MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA TANO - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Sunday, August 12, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA TANO

CO-Founder at MT Sialove Lukumay

Bwana Yesu asifiwe! Namshukuru Mungu kwa ajili yako kwa kuwa amekutunza mpaka sasa, na hii ni siku njema na inayopendeza machoni pake na kwetu pia, Hata siku hii ya leo Mungu ana ujumbe maalumu kwa ajili yako na ndiyo maana ninakukaribisha tujifunze neno la Mungu kwa pamoja 


Tunaendelea na mada yenye kichwa cha habari kinachoitwa Malango ya kiroho na leo ni sehemu ya tano, Mungu akubariki sana na kwa uweza wa Roho Mtakatifu akufunulie neno ambalo ameliandaa kwa ajili yako katika Jina la Yesu Kristo


Tulipoishia...


TUNAJUAJE KWAMBA MLANGO NI SAHIHI AU LAA?

Ni kupitia Roho Mtakatifu aliye ndani yetu, Yeye hutushuhudia na hutusemesha mara nyingi juu ya mambo mengi tatizo ni kwamba wengi huwa hawataki kumsikiliza, Paulo alikumbana na changamoto nyingi sana kwenye kuiendeza injili kwa mataifa kwa sababu wakati mwingine alikuwa anashindwa kumsikiliza Roho Mtakatifu, hata kufungwa kwake ni kutokana na kutomtii Roho Mtakatifu pale alipomuambia asiende....


Inaendelea...


Yohana 16:13 “ Lakini Yeye atakapokuja huyo Roho wa kweli,  atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari, hivyo kimsingi Roho Mtakatifu ndie anayetuwezesha kufahamu kama mlango fulani ni sahihi au laa


Inaweza kuwa ni kwa kukupa ishara au kukukosesha amani katika suala unalotaka kuliendea au wakati mwingine utashikwa na huzuni ndani yako au atakuotesha ndoto lakini hakika Yeye hunena nasi juu ya mambo yajayo naam hata yale ambayo tunayotaka kuyaendea

Kama haukusoma neno la Mungu la malango ya kiroho sehemu ya nne unaweza⇒⇒⇒ KUGUSA HAPA KUISOMA YOTE


JE MLANGO USIPOFUNGULIWA UPESI?


Naomba mpaka sehemu hii uelewe kwamba siyo kila mlango unaofungwa ni Mungu kaufunga mingine ni Shetani mkuu wa hila na uwongo huwa ameifunga ili udhani ni Mungu ndio maana ni lazima uwe makini sana kuhakikisha unamsikiliza Roho Mtakatifu aliyeko ndani yako anakushuhudia nini


Yohana 10:27-28 "Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata, nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu


Ni lazima uweze kutofautisha sauti ya Mungu na sauti ya Shetani kwa sababu wote hunena kwa sauti, ndio maana ni lazima kuwa makini sana kuweza kutofautisha sauti hizi ili usipotee na kwenda kwa Shetani 


Kama kuna suala fulani ulikuwa unalifanya na likaharibika au likaanza kwenda kinyume lakini ndani yako unashuhudiwa kuendelea kulifanya basi pambana zaidi katika maombi huenda ni hila za Shetani


Pale Shetani anapofunga mlango wako haumuombi aufungue tafadhali naomba elewa hili, huwa tunamuomba Mungu pekee Shetani haombwi bali anaamrishwa atake asitake lazima aachie mlango wako alioushikilia kwa sababu ni haki yako siyo yake unapaswa kufahamu kwamba haukuumbwa na Shetani na isitoshe siyo binadamu mwenzako lazima afungue atake asitake ataachia katika Jina la Yesu Kristo


Yohana 11:12 “ Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni  hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu huuteka” 1Kor 4:20 “Maana  ufalme wa Mungu hauwi katika neno bali katika nguvu” Nilipoelewa hii mistari miwili nilipona malaria ambayo ilinitesa siku tatu na niliapa sitakunywa dawa mpaka Mungu aniponye peke yake tatizo langu nilikuwa ninaomba tuu kwa Mungu kisha ninasahau sehemu moja ya kumwamrisha Shetani aachie afya yangu


Hasira ya kiroho inaruhusiwa kabisa wakati unasali nilikuwa siwaelewi baadhi ya watumishi ambao huwa wanaomba kwa hasira kudai afya zao na mafanikio yao mpaka Roho Mtakatifu aliponifunulia hii siri kwamba kuna vitu vya kuomba na kuna vitu vya kuamrisha


Mimi binafsi simuheshimu wala sitakaa nimuheshimu Shetani nitampiga kwenye ardhi, kwenye maji, angani, nchi kavu na kila mahali ambapo ninapaswa kumpiga maana nimeshagundua siri ambayo ni kuzipinga hila zake kwa hasira zote za kiungu hapa ndipo unapompiga Shetani mchana kweupe kinyume na hapo atakutesa sana na magonjwa


Somo hili siyo la namna ya kuuteka ufalme ila ni bora uanze kubadili namna unavyoomba inapokuja kwenye suala la kudai haki zako ambazo Mungu ameshakupatia na Shetani amezizuia, Mungu anatupenda kila kitu ameshakiachilia huyu mwovu ndie anayezuia hivyo lazima uwe tayari kumpiga vizuri afungue milango yako


Tambua ya kwamba mlango na ufunguo tuliokuwa tunaouongea hapa ni SIMBA WA KABILA LA YUDA Yohana 10:9 “Mimi ndimi mlango mtu akiingia kwa mimi , ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho hivyo mlango na ufunguo vyote ni Yesu kwa sababu huwezi kumiliki ufunguo wa nyumba ambayo siyo yako ikitokea utakuwa umepanga au umembebea mwenye nyumba


Biblia inatutambua sisi kama kondoo na mchungaji wetu ni Yesu Kristo hivyo anayetulisha na kutufungulia mlango ni Yesu pekee, anatupeleka kwenye malisho ya majani mabichi na anatufungulia milango yetu 

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana