MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA PILI - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, August 7, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA PILI


CO-Founders at MT  from left  Pendo Wisso and Sialove Lukumay

Bwana Yesu asifiwe ..! Tunaendelea na mfululizo wa mada mpya ambayo tumeianza jana ya malango ya kiroho, tunapaswa kufahamu ya kwamba malango ya kiroho ndio njia ambayo hutumika kupitisha vitu mbalimbali vinavyotokea kwenye maisha yetu


Jana tuliishia hapa..

Binadamu naye ana milango ambayo vitu hupita kupitia hiyo, milango mikuu miwili ambayo ni macho na masikio, kitu chochote huingia katika akili kupitia masikio au kuona Biblia inasema kwenye Warumi 10:17 “ Basi imani chanzo chake ni kusikia ; na kusikia huja kwa neno la Kristo, Bartimayo kilichoamsha imani yake ni kusikia ndio maana japokuwa hakuwahi kumuona Yesu kwa macho lakini alisikia kwamba anaponya na aliamini ndio maana alipokea uponyaji wake


Endelea hapa.....

Njia nyingine ni kupitia macho yaani kuona, kadhalika pia mlango mwingine ambao vitu hupitia kuingia kwa binadamu ni mdomo na hii hutokea wakati wa kula au wakati wa kunena / kusema jambo fulani


Watu wengi hatma zao zimeharibika kwa sababu ya vyakula ambavyo walikula sehemu fulani, inaweza kuwa kwenye msiba, sherehe au kwenye mgahawa, pia kuna ambao hatma ziliaribika kwa maneno ambayo walitamka au walitamkiwa yakatumika kama mlango wa kuwafunga kiroho


Hivyo kiuhalisia katika ulimwengu huu ambao tunaishi ni muhimu ukatambua ya kwamba kuna milango mikuu mitatu


Kama hukusoma neno la jana la milango ya kiroho sehemu ya kwanza ⇒⇒⇒BOFYA HAPA KUISOMA YOTE


Milango ya Kiroho, tambua hii ni milango ambayo inatumika katika ulimwengu wa kiroho kumbariki au kumaani mtu, tofauti na milango mingine yote milango hii haionekani kwa macho ya nyama, unahitaji kukuwa kiroho ili kuweza kuiona milango hii, ninapoandika milango wa kiroho namaanisha Mungu pamoja na Ulimwengu wa giza 


Milango ya kimwili hii ndio imegawanyika katika macho, masikio na mdomo hakuna namna nyingine ambayo kitu kinaweza kuingia katika mwili isipokuwa kwa njia hizi tatu



Milango ya kidunia, hii inaonekana kwa macho ya nyama kama mlango wa kuingilia miji, mlango wa kuingilia nyumbani, mlango wa kuingilia ofisini kwako, mlango wa kuingia katika uwanja wa mpira n.k, mara nyingi tunapokuwa tuaongelea suala la mlango au malango hatuongelei mlango  huu kwa sababu siyo kina haswa cha matatizo au vifungo ambavyo binadamu anapata

Mbeleni tutakuja kujifunza juu ya malango ya mji na kwa uweza wa Roho Mtakatifu atatufundisha namna ambavyo malango ya miji au malango ya familia au ukoo yanaweza kuwa sababu ya kulaaniwa au kubarikiwa kwetu



Katika milango hii ya Kiroho kuna watu watatu ambao wanaweza kuingia na kusababisha vitu kutokea wa kwanza kabisa ni Mungu mwenyewe na wa pili ni wewe mwenyewe na wa tatu ni Shetani, hivyo usikae ujidanganye Shetani au roho chafu haiwezi kukuvaa au kukuingilia maadamu umeruhusu mlango fulani basi utavamiwa kama kawaida


Biblia inatuambia tuvae silaha za Mungu ili tuweze kumshinda hila za Shetani (Waef 6:11) hii ni kwa sababu hatushindani katika ulimwengu wa damu na nyama bali katika falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili na juu ya majeshi ya pepo wabaya


JE KILA MLANGO NI SAHIHI?


Sio kila mlango unauona umefunguka kwako ni sahihi, isitoshe Shetani amekuwa akitumia vitu ambavyo vinaonekana kama ni sawa ili kuharibu vitu sahihi kwa binadamu wengi na kuwaondoa kwenye makusudi yao na moja ya mlango mkubwa anaoutumia ni fedha au zawadi ambazo tunapatiwa na watu


Wengi wamepoteza utumishi wao na kazi zao kwa kukubali kupokea vitu fulani ambavyo waliona ni sawa au ni haki kwao lakini mwishowe ulikuwa ni majuto ukisoma kitabu cha wafalme utakumbuka kwamba Gehazi msaidizi wa Elisha aliishia kupatwa na ukoma wa Naamani baada ya kuchukua zawadi kwake ambazo Elisha alikataa kupokea


Hivyo kuna milango fulani ambayo Mungu huwa anaifunga kwenye maisha yetu siyo kwa ajili ya kutukomoa au kututesa ila ni kwa ajili ya kutuepusha na mambo ambayo yatatukia mbeleni, ole wako wewe ambaye utaendelea kukumbatia mlango fulani uliofungwa na Mungu


Wakati mwingine Mungu hufungua mlango wa majaribu kwetu ukisoma habari ya Ayubu mlango wa kwanza utaona Mungu alivyokuwa akiongea na Shetani huku Mungu akijitamba na kusikia furaha na faraja kwamba ana mtu ambaye anamtumikia na amesimama katika imani, tunaona baadae Mungu aliruhusu Ayubu kujaribiwa na Shetani


Ayubu 1:12 "BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyonayo yako katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA 



Siku zote unapaswa kukumbuka kwamba Mungu ana mpango na wewe Isaya 55:8 “ Mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA, hivyo hata kama jaribu liwe gumu kiasi gani kama limetoka kwa Mungu hakika una heri kwenye maisha yako, tena Mungu anasema kama vile mbingu zilivyo mbali na nchi ndivyo jinsi njia zake zilivyo tofauti na njia zetu, hivyo muamini Mungu na amini neno lake pia

Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;



SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana