwondoa kiulaini


Yesu Kristo kwa kuliona hili aliweka wazi kabisa kusudi la kuja kwake Luka 4:18 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiria masikini Habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kuutangaza mwaka wa Bwana


Tizama tena Mdo 10:38 “Habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huku na huko, akitenda kazi njema na kuwaponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye


Neno kuonewa na Ibilisi tizama tena maana ya kugandamiza ni kuonea, hivyo watu walikuwa chini ya maonevu ya Ibilisi hii ndiyo sababu kubwa wa Yesu kuja  kuihubiri Injili
ukisoma vizuri mistari hiyo yote inaongelea kugandamizwa watu wengi hawataki kukubali kwamba umasikini ni moja ya ugandamizaji wa Shetani kwa wakristo wengi, siyo kusudi la Mungu mtu hata mmoja awe masikini ndio maana alikuja kuwahuiria habari njema masikini ili watoke kwenye umasikini wao, kiroho na kimwili


Neno la Mungu halipindishi jambo 3Yohana 1:2 “Mpenzi ninaomba ufanikiwe katika mambo yako yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo, hivyo hakuna kisingizio cha kuwa masikini kwa mkristo ndio maana unasisitizwa kufanikiwa katika mambo yote

Kama kuna eneo linakutatiza maishani unapaswa kutafuta maarifa juu ya eneo hilo mpaka utakapoweza kulistahimili, utumishi siyo kuomba omba, wala siyo kuwa masikini, utumishi ni kujua ni nini cha kufanya ili Mungu aweze kukubariki nawe uwe baraka kwa wengine


Leo nataka utilie maanani jambo hili Mungu anakupenda kiasi ambacho hata mtu akikufyonya tuu anasimama kukutetea Zaburi 12: 5”Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, sasa nitasimama asema BWANA, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya


Hivyo tafadhali sana usiuchukulie upendo wa Mungu kirahisi rahisi, Mungu anakupenda na anamaanisha, kamwe hataki uangamie ndio maana anafanya kila mbinu na kila namna kukuokoa na hila za mwovu Ibilisi, hivyo na wewe mpe Mungu muda wako


Tenga muda wa kusoma neno lake, kuombea wengine na kuomba kwa ajili yako, kuombea ufalme wake, tafuta muda wa kukaa katika uwepo na Mungu utashangaa mambo ambayo atakuonesha na kukufundisha katika maisha, Mungu yupo sana karibu yako sema hujataka kumpatia muda umsikilize anachotaka kukuambia


Ukaribu wetu na Mungu ni kama mtu na mboni ya jicho lake, tunaanza kuzishika amri zake kama mboni ya jicho letu  Mithali  7:2 “Uzishike amri zangu ukaishi, Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako, kisha tunamuomba atulinde kama mboni ya jicho lake Zaburi 17:8 “Unilinde kama mboni ya jicho na Mungu anatujibu mwenyewe Zakaria 2:8 ….Maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake


Mungu akubariki sana, tutaendelea …..

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636 


No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana