MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA SITA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, August 13, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA SITA

CO-Founder at MT Sialove Lukumay

Bwana Yesu asifiwe..! Ninakusalimu sana kwa Jina takatifu la Bwana wetu Yesu Kristo nikiamini unaendelea vyema pasipo shaka yoyote, ninamshukuru Mungu aliyenipatia kibali cha kuandaa somo hili la malango ya kiroho lakini pia ninamshukuru kwa kukuwezesha wewe kuweza kuingia katika mtandao wetu huu na kujifunza pamoja nasi


Roho Mtakatifu aliye mwalimu mwema na msaidizi wetu ninamuomba akusaidie kuweza kupata ufunuo maalumu uliokusudiwa kwa ajili yako siku hii ya leo, ninaamini kwamba utapokea kile ambacho Mungu amekusudia upate kukipokea na atakuwezsha kukifanyia kazi pasipo kuchoka wala kukata tamaa katika Jina la Yesu Kristo


Tunaendelea na somo letu la malango ya kiroho na leo tunaingia sehemu ya sita ya somo hili, karibu tujifunze kwa pamoja kwa msaada wa Roho Mtakatifu


Tulipoishia...



Neno la Mungu linatutambua sisi kama kondoo na mchungaji wetu ni Yesu Kristo hivyo anayetulisha na kutufungulia mlango ni Yesu pekee, anatupeleka kwenye malisho ya majani mabichi na anatufungulia milango yetu kwa ajili ya sifa zake mwenyewe

Endelea...

Leo kipekee tuangalie moja ya malango ambayo yameelezewa sana katika neno la Mungu ambayo ni malango ya mji, mtu anapotaka kuingia au kutoka katika mji fulani ni lazima apite katika malango ya mji ambayo humuwezesha kutambua kwamba kaingia au katoka katika mji husika

Kila unaposafiri kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine unapokuwa unaingia mji mwingine ni lazima utakutana na kibao chenye maandishi ya kukutaarifu ya kwamba unaingia katika mji mwingine na jina la mji husika litakuwa limeandikwa katika kibao kile kukuonesha kwamba umeingia mji mwingine

Malango hubeba baraka au laana ya mji ndio maana ni muhimu kuyaamrisha malango ya miji kwa ajili ya mafanikio yetu wenyewe, mfano unaposafiri kwenda mkoa mwingine kwa mara ya kwanza hakikisha unazungumza na malango ya mkoa huo unapoingia hii inakusaidia kuweza kufanikiwa katika suala uliloliendea sehemu hiyo 

Kama hukusoma neno la jana la Mungu malango ya kiroho sehemu ya tano unaweza ⇒⇒⇒ KUGUSA HAPA KUISOMA YOTE

Tunafanya hivyo kwa sababu vitu vyote hupita katika malango, hivyo unapoyaamrisha malango unaamrisha kile ambacho umekifuata ndani ya mji kiwe upande wako na unakuwa umejitengenezea njia kwa ajili ya kufanikisha suala lako 

Isaya 62:10 "Piteni, piteni katika malango; itengenezeni njia ya watu, Tutieni, tutieni barabara toeni mawe yake; Twekeni bendera kwa ajili ya makabila ya watu

Matambiko na kafara hufanywa katika malango kwa sababu wachawi na wakuu wa giza wanatambua ya kwamba hiyo ndiyo sehemu pekee ambayo kila mgeni na mwenyeji wa mji ni lazima atapita akiwa anatoka au anaingia, mara nyingi watumishi wengi wamekuwa wanafanya mikutano baadhi ya miji na inakosa nguvu kwa sababu ya kutokufahamu siri hii

Unapoamirisha malango ya mji unakuwa umefanikiwa kuzima nguvu za wakuu wa giza wa mkoa au mji husika na kuruhusu nguvu za Mungu kutamalaki katika kila unachokifanya, kutweka bendera kama ilivyotumika katika mstari huo ni ushindi, baada ya kuyaamrisha malango na kututia barabara na kutoa mawe kinachofuata ni ushindi ambao ni kuweka bendera ya Bwana

Tunazungumza na malango kwa sababu yanasikia yakisemeshwa Zab 24:7-10 "Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia, kitu chochote ambacho kinaonekana kilitokana na kisichoonekana na tunatambua na kusadiki hili kwa njia ya imani

Hivyo malango ni suala la kiroho ndio maana unaweza kuzungumza nayo na yakatii kile ambacho unayaambia kwa sababu umepewa mamlaka ya kufanya hivyo Luka 10:19 " Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na n'ge, na nguvu zote za yule adui wala hakuna kitakachowadhuru

Katika ujenzi wa ukuta wa Yerusalemu, katika kuzinduliwa kwake tunaona pia malango yakitakaswa Neh 12:30 "Makuhani na walawi wakajitakasa, nao wakawatakasa watu, na malango, na ukuta, hivyo hata tunapomaliza ujenzi wa nyumba zetu ni muhimu kutakasa malango na kuta zetu pamoja na watu wa nyumbani kwetu

Kuna baadhi ya sehemu ambazo ukipita katika mji huwa zina makelele au watu wanaoendesha vyombo vya moto wakifika maeneo hayo huwa wanakuwa kama wamewehuka akili, watafanya mambo ya ajabu, watapiga makelele n.k sehemu zile kiroho huwa zina malango ya kuzimu ambayo yanawafanya watu kuwa namna hiyo

Pia kuna sehemu ambazo huwa ajali nyingi zinatokea kwa mfano Morogoro nafahamu sehemu moja inayoitwa mikese karibuni aslimia themanini na tano ya ajali zote za morogoro na zinazouwa watu wengi hutokea eneo hili, sehemu za namna hii pia huwa na milango ya kuzimu inayodai damu za watu

Hivyo ili uweze kupona katika sehemu hizi ambazo malango yake siyo ya haki ni lazima uhakikishe kwamba unamuomba Yesu Kristo akufungulie Zab 118:17 "Nifungulieni malango ya haki, nitaingia na kumshukuru BWANA, hapo ndipo utakapoweza kuzishinda nguvu za malango yasiyo ya haki

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana