MAANA YA NAMBA SABA KIROHO - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Sunday, August 26, 2018

MAANA YA NAMBA SABA KIROHO

Co-Founder at MT Sialove Lukumay

Ninakusalimu kwa Jina lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo Bwana wetu ninatumaini wewe ni mzima wa afya na unaendelea vyema, hii ni siku ambayo BWANA ameifanya, Tutaishangilia na kuifurahia

Leo tumeanza rasmi mfungo wetu wa siku saba, kama tulivyokubaliana na nimeona ni vyema kama nikiandaa somo maalumu kwa nini tunafunga siku saba litasaidia wengi kuweza kuelewa kama hukusoma neno lililopita lenye maombi na mahitaji ya mfungo huu ⇒⇒BONYEZA HAPA TAFADHALI

Tuliishia kwenye sala maalumu kwa ajili ya mfungo huu wa siku saba hivyo hakuna haja ya kuweka sehemu ya mwisho ukibofya hapo juu utakutana na kila kitu kinachohusiana na mfungo huu tunaoanza leo, kumbuka unaweza kuanza wakati wowote zingatia maelekezo pekee


Endelea.....

Mpendwa katika Bwana, hizi siku saba za mfungo hazikuchaguliwa kwa bahati mbaya bali kulikuwa na kusudi kubwa sana la kiroho la kufanya hivyo, na leo tutajifunza kwa pamoja namba saba katika ulimwengu wa roho inamaanisha nini

Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli Yoh 4:24, mfungo ni tendo la kiroho siyo la kimwili kama wengi wanavyodhani, na sababu kubwa ya kufunga ni kuutiisha mwili ili roho ipate nguvu na kuweza kuutawala mwili

Wengi wanashindwa kumtumikia Mungu vizuri na kusikia sauti yake kwa sababu kila muda matumbo yao yamejaa, mwili na roho hupingana na ndiyo maana ukitaka kuwa vizuri zaidi kiroho ni lazima ufunge ili uweze kuutiisha mwili

Wagalatia 5:17 "Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka, hivyo ili tuweze kuleta usawa kati ya mwili na Roho ni lazima tuutiishe mwili kwa kufunga

Jeuri ya mwili ipo kwenye shibe, ndiyo maana waswahili waliwahi kusema shibe mwana malevya na njaa mwana malegeza, kadiri mtu anavyokuwa dhaifu katika mwili ndivyo anavyokuwa na nguvu katika Roho hii ni kama amefunga kwa kusudi maalumu 

Tambua ya kwamba tuamtumikia Mungu katika Roho lakini pia tunatumia miili yetu katika kukamilisha utumishi wetu kwa Mungu, hivyo usiuruhusu mwili kukutawala katika kipindi hiki maalumu kabisa cha mfungo, zidi kukua kifikra na kimarifa kwamba haufungi kwa ajili ya mtu bali kwa ajili yako mwenyewe 


Maana ya namba saba kiroho

Namba saba inamaanisha ukamilifu, inamaanisha vyote, inamaanisha kupumzika, inamaanisha kumaliza na inamaanisha kutoshelezwa, hivyo unavyoanza mfungo huu leo hayo ndiyo mambo ambayo utakayoyapata baada ya kumaliza mfungo 

Mungu ni Mungu mwenye nguvu, anaweza kufanya lolote kwa wakati wowote na likatokea lakini kwa nini alitumia siku saba kukamilisha uumbaji wa dunia? Mwanzo 2:2 "Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya

Siri iko hapa Mungu ana Roho saba Isaya 11:2 " Na Roho ya BWANA itakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na kumcha BWANA, na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA, hivyo katika kila siku unayofunga utajazwa na moja ya roho za Bwana 

Pia katika kitabu cha ufunuo 3:1 "Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo huyo aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba, Ufunuo 4:5 " Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu tizama na ufunuo 5:6

Inawezekana katika maisha yako umekuwa na changamoto ya afya au kipato au kukosa kazi namba saba ni namba ya unabii inayomaanisha shibe au kutoshelezwa, hivyo unavyomaliza huu mfungo tarajia kushiba na kutoshelezwa Mwanzo 41:29 "Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri

Inamaanisha kumtumkia Mungu, Mambo ya walawi 25:8 "Nawe utajihesabia sabato saba za miaka, yaani, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za sabato saba za miaka kwenu, yaani miaka arubaini na tisa (kukamilishwa kabisa)

Inamaanisha utakatifu, Kutoka  35:2 "Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; hivyo unavyotoka katika mfungo huu ni lazima utakasike kwa sababu unatembea katika namba ya kinabii

Namba saba inamaanisha kusamehe na kusamehewa, Mathayo 18:22 "Yesu akamwambia, Sikwambii mara saba, bali hata saba mara sabini, hivyo tarajia kusamehe watu ambao hukuwahi kuweza kuwasamehe kabla, lakini pia tarajia kujisamehe mwenyewe kwa makosa mengi uliyojifanyia mwenyewe na pia tarajia kusamehewa

Inamaanisha kusimama tena upya katika sehemu ambazo ulikuwa umeanguka na kuona kwamba ni mwisho wako, Mithali 24:16 "Kwa maaana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; bali wasio haki hukwazwa na mabaya

Inamaanisha kupata kibali mbele ya watu uliowahi kuwakosea inawezekana kwa ujinga wao wenyewe au kwa ujinga wako Mwanzo 33:3 "Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake,

Inamaanisha kuanguka kwa kuta na malango yote ya kiroho yanayokutesa na kukusumbua Joshua 6:15 "Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ni siku hiyo tuu waliuzunguka mji mara saba, baada ya hapa makuhani walipiga mabaragumu watu wakapiga kelele na kuta za miji zilianguka

Inamaanisha kutakaswa au kutakasika pale ambapo utatumia mafuta, Mambo ya walawi 8:11 "Kisha akanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kuitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na kitako chake, ili kuvitakasa, tarajia utakaso katika siku hizi saba za mfungo na maombi

Inamaanisha kurudi katika hali yako ya awali ambayo Mungu alikuumba nayo ( kuwa safi) 2Wafalme 5:10 "Naye Elisha akampeleka mjumbe, akisema, Nenda ukaoge, katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia 

Inamaanisha kuona vizuri, kuondolewa ukungu katika macho yako kwa vitu ambavyo hukuwa unaviona 1Wafalme 18:43 " Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatizama, na kusema hakuna kitu. Naye akanena, Nenda tena mara saba, Ikawa mara ya saba akasema, Tazama,  wingu linatoka katika bahari

Kumbuka ya kwamba maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi, iliyosafishwa mara saba Zaburi 12:6

Natumaini umezidi kufahamu zaidi siri ya namba saba katika ulimwengu wa Kiroho na umefahamu kwa nini tumefunga kwa siku saba na siyo siku mbili au tatu, Mungu azidi kukubariki na kukupa nguvu katika juma lote hili la mfungo, Amen

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana