Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo Bwana wetu, nina imani kwamba ni mzima wa afya na unaendelea vyema, karibu tena katika wakati mzuri wa kujifunza neno la Mungu lenye nguvu pamoja nasi, Roho Mtakatifu aliye mwalimu mwema akufundishe na kukufunulia ujumbe ambao ameuandaa kwa ajili yako siku ya leo
Leo tutaendelea na somo letu la malango ya kiroho sehemu ya nane kama hukusoma mfululizo huu wa masomo haya mpaka tulipofikia unaweza⇒⇒⇒ KUBOFYA HAPA KUSOMA YOTE
Tulipoishia.....
Kor 4:20 "Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu, hizi nguvu siyo za mwili ni za Kiroho hivyo ni lazima kujijenga katika eneo la Kiroho matokeo yataonekana nje tuu, watu watamjuaje Yesu tunayemtumikia kama hatendi matendo makuu katika maisha yetu?
Endelea hapa.....
Ni mtu pekee ambaye amegundua siri ndiyo anayeweza kufungua malango yaliyomfunga na kuweza kufurahia wokovu wake, Joshua na Kalebu Mungu aliwapatia siri ya kuyafungua malango ya mji wa Yeriko na waliweza kuitumia siri ile kuingia nchi ya ahadi pamoja na wana wa Israeli, waliuzunguka mji mara sita kimya kimya na mara ya saba walipiga kelele pamoja na shofar na malango ya mji yalibomoka na wakauteka mji
Kila sehemu ya maisha yako ambayo unaona kuna ugumu jua kuna tatizo, Mungu ametutengenezea kila kitu kiende kwa utaratibu maalumu kama unafuata utaratibu na haupati matokeo ni dhahiri kwamba kuna kifungo sehemu fulani kimefungwa na unapaswa kukifungua
Yesu Kristo hakumtamkia Petro neno lolote juu ya kujenga kanisa lake juu yake mpaka Petro alipolijibu swali la Yesu ni nani Mathayo 16: 16 "Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, ufunuo huu Petro alifunuliwa na Mungu mwenyewe
Hivyo kuna mambo ambayo yanakusumbua katika maisha yanahitaji ufunuo kuweza kuyaondoa moja kwa moja, ufunuo unatoa njia ya haraka na ya uhakika ya kutatua changamoto yoyote ile ambayo inamsumbua mtu kwa wakati fulani
Zipo njia mbalimbali ambazo Shetani hutumia kama silaha ya kuvamia kwenye malango yetu ya kiroho, mtu yeyote ambaye anaanguka katika njia hizi huwa ni chakula halali kwa Shetani;
Njia ya kwanza ni vishawishi
Katika njia hii Shetani anamuonesha mtu ni kitu gani atapata kama akikubali kumtumikia, Shetani hana kitu cha kumshawishia mtu zaidi ya vitu vya mwili, hivyo ni lazima atamuonesha umaarufu, magari, thamani na vitu vinavyofanana na hivi
Yesu Kristo alikuwa ni binadamu halisi, aliishi kama mimi na wewe na hakuwa na nguvu za kumwezesha kutenda matendo makuu mpaka alipopokea ubatizo wa maji ambapo Yohana Mbatizaji alimbatiza, ubatizo wa Yohana ulikuwa ni kwa ajili ya toba tuu, wakati Yohana anafikiri yeye ndio anapaswa kubatizwa na Yesu Mathayo 4:15 " inasema Yesu akajibu akamwambia kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kutimiza haki yote. Ndipo akakubali
Elia alikuja kupitia roho ya Yohana Mbatizaji ili kumwandalia Yesu Kristo njia Luka 1:17 "Naye atatangulia mbele yake kwa roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliyotayarishwa
Yesu kubatizwa na maji pekee haikutosha ilibidi aende hatua nyingine kubwa zaidi ambayo ni kubatizwa kwa Roho Mtakatifu ambapo Mathayo 4: 16"....., mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, na kutua juu yake. 17 "...........Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye
Luka 3:21 "Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye akaomba, mbingu zilifunuka;
Kuna somo hapa natamani ulifahamu kwamba baada ya mambo haya kutokea ndipo Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi na hakujaribiwa kwanza ni mpaka alipofunga kwa siku arubaini na akaona njaa Mathayo 4:1-2
Haupaswi kabisa kuruka maandiko kwa sababu kila kitu kinakwenda kwa utaratibu na Mungu wetu ni wa utaratibu, Shetani alikuja kumjaribu Yesu baada ya mambo manne, ubatizo wa maji, kuomba, ubatizo wa Roho Mtakatifu na kufunga hivyo Shetani anapokuletea kishawishi ni lazima uwe umejizatiti katika mambo haya manne ndipo utakapoweza kumshinda vyema
Majaribu yote aliyopewa Yesu na Shetani yalikuwa ni ya kumshawishi, ndiyo maana lugha ya kushawishi watu siyo lugha ya Mungu kwa Mungu kuna lugha mbili tuu ambazo ni ndiyo au hapana na hakuna kufanyiwa maamuzi mtu anayeshawishiwa ni anayefanyiwa maamuzi kwa sababu hawezi kuchagua katika kile anachoambiwa ufunuo 3:16 "Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala hu moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu
Isaya 11:2 " Na Roho ya BWANA itakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na kumcha BWANA, na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA, hivyo roho nyingine yoyote ambayo haitokani na roho hizi siyo roho ya BWANA epuka sana watu wanaotumia lugha za ushawishi
Tizama tena maisha yako leo ni wapi Shetani anatumia kama mlango kukushawishi kutenda mambo ambayo yanakuzuia kuweza kufikia hatma yako ya utukufu ambayo Mungu amekuandalia, kumbuka siyo kila wakati ni waliotutangulia wanatengeneza malango wakati mwingine ni sisi wenyewe na maisha yetu
Mpendwa katika Kristo Yesu, mimi ninaomba ufahamu ukweli huu, maadamu upo katika mwili jua ni lazima majaribu yatakujia 1Kor 10:13 " Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo la kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita muwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili muweze kushahimili
Inaendelea kesho........
Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;
SALA YA TOBA
Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa
Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani
Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.
Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu
Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana
Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana