MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 15 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Saturday, August 25, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 15


Nikusalimu katika Jina lipitalo majina yote Jina la Yesu Kristo, ninafuraha na amani moyoni na nina uhakika unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku, nitangulize kuomba radhi kwa kuwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu nilishindwa kuandaa somo la leo asubuhi 

Ninaamini umenisamehe kwa moyo mweupe na jioni ya leo nimeona isipite bila kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kwa sababu Neno ni taa na uzima wetu, tulikubaliana kwamba tutakuwa na maombi ya kufunga malango yanayotutesa, hivyo tuendelee.....

Tulipoishia...


Neno la Mungu ni ngao linakulinda na kila aina ya mashambulizi kwa sababu Neno la Mungu limehakikishwa na Mungu hawezi kwenda kinyume na Neno lake kwa sababu Neno ni Yesu mwenyewe kama hujasoma malango ya Kiroho sehemu ya 14⇒⇒⇒ BOFYA HAPA KUSOMA

Mithali 30:5 "Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio
Yohana 1:1 "Hapo mwanzo palikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu

Tunaendelea....
Tulikubaliana kwamba tukajifunza juu ya damu ya Yesu katika somo lililopita, sijui kama ulipata muda wa kujifunza lakini kwa faida ya wengi nitaelezea kwa kifupi sana juu ya damu ya Yesu, kisha utajifunza mwenyewe kwa wakati wako au kama unatamani kufahamu zaidi kuna kitabu maalumu cha damu ya Yesu kinachoandaliwa

Maombi haya yatakugharimu mambo yafuatayo ni vema kuzingatia na kufanya kwa imani, kumbuka kila kitu kinachofanywa nje ya imani ni dhambi Warumi 14:23 "Na kila tendo lisilo katika imani ni dhambi, hivyo tengeneza imani yako kwanza kabla ya kuanza maombi haya, usijaribu bali fanya na maanisha

Yatafanyika kwa muda wa wiki nzima yaani siku 7 na yanakupasa kuomba mara 4 kwa siku ikijumuisha saa tisa usiku hivyo utaomba saa tisa usiku, saa tatu asubuhi, saa saba mchana, saa kumi na moja jioni na saa tatu usiku

Haya ni maombi ya vita ndiyo maana kuna matumizi ya damu ya Yesu, hivyo ni lazima kujitakasa na kuwafunika wapendwa wako wote, kufunga roho za malipizi na visasi kama usipofanya hivyo inaweza kusababisha maafa sehemu nyingine, zingatia sana hili

Kipindi chote cha maombi haya Neno la Mungu katika mtandao huu litaendelea kama kawaida hivyo usije ukaona neno linaendelea ukafikiri hakuna maombi, mtu yeyote ambaye anafikiri anasumbuliwa na vidonda vya tumbo afunge na afanye maombi haya aone kama havitaisha vyenyewe andaa tuu imani yako

Siku zote saba mchana tutafunga na kufungua jioni saa kumi na moja, kila baada ya kufungua maombi haya  kunywa damu ya Yesu

Kama mbali kabisa na watu walio na mzaha na fanya hii kama aina ya maisha yako, kuwa makini na jambo hili jua haufanyi kwa ajili ya mtu bali kwa ajili yako na kwa ajili ya watoto, wapendwa wako pamoja na ndugu zako kwa ujumla

Tutatumia aina mbili za damu, moja utakunywa nyingine utanyunyiza kabla ya kulala kuzunguka nyumba yako, kama una biashara nyunyiza  ndani na nje ya jengo, na unapotoka nyumbani kwako asubuhi nyunyiza pia

Unaweza kuanza mfungo huu siku yoyote cha muhimu ni kuzingatia siku saba za mfungo zilizovuviwa siku utakayoanza ndiyo utakayomaliza juma linalofuata, hakikisha unasoma kila kitu na kukielewa kabla ya kuanza maombi haya;

Hivyo ninatangaza leo mfungo rasmi Jumatatu ya tarehe 27/8/2018-03/09/2018, siku hii ya leo na kesho tutaitumia kujifunza na kujiandaa na Mungu akutangulie

DAMU YA YESU NI NINI?
Hakuna wokovu kama siyo kwa damu, dhumuni au sababu kubwa ya kuja kwa Yesu ilikuwa ni kuja kuokoa kilichopotea, isingaliwezekana pasipo Yesu kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake hivyo tumefanywa kuwa wapya tena kwa damu ya Yesu

Yohana 3:16 "Kwa maana jinsi Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele

Agano jipya ni juu ya damu, kama tunavyofahamu kwamba uhai wa mtu umebebwa na damu ndiyo maana damu ya Yesu ilimwagwa ili tuweze kurejeshewa uhai ambao tuliupoteza tangia awali kutokana na anguko la Adamu wa kwanza Mwanzo mlango wa 3

Kwa nini damu ya Yesu?

Kuna uhai kwenye damu ya Yesu, uhai wa kiumbe chochote uko katika damu ndiyo maana katika agano la kale na hata sasa sio sahihi kunywa damu ya ya kiumbe Walawi 17:11"Kwa kuwa uhai wa mwili uko katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi damu hiyo juu ya madhabahu, ili kupata upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu, hivyo tunapokunywa damu ya Yesu tunapata uhai mpya ndani ya Yesu Kristo mwenyewe 

Yohana 6:53"Basi Yesu akawambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake mwana wa Adamu na kuinywa damu, hamna uzima ndani yenu

Damu ya Yesu inatusafisha dhambi zetu, binadamu wote wana dhambi ya asili walioirithi kutoka kwa Adamu wa kwanza ambayo ni lazima kila mtu kuitubu na kutakaswa na hii ilitutenga na Mungu kwa sababu Mungu hachangamani na dhambi, damu ya Yesu ilikuja kumwagwa ili kutusafisha na kuondoa ile dhambi Ufunuo 1:5 "...Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,

Damu ya Yesu inatufanya kuwa watakatifu, kumbuka Yesu hakuwa na uchafu wala mawaa wala hakuwa na dhambi, alimwaga damu takatifu ili kusafisha damu zetu zenye dhambi Waebrania 13:12 "Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango

Damu ya Yesu inaleta ukombozi, tunakombolewa kwa neema ambayo tumeipata bure kupitia kumwagika kwa damu ya Yesu Kristo, Waefeso 1:7 "Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, msamaha wa dhambi, sawa sawa na wingi wa neema yake

Damu ya Yesu inanena mema, damu huongea ndiyo maana damu ni uhai wa mtu hii unaweza kulidhihirisha katika Neno la Mungu, na damu inaweza kunena mabaya au mema inategemea ni kitu gani, damu ya Habili ilinena pia Mwanz 4:10 "Akasema, Umefanya nini?, sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi, pia Waebrania 12:24 "Na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili

Damu ya Yesu inatufanya tuweze kuishi naye milele, pasipo damu ya Yesu kumwagika ingekuwa mtu akifa hawezi tena kufufuka milele na kusingekuwa na sababu ya mwisho wa dunia, hivyo mwisho wa dunia upo kwa sababu ya siri ya damu ya Yesu Kristo 1Wathesalonke 5:10 "ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tunakesha au tunalala (kufa)

Damu ya Yesu inaleta ubatizo mpya, tumebatizwa na Yesu katika mauti yake na tumefufuliwa pamoja naye, hivyo kila udhalimu, dhambi, uchafu na uovu tulivizika pamoja naye katika kifo chake Warumi 6:3-4"Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?......kusudi kama Kristo Yesu alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima

Wagalatia 3:27 "Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo, Wakolosai 2:12 "Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu

Damu ya Yesu Kristo imelinunua kanisa, sisi tumenunuliwa na Mungu kupitia damu ya Yesu Kristo, biblia inapotaja kanisa haimaanishi jengo bali watu, hii iathibitisha kwamba hakuna kitu cha bure duniani, Mungu alituumba na bado alitununua, kuna gharama ya kila kitu tunachokitaka maishani, hata kumtumikia Mungu kuna gharama kubwa sana ya kulipa

Matendo 20:28 "Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolonunua kwa damu yake mwenyewe

Kuna kazi nyingi zaidi na matumizi mengi zaidi ya damu ya Yesu hii ni sehemu tuu, ndiyo maana niliandika awali kwamba kujifunza kiundani siri ya damu ya Yesu kuna kitabu maalumu tunakiandaa kitaelezea kiundani

Wokovu hauna maana pasipo damu ya Yesu Kristo, pasipo neno la Mungu, pasipo kanisa, pasipo ubatizo hivyo wokovu unapatikana kupitia siri ya kulikiri Jina la Yesu iliyoletwa kwetu kwa njia ya kumwaga damu yake msalabani, ni sawa na kusema kama Yesu asingalimwaga damu yake takatifu wokovu usingewezekana

Tuingie moja kwa moja katika maombi yetu:

01.ANZA KWA KUSIFU NA KUABUDU 

02.OMBA SALA YA TOBA, NA KUJITAKASA TUMIA ZABURI YA 51

Kwa sababu mfungo huu utahusisha damu ya Yesu nimeandaa sala hii maalumu ambayo utaitumia kubadilisha kimiminika chochote chenye rangi nyekundu, unaweza kununua juisi ya fruto ukaweka kwenye chupa ya maji ya kilimanjaro ukabeba katika pochi yako

03.SALA YA KUBADILI KIMIMINIKA KUWA DAMU YA YESU

Mungu Baba katika Jina la Yesu Kristo, ninakushukuru kwa ukuu wako na kwa kumtoa mwanao wa pekee kufa kwa ajili ya dhambi zangu msalabani, 

Niko hapa niliko kwa ajili ya utukufu wako, ahsante Mungu kwa zawadi ya uhai na kwa kunipenda namna hii, neno lako linasema katika Yohana 15:16 "Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, ahsante Mungu kwa kunichagua

Mkoni mwangu nimeshika (taja jina) na ninakibadilisha kuwa damu ya Yesu sawa na agizo lako kwenye Yohana 6:53 "Basi Yesu akawambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake mwana wa Adamu na kuinywa damu, hamna uzima ndani yenu

Ninakiri kuwa nitapata uzima katika maisha yangu baada ya kunywa damu hii ya Yesu Kristo, kwa sababu damu imebeba uhai wako, kama wewe huwezi kuumwa na mimi kamwe siwezi kuumwa, kama wewe huwezi kulogwa na mimi siwezi, kama wewe huwezi kufungwa na kugandamizwa na Shetani na mimi siwezi kamwe

Kama wewe huwezi kukosa fedha wala dhahabu, wala shaba na mimi kamwe siwezi kukosa kwa sababu wewe ni Mungu na tegemeo langu, ninatamka kwamba damu hii itakuwa kinga yangu katika kila mipango na hila za adui, ninatamka kwamba damu hii itanipatia mali zangu zote za gizani zilizofichwa na adui

Hakuna silaha itakayoinuka katika maisha yangu ikafanikiwa sawa na Isaya 54:17 "Kila silaha itengenezwayo juu yako haitafanikiwa, na kila uimi utakaoinuka juu yako utauhukumu kuwa mkosa
Ninatamka kwa mamlaka uliyonipa mwenyewe kwenye Luka 10:19 "Tazama, nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na n'ge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru

Asante Mungu kwa kubadili (taja jina) kuwa damu ya Yesu, ninapoenda kuitumia ikafanyike kama nilivyoomba katika sala yangu katika Jina la Yesu Kristo, Amen

04.OMBA SALA YA KUWAFUNIKA WAPENDWA WAKO

05.KAMA HAUJAMPOKEA YESU UNA NAFASI NZURI YA KUMPOKEA 

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


06.MAOMBI YA KUJIKOMBOA KWENYE VIFUNGO NA MAGANDAMIZO YA SHETANI

01. Moto wa Roho Mtakatifu, shuka sasa katika maisha yangu, uwa, choma, teketeza na angamiza kila mpango na hila za adui kwenye maisha yangu, katika Jina la Yesu

02.Kila aina ya magandamizo ya kipepo, kichawi, ukoo na familia ungua sasa kwa nguvu ya moto wa Roho Mtakatifu, katika Jina la Yesu

03.Kila hitilafu iliyopo kwenye mwili wangu, inayotokana na kurithi kama magaonjwa ya kisukari, presha, saratani, vidonda vya tumbo, ugumba, kukosa watoto ungua sasa kwa moto wa Roho Mtakatifu na kwa siri ya damu ya Yesu ninatamka uponyaji wa kiungu sasa, katika jina la Yesu

04.(Weka mkono wako kwenye tumbo) kila ina ya nyoka wa kipepo, pamoja na n'ge, kufa sasa, katika Jina la Yesu Kristo

05.Kila aina ya ukungu ulioko katika nyumba yangu, katika biashara yangu, katika kazi yangu, toweka na yeyuka sasa, katika Jina la Yesu Kristo

06.Pepo wachafu mnaoiba ndoto zangu, kufeni sasa, katika Jina la Yesu Kristo

07.Ninarudisha mishale yote mara saba zaidi iliyotumwa ili kuniangamiza kwa mtumaji, na iwe juu yake, na uzao wake, katika Jina la Yesu Kristo

08.Kila aina ya magandamizo ya kurithi katika maisha yangu, kufa sasa, katika Jina la Yesu Kristo

09.Damu ya Yesu na moto wa Roho Mtakatifu, safisha kila kiungo kwenye mwili wangu, katika Jina la Yesu Kristo

10.Ninavunja na ninajiondoa kutoka kwenye maagano ya kurithi, katika Jina la Yesu Kristo

11.Ninatapika kila pando ovu nililokula katika utoto wangu, au nililolishwa katika Jina la Yesu Kristo

12.Eeeh Mungu wangu, ninakuomba uifanye damu ya Yesu ipite katika kila mishipa ya mwili wangu sasa, katika Jina la Yesu

13.Mungu wangu, yatakase macho na masikio yangu ili niweze kuona na kusikia mambo mema kutoka mbinguni, katika Jina la Yesu

14.Moto wa Roho Mtakatifu, nitie mwanga kwa ajili ya utukufu wa Mungu, katika Jina la Yesu

15.Kila tatizo kwenye maisha yangu, ambalo linatokana na uchawi, pokea jawabu la kiungu sasa, katika Jina la Yesu

16.Kila madhabahu ya kipepo katika nyumba yangu, kaangwa na ungua sasa, katika Jina la Yesu

17.Kila sehemu ya siri ambapo uchawi umejificha na unafanyika, onekana sasa na ungua kwa moto wa roho Mtakatifu

18.Kila aina ya uchawi wa ndani ya nchi, na wakimatifa ambao umetengeneza mtandao katika nyumba yangu, vunjika vipande vipande sasa, katika Jina la Yesu

19.Kila aina ya mfumo wa mawasiliano uliojengwa na wachawi na nguvu za giza katika nyumba yangu, changanyikiweni sasa, katika Jina la Yesu

20.Kila aina ya viapo, nadhiri na maagano yaliyofanywa na wachawi walio katika nyumba yangu, yanayoniathiri, haribiwa sasa na damu ya Yesu Kristo

21.Kila kitu changu kilichochukuliwa na wachawi, kinachotumika katika madhabahu zao, kaangwa sasa na moto wa Mungu, katika Jina la Yesu

22.Ninarudisha mazishi ya kichawi, yaliyokuwa yameletwa kwangu kwa kunitupia ugonjwa katika Jina la Yesu Kristo

23.Kila mtego wa kipepo walionitegea, na uanze sasa kumnasa alieutega mwenyewe kisha urudi kwenye familia yake, na kamwe usinipate katika Jina la Yesu

24.Kila ukuta wa kipepo, uliojengwa kwa ajili yangu na mwaribu, pokea radi ya uharibifu sasa kutoka kwa Mungu na bomoka, katika Jina la Yesu

25.Kila kibaraka wa kipepo, aliyetumwa kinyume na maisha yangu, ili kuniharibu na kurudisha hatma yangu nyuma, anguka sasa na kufa mbele yangu, katika Jina la Yesu

26.Kila pepo linalonifanya nipoteze muda, legea na sambaratika, anguka na kufa, katika Jina la Yesu Kristo

27.Mungu wangu, haribu na mteketeze kila mmisri, anayekwenda kinyume nami katika bahari, katika Jina la Yesu Kristo

28.Kila kizuizi kinachoonekana na kisichoonekana, kilichotengenezwa na adui ili kuzuia mbegu zangu zisizae na kuonekana katika maisha yangu, vunjika vipande vipande sasa, katika Jina la Yesu

29.Kila baraka zangu zilizotekwa na adui, naziamuru zianze kunirudia sasa, katika Jina la Yesu

30.Kila mwanaume/mwanamke anayenizuia mimi kufanikiwa, Oh Mungu wangu, tamka kifo chake sasa, katika Jina la Yesu

31.Anza kumshukuru Mungu kwa kukuondoa kwenye vifungo, migandamizo, hila na mipango ya shetani

Ninakutakia maombi mema, yatakayokupatia majibu yako yote katika Jina la Yesu Kristo

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana