MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 13 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, August 22, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 13



Ninakusalimu katika Jina la Bwana Yesu, nina imani ya kwmba ni mzima wa afya na unaendelea vyema na shughuli zako za kila siku, hii ni siku nyingine mpya ambayo Bwana ameifanya unapaswa kuifurahia na kuishangilia

Hongera sana kwa kuwa mmoja wa watu wanaofuatilia kwa ukaribu neno la Mungu linalofundishwa katika mtandao huu, leo kipekee ninaomba nikushirikishe jambo moja muhimu sana tuna wahudhuriaji wengi katika mtandao huu mpaka sasa tuna wahudhuriaji 21,464 lengo kabla ya mwaka huu kuisha tufikie watu 40,000

Hili linawezekana na zaidi kama kila anayetembelea mtandao huu atashea kile anachojifunza na kila anayemfahamu katika simu yake, hivyo kama tunakubariki na wewe kuwa baraka kwa wengine kwa kushea nao neno hili

Kumbuka ya kwamba umebarikiwa ili uwe baraka kwa wengine, na siyo kinyume chake unapopata kitu kizuri ukaona kinakusaidia usifurahie peke yako wafikirie ndugu zako, rafiki zako na jirani zako na uweze kuwashirikisha, Mungu akubariki

Tulipoishia.....

Mungu anakupenda kuliko unavyofikiri ndiyo maana neema aliyoiachilia ni kubwa kliko dhambi ambazo unazifanya, kama siyo hivyo hakuna ambaye angaliweza kupenya katika dunia hii, ndiyo maana hata Mfalme Daudi rafiki wa Mungu alianguka kwenye zinaa lakini hakuruhusu jambo lile limwondoe Mungu maishani mwake aliinuka akatubu na akasamehewa
Warumi 5:20 "Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi 

Tunaendelea...

Jana tuliangalia njia ya tatu ambayo Shetani anatumia kuingia katika malango yetu ya kiroho ambayo ni kumiliki (possession) kwa watu waliookoka na ambao hawajaokoka na tuliweza kuona namna gani hata mtu aliyeokoka kwa wakati fulani anaweza kumilikiwa na Shetani

Kama hukusoma neno la Mungu la Jana malango ya kiroho sehemu ya kumi na mbili unaweza⇉⇉⇉ KUBOFYA HAPA

Leo tunarukia kipengelea kingine na tutaangalia ni njia gani mtu anaweza kuzitumia ili kujiondoa katika magandamizo ya Shetani, na mtu anaweza kusimamia njia hizi na kuweza kuondokana na magandamizo yote ya Shetani

Njia ya kwanza ni kutubu, kukubali kutubu ni hatua ya kwanza ya kuweza kutambua ya kwamba wewe siyo mkamilifu lakini pia ni kujiondoa katika dhambi na vifungo unavyovifahamu na usivyovifahamu, hakuna binadamu aliyekamilika mbele za Mungu Warumi 3:23 "Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu

Tunapotubu tunajiwekea uhakika wa kufanikiwa na kupata rehema Mithali 28:13 "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema, Mungu peke yake anatuita tukatubu dhambi zetu

Kutubu ni kuomba msamaha na kuwa tayari kubadilika na kuenenda na jinsi ambavyo neno la Mungu linavyosema, kila mtu anayetubu dhambi fulani aliyoifanya anapaswa kusamehewa na kuachwa huru Luka 17:3 "Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe na tunapaswa kufahamu kwamba kama hakuna msamaha basi hakuna toba kwa sababu tunatubu ili kusamehewa

Kutubu kunaondoa ngazi na malango halali ambayo Shetani anayo kwenye maisha yako, wengi kati yetu tunapaswa kutubu dhambi tulizozifanya kwa kutumia macho yetu, masikio yetu, midomo yetuna hata mioyo yetu ili tuweze kujiweka safi mbele za Mungu

Tunatubu kwa sababu Mungu ni mtakatiifu na hachangamani na dhambi, na Mungu hataki mtu hata moja aangamie katika dhambi ndio maana anamvumilia kila mtu ili aweze kutubu na kuweza kupata mema aliyomuandalia 


Ukichunguza kiundani utagundua kuwa dhambi kubwa tunazozifanya zipo nje yetu (external to us), lakini kinachozifanya ziwe dhambi ni sisi wenyewe (inner us)
Tupo hapa duniani kwa sababu tuna miili, miili pamoja na fikra zetu ndio inatupelekea kwenye dhambi, siku ambayo roho inapotengana na mwili binadamu hukosa haki ya kuendelea kuwepo duniani

Ndiyo maana Biblia inasema kwenye Mhu 3:20 "Wote huendea mahali pamoja; wote hutoka katika mavumbi; na hata mavumbini hurudi tena


Hivyo miili yetu ndio kikwazo namba moja ambacho kinatufanya tumtende Mungu dhambi ndio maana tunapaswa kufunga na kuomba kila wakati ili tuweze kuitiisha miili yetu na tuweze kukua katika roho


Mungu ni Roho nasi ambao tunaomuabudu inatupasa kumwabudu katika Roho na kweli Yoh 4:24, japokuwa tunamwabudu Mungu na mwili lakini ni katika Roho tunaupata uwepo wake


Hakika ni dhahiri kwamba hatuwezi kuupata uwepo wa Mungu katika hali ya kimwili, ila tunaweza kuusikia uwepo wa Mungu katika mwili pale tunapomuabudu katika Roho na kweli

Tukiwa kama wakristo wenye ufahamu tunatubu kwa sababu dhambi ni chukizo kwa Mungu, pale tuu ambapo unapofanya dhambi na ukashindwa kutubu Mungu hujitenga na wewe

Lakini ni muhimu sana tukafahamu kwamba Mungu atatuona sisi ni wapumbavu kupindukia kama ametupatia nafasi ya kutubu nasi tunaifanya mioyo yetu kuwa migumu 1Yoh 1:9 "Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.

Kwa nini tunatubu dhambi?
Tunatubu ili Mungu aweze kutufutia dhambi zetu naam tuweze kuwa wasafi na kuhesabiwa haki, lakini pia ili tuweze kuburudishwa Mdo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;

Hakujawahi kuwa na raha yoyote katika dhambi kama unataka burudiko na starehe pande zote hauna budi kutubu dhambi zako zote Yoshua 21:44 "Kisha BWANA akawapa raha pande zote, sawasawa na hayo yote aliyokuwa amewaapia baba zao; wala katika adui zao wote hakusimama hata mtu mmoja miongoni mwao mbele zao; yeye BWANA akawatia adui zao wote mikononi mwao.

Unaposikia kupewa raha pande zote ina maana hakuna shida ya aina yoyote ile itakayokusogelea, katika kila upande wa nchi wewe utasitawi na hakuna ambaye atakayeweza kusimama mbele yako

Lakini pia kila ambaye atakayeinuka juu yako Bwana wa majeshi atamtia mikoni mwako yaani huu ni ishindi baada ya ushindi

Tunatubu dhambi ili tuepukane na mabaya, unapodumu katika dhambi unaandamwa na mabaya na ndio maana Mungu ameachilia neema ya kutubu dhambi ili tuweze kurudi kwenye mstari na yale mabaya yatuondoke Yoel 2:13 "rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya

Njia ya pili ni kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, wakati Bwana wetu Yesu Kristo anaondoka alituachia msaidizi ambaye ndiye mwalimu wetu hutongoza katika kila jambo Yohana 14:26 "Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia

Huwezi kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu kama bado upo katika dhambi ndiyo maana njia ya kwanza kabisa ni kutubu dhambi kisha njia zingine hufuata, Roho Mtakatifu ni Mtakatifu kama jina lake lilivyo na hivyo hawezi kuingia katika mwili ulio na uchafu

Kunena kwa lugha mpya ni moja ya kithibitisho kikubwa cha kumpokea Roho Mtakatifu, kila ambaye anaokoka anakuwa kapokea nguvu za Roho Mtakatifu lakini kiwango cha nguvu huofautiana baina ya mtu mmoja hata mwingine, ni vyema kujifunza zaidi juu ya Roho Mtakatifu na uweza wake 

Kuwa makini siyo kila anayenena lugha mpya ananena lugha ya Roho Mtakatifu halisi katika nyakati hizi za mwisho hata pepo wachafu wananena ndiyo maana ubatizo wa Roho Mtakatifu ni lazima uwe ni halisi na kweli kwako kwa ajili ya matendo makuu

Mtu ambaye amempokea Roho Mtakatifu halisi ni lazima kama amesimama kila aina ya magandamizo na vifungo vya Shetani vitamuachia kwa sababu katika kuomba kwake hata Shetani mwenyewe haelewi lugha ambayo anaongea, hivyo ataondoka tuu hii ndiyo siri ya Mungu kuwasiliana nasi

Tutaendelea kesho na njia nyingine......


Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana