Co-Founder at MT Sialove Lukumay |
Ninakusalimu katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, nimejawa na furaha na amani tele siku hii ya leo ninatumaini na wewe ni mzima wa afya na unaendelea vizuri na shughuli zako za kila siku.
Zaburi 118:24 "Siku hii ndiyo aliyoifanya BWANA, Tutaishangilia na kuifurahia, namshukuru sana Mungu kwa neema hii anaotupatia kuweza kujifunza neno lake kila siku, na ninamshukuru kwa ajili yako kwa sababu kiu ya kujifunza haijakuisha
Tukiwa tunaelekea kabisa katika kuimalizia malango ya kiroho ili tuendelee na somo jingine ni wakati mzuri wa kuweza kurudi nyuma na kuangalia vitu vyote tulivyojifunza, kwa sababu hakuna haja ya kujifunza mambo mengi kisha usiyafanyie kazi au usiyaelewe kiundani
Faida kubwa ya mtandao huu ni kwamba Neno moja huzaa neno jingine hivyo hata kama leo ndiyo siku yako ya kwanza kuingia katika mtandao huu bado una nafasi ya kujifunza masomo yote ya nyuma yaliyopita, kama hukusoma malango ya kiroho sehemu ya kumi na tatu ⇒⇒BOFYA HAPA KUSOMA
Tulipoishia.....
Mtu ambaye amempokea Roho Mtakatifu halisi ni lazima kama amesimama kila aina ya magandamizo na vifungo vya Shetani vitamuachia kwa sababu katika kuomba kwake hata Shetani mwenyewe haelewi lugha ambayo anaongea, hivyo ataondoka tuu hii ndiyo siri ya Mungu kuwasiliana nasi
Inaendelea......
Jana tumeanza kipengele kingine muhimu cha njia ambazo mtu anaweza kuizitumia ili kujiondoa kwenye magandamizo ya Shetani na tuliweza kupata wakati mzuri wa kujadiliana njia kuu mbili ambazo ni kutubu na kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, leo tutaendelea tulipoishia jana
Njia ya tatu ni Imani yenye fujo, kama unakumbuka katika kujifunza nimekua nikiandika kwamba tengeneza hasira ya kiungu kwa ajili ya Jumamosi kwenye maombi, Jee hii hasira ya kiungu ninayoizungumzia ni nini? Hasira ya kiungu ni imani yenye fujo, na Imani yenye fujo maana yake ni sikubali mpaka nipate na hakuna cha kunizuia
Watu wengi ni wepesi kukata tamaa haswa wanapoomba juu ya swala moja kwa siku mbili au tatu na kuona hawajapata majibu, wengi wanaona Mungu kawaacha lakini hawaelewi kwamba wanapoacha hata malaika waliotumwa kuwaletea majibu huyarudia njiani
Danieli aliomba sala moja kwa wiki tatu mfululizo, na siyo kwamba Mungu hakuwa amemjibu alishamjibu tangu siku ya kwanza lakini wakati malaika wanaleta majibu kulitokea mapambano makali katika anga mpaka Mikaeli alipoingilia kati ndipo alipopata majibu
Imani yenye fujo ni kunuia moyoni mwako ya kwamba ni lazima nipate hata iweje, sisikilizi tamaduni, sisikilizi neno la mtu, hakuna wa kunizuia, nitapigana mpaka kieleweke, leo ni leo lazima mbivu na mbichi zionekane
Mathayo 11:12 "Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu huuteka, sasa hivi ni watu wenye nguvu tuu ndio wanauteka ufalme wa mbinguni na hauwezi kuwa na nguvu za kutosha kama hauna hasira ya kiungu
Hasira ya kiungu ndiyo inachochewa na imani yenye fujo hivyo huzalisha nguvu za kukuwezesha kuchukua kwa nguvu kila kitu ambacho Shetani amekunyang'anya, kuna viwango mbalimbali vya imani kiwango cha juu kabisa cha imani ni imani yenye fujo
Kuna mtu aliyekuwa anaitwa Bartimayo kwenye Biblia ni mfano wa mtu mwenye imani yenye fujo japokuwa wanafunzi wa Yesu walikuwa wanamzuia asimuone Yesu, wala asiweze kuponywa, lakini kadiri Bartimayo alipokuwa anaambiwa anyamaze ndivyo alivyokuwa anapiga kelele zaidi akisema "Yesu mwana wa Daudi unirehemu
Kumbuka Bartimayo hakuwahi kumuona Yesu, hakuwahi kusoma habari za Yesu ni kwa kusikia tuu habari zake alipaza sauti kwa nguvu zaidi na Yesu alipoiona aina ya imani aliyonayo alimponya
Kuna mambo ambayo watu wanakuambia haiwezekani au ni vigumu kufika sehemu fulani au wanakukatisha tamaa na kukurudisha nyuma lakini ninakuhakikishia kwamba hakuna jambo lolote lile linaloshindikana chini ya hili jua kama una imani yenye fujo ni lazima tuu Yesu atakupatia
Leo una miaka zaidi ya ishirini unasoma Biblia, unaifahamu miujiza aliyoifanya Yesu na manabii, pamoja na mitume mbalimbali lakini bado unashindwa kuamini na kupata uponyaji, hii ni kwa sababu umeridhika na hali yako au hauamini au haupo tayari kujifunza
Kuna baadhi ya mambo hayawezi kukuacha katika maisha yako mpaka uwe na hasira za kutosha mojawapo ya mambo hayo ni vifungo, uponyaji na umasikini, hivyo hasira ya kiroho zinaruhusiwa ila hasira za kimwili ndio haziruhusiwi, mpaka utakapokasirika vya kutosha ndipo utakapoondoka kwenye magandamizo ya Shetani
Haujatoka ulipo kwa sababu umeridhika, unaona ni sawa na unasema moyoni mwako ipo siku, jamani uponyaji siyo fedha uponyaji na kufunguliwa ni suala la papo hapo halihitaji muda ni kuchochea hasira tuu na kuingia kwenye uwanja wa mapambano unamtungua adui unamaliza kazi
Njia ya tatu ni neno la Mungu, kiuhalisia hii ndiyo njia kuu njia zingine zote zinatokea kwenye njia hii, ndiyo maana neno la Mungu ni taa ya maisha yetu kama umeshiba neno vya kutosha hivyo vifungo na magandamizo hata vishawishi vitaondoka vyenyewe
Kuomba, imani yenye fujo, ubatizo wa Roho Mtakatifu, maombi ya vita, kutubu pamoja na wokovu vyote vinatokana na Neno la Mungu ambalo ndiyo Mama anayezaa vyote, hivyo ni lazima utenge muda wa kutosha wa kusoma neno la Mungu, unapojaa neno vitu vingine huondoka vyenyewe pasipo maombi wala kufunga
Neno la Mungu ni moto, linachoma na kuunguza kila pando la adui katika maisha yako ambalo halitokani na Mungu, Neno la Mungu ni nyundo linavunjavunja na kuharibu kila kifungo, magandamizo, na maonevu yote ya Shetani
Yeremia 24:29 "Je! Neno langu si kama moto?Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande, unapoijaza na kuinoa akili yako vya kutosha na neno la Mungu unajiweka katika nafasi nzuri ya kumshinda adui kirahisi
Ushuhuda wa kutokuwa na neno la kutosha ni kuteswa na adui na vifungo mbalimbali ulivyo navyo, hauna haja ya kwenda kwa daktari kupima hili wewe fanya mwenyewe vipimo angalia ni wapi unateseka na kama ipo jua neno ulilonalo halijatosha
Neno ninaloongelea hapa siyo kukariri vifungu vya Biblia na mistari hapana! Ni kujua unapaswa kufanya nini kwa wakati fulani kulingana na neno ni kuwa na ufunuo wa Neno na kulitendea kazi unaweza kufahamu sehemu fulani ya Neno na ukajua kulitumia vyema na matokeo yake yakawa mazuri sana
Neno la Mungu ni ngao linakulinda na kila aina ya mashambulizi kwa sababu Neno la Mungu limehakikishwa na Mungu hawezi kwenda kinyume na Neno lake kwa sababu Neno ni Yesu mwenyewe
Mithali 30:5 "Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio
Yohana 1:1 "Hapo mwanzo palikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu
Kumbuka kesho tutakuwa na yale maombi maalumu hivyo kipekee jiandae na maombi haya kama upo tayari lakini yatakugharimu kufunga itakapobidi, acha kuomba mambo muhimu yanayohusu maisha yako tumbo likiwa limejaa ndiyo maana unasinzia
Mambo ya kuzingatia kesho tutakapoanza maombi haya;
Jifunze namna ya kutumia damu ya Yesu, unaweza kugeuza kitu chochote chenye asili ya kimiminika kuwa damu ya Yesu
Jiandae kupiga photocopy maombi haya sifikiri kama ni wakati wote utaingia kwenye mtandao na kuanza kuomba huku unayasoma lakini kama ni rahisi kwako sawa
Jiandae kuamka kuamka saa tisa kamili usiku kusali, maombi haya utapaswa kuyaomba angalau mara nne kwa siku moja
Kumbuka kwamba kuna vipengee katika kichwa hiki cha Malango ya Kiroho tumeviacha ili tuweze kumaliza somo hili na tuingie jingine, hivyo mbeleni tunaweza kulirudia na kuendelea, Mungu akubariki sana
Tutaendelea tena kesho....
Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;
SALA YA TOBA
Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa
Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani
Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.
Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu
Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana
Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana