MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 12 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, August 21, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 12

Co-Founder at MT Sialove Lukumay

Bwana Yesu Kristo asifiwe! Ninamshukuru Mungu kwa wakati huu mwema ambao ameufanya kwa ajili yetu, ninatumaini unaendelea vyema na mzima wa afya tumekuwa na wakati mzuri katika somo lenye kichwa cha habari Malango ya kiroho na tunaelekea kumalizia somo hili na kama tulivyokubaliana jumamosi tutakuwa na maombi maalumu hivyo endelea kujiandaa

Tulipoishia....

ix/Kugandamizwa kwa kurithi, hii inaambatana na dalili hizi; unapokuwa umeunganishwa na maagano usiyoyafahamu, unapokuwa unaumwa na magonjwa ya kurithi, unapoona tatizo linalofanana linatokea kwa watu wengi katika ukoo mmoja, unaposhiriki ibada za kafara na za wafu, unapohusishwa kwenye uchawi na nguvu za giza, vifo vinavyofanana vinapotokea katika ukoo, inapokuwa vigumu watu kuolewa kwenye familia, uzao unapokuwa changamoto kwenye ukoo nk

Kama hukusoma sehemu ya kumi na moja ya mada hii unaweza⇒⇒ KUBOFYA HAPA

Endelea.....

Tumeona katika makala zilizopita njia mbili ambazo Shetani anatumia kuingilia malango yetu ya kiroho ambazo ni vishawishi na kugandamizwa ambapo kwenye kugandamizwa tumeona kuna aina nyingi za kugandamizwa japo tulijadiliana dalili tuu ili tuweze kuendelea na masomo mengine

Leo kipekee tunaendelea na njia ya tatu ambayo ni kumilikiwa (possessed) na Shetani mwenyewe, sisi tumeombwa na Mungu na ni viumbe wake lakini kuna maagano ukishiriki au kama waliokutangulia walishiriki unakuwa unamilikiwa na Shetani kwa sababu anakuwa na uhalali na maisha yako

Zaburi 100:3 "Jueni ya kwamba BWANA ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake na kondoo wa malisho yake.

Naomba uelewe hili kwamba hii haijalishi umeokoka au haujaokoka ni kwa watu wote na tutaangalia katika pande zote mbili inakuwa namna gani Shetani anaweza kuwa na umiliki kwa mtu kwa wakati fulani

Kumilikiwa kunakuwa ni ndani, yaani anaweka makazi kwa mtu, ndiyo maana Yesu Kristo alitangaza kusudi la kuja kwake namna hii Luka 10:18 "Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema, Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kuona tena, na kuacha huru waliosetwa

Mtu unapokuwa chini ya umiliki wa Shetani inakuwa ni vigumu kuona vitu sahihi kwa sababu anaharibu imani yako na kukuondolea maarifa ya kutambua hata vitu ambavyo vinaonekana kwa macho ya kawaida


i/Kwa wasioamini, 2Kor 4:4 "Ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, wasiione nuru ya Injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu, hivyo mungu wa dunia hii ambaye ni Shetani anaharibu akili za watu na hawaoni kabisa kwamba neno la Mungu ni nuru ya maisha yao

Hakuna mtu ambaye Shetani anamfurahia na anammiliki kirahisi kama asiyeamini kwa sababu anapanda kitu chochote kile anachotaka katika maisha yake, kuna habari ya mpanzi aliepanda mbegu na usiku Shetani akaja kupanda magugu

Kumshinda adui inabidi uweze kujua alikuja ili kufanya nini, Yohana 10:10 "Mwizi huja tu kuiba, kuua na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, tena wawe nao tele, hivyo kusudi lake ni kuiba, kuua na kuharibu hii ni kwa anayeamini na asiyeamini, hivyo haijalishi unafahamu au haufahamu kusudi hili ila linakuhusu

Hosea 4:6 "Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, angalia neno "wanaangamizwa" ina maana kuna mtu/ kitu kinachowaangamiza watu hawa ambacho ni mungu wa dunia hii, kama kwa mfano ingekuwa limeandikwa neno wanaangamia ina maana ni wenyewe

Kama hutaki kuangamizwa ni lazima mahusiano yako na Mungu yawe vizuri ili uweze kutoka kwenye kumilikiwa na Shetani na uwe chini ya umiliki wa Mungu, jua hili ni jukumu lako binafsi usitarajie kusaidiwa na mtu ni wale wanaomtafuta Mungu kwa moyo wao wote ndio wanaomuona, siyo wanaoigiza

Yeremia 29:13 " Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote, hivyo siyo watu wote wanaomtafuta Mungu wakati fulani wanamuona ni wale tuu wanaomtafuta kwa moyo wao wote ndio maana Mungu hujificha ili wale wanaomtafuta kwa moyo wao wote waweze kumona Zaburi 30:7 "BWANA, kwa radhi yako wewe uliimarisha mlima wangu.Uliuficha uso wako nami nikafadhaika

Yesu Kristo katika Biblia ameonekana akilia na akifadhaika moyoni mwake mara mbili mara ya kwanza ni wakati anaingia Yerusalemu, aliuangalia mji akaulilia kwa ajili yake na wakazi wa mji ule kwa sababu ya kukosa maarifa 

Luka 19:41-42 "Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, laiti ungalijua wewe hata siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako, kama Yesu mwenyewe alilia kwa sababu ya watu kukosa maarifa inamaanisha kwamba Shetani anawatesa watu kwa sababu hii pasipo kufahamu


ii/Kwa wanaoamini 2Tim 2:26 "Wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambaye amewanasa, hata wakayafanya mapenzi yake, hii ni kwa mtu ambaye alishaokoka kisha akarudi nyuma kwa kufanya jambo/ mambo fulani

Ukweli ni kwamba kuokoka siyo mwisho wa majaribu ila ni mwanzo wa maisha mapya, mara nyingi Shetani akishamtega mtu aliyeokoka akanasa katika mtego wake anachokifanya ni kumtengenezea roho ya kujikataa na kujiona hafai kwa alichokifanya na hivyo anakuwa chini ya umiliki wake

Kama unataka kujiondoa ukigundua tuu umekosa tubu, jitakase na damu ya Yesu kisha songa mbele kwa sababu jambo hili limewatafuna watu wengi waliookoka na kuwarudisha nyuma kwa sababu tuu hujiona hawafai tena na Yesu hawezi kuwapokea, nataka ufahamu ya kwamba bado una nafasi nzuri sana katika ufalme wa Mungu

Mungu anakupenda kuliko unavyofikiri ndiyo maana neema aliyoiachilia ni kubwa kliko dhambi ambazo unazifanya, kama siyo hivyo hakuna ambaye angaliweza kupenya katika dunia hii, ndiyo maana hata Mfalme Daudi rafiki wa Mungu alianguka kwenye zinaa lakini hakuruhusu jambo lile limwondoe Mungu maishani mwake aliinuka akatubu na akasamehewa


Tutaendelea tena na somo hili kesho......


Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636 



No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana