MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 11 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, August 20, 2018

MALANGO YA KIROHO- SEHEMU YA 11

CO-Founder at MT Sialove Lukumay

Bwana Yesu asifiwe, ninamshukuru Mungu kwa ajili yako na kwa ajili ya Neno lake la uzima, ninashukuru kwa kibali ambacho ametupatia cha kujifunza Neno lake kila siku na kwa ajili ya mtembeo usiokuwa mawaa 

Tumekuwa na kichwa cha habari cha malango ya kiroho kwa muda sana na nimekuwa nikiangalia namna ya kufupisha Neno hili ili tuweze kuingia katika kipengele cha maombi maalumu ambayo nina imani unaendelea kuandaa hasira ya kiroho kwa ajili ya tukio hili

Baada ya kupangilia mada hizi vyema nimependelea jumamosi ndiyo iwe siku ya maombi haya hivyo juma hili tutaendelea na somo hili la malango ya kiroho na itabidi tulifikishe tamati jumamosi hii ili tuweze kuingia katika Neno jingine kama jinsi Roho Mtakatifu atakavyokuwa ananena nasi

Kama haujasoma malango ya kiroho sehemu ya kumi tafadhali ⇉⇉⇉GUSA HAPA


Tulipoishia........


v/Kugandamizwa kimwili kunakuwa namna hii; unahisi kuna vitu haviko sawa ndani ya mwili wako; unapatwa na maumivu yasiyo na sababu; unakosa kuona japo ni mdogo kiumri; unaumwa hovyo bila sababu; unakosa afya na kudhoofika hata kama una fedha; unatupiwa magonjwa na vimbe katika mwili wako; unakuwa rafiki na hospitali; unazeeka kabla ya wakati wako; unapenda kuambatana na watu ambao hamuendani kiumri pasipo sababu za maana; unajihusisha na moja au zaidi ya  matendo ya kimwili kama yalivyoelezwa wagalatia 5:16-21 (soma tafadhali)


Endelea.....

Ninaomba nianze na sentensi hii itakuchukiza lakini utajifunza, Wakristo wengi ni wavivu na pia wamekuwa ni wepesi sana kukubali kushindwa na kuishia kusema namwachia Mungu hata kwa vitu ambavyo ni haki yao kiungu, hali hii imekuwa inampatia Shetani nafasi nzuri ya kuwagandamiza zaidi kwa sababu ni wavivu lakini pia wanakata tamaa mapema

Jambo ambalo hulifahamu litakutesa sana, wengi hawajajua nguvu walizo nazo ndiyo maana hawazitumii au kama wanajua hawajui namna ya kuzitumia au hawaamini au wanafikiri ni watu fulani tuu ndio wanapaswa kutembea katika mtembeo fulani wa nguvu za kiungu

Leo nataka ujifunze neno moja kubwa kwamba Mungu siku zote hatumii watu wenye sifa/vigezo bali Mungu anatumia watu ambao wapo tayari kutumika na ambao wanapatikana hili nimewahi kulisema na nimelirudia tena, wewe kuwa mwaminifu tuu na patikana unapohitajika utaona namna ambavyo Mungu atakutumia

Mimi nimekuwa katika familia ambayo nikiumwa na malaria, kifua au mafua napelekwa hospitali au naenda mwenyewe lakini baada ya kuwa tayari kutumika ninaongea na ugonjwa na unaondoka wenyewe na sina mpango wa kuumwa wala kunywa dawa yoyote tena tangia nimjue Yesu ninayemtangaza

Ninapoongelea kugandamizwa ninaelewa naongelea nini kwa sababu nilikuwa na msimu wa kuumwa kifua, msimu wa malaria, msimu wa mafua n.k lakini ole wake ugonjwa udhubutu kuinuka katika mwili huu kwa sababu utaondoka wenyewe kwa sentensi tatu tuu

Shetani akiwa anamgandamiza mtu katika magonjwa au kitu fulani lengo lake haswa ni kumkosesha furaha mtu yule ili azidi kutumia mwanya huo kumuingizia roho zingine mbaya zinazoambatana na huzuni, kumbuka nilikuambia kwamba roho mbaya inapoomvaa mtu huja na roho zingine ndiyo maana .......

Wafilipi 4:4 inasema "Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema, Furahini, tunasisitizwa kufurahi siku zote kwa sababu tutakapoendekeza roho za huzuni au masononeko ni nafasi kwa Shetani kuingiza roho chafu katika maisha yetu

Hivyo kama unafahamu kuna eneo lolote lile ambalo Shetani anakugandamiza, siyo hekima kumuacha aendelee kukutesa, hakikisha unamwondoa kwa nguvu, chukua hatua na hakuna kukata tamaa katika mapambano haya kwa sababu aliyehakikishiwa kushinda ni wewe na siyo yeye 

Luka 10:19 "Tazama, nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na n'ge na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitakachowadhuru, kushindwa kwa mkristo katika vita vya kiroho ni aamue yeye mwenyewe yaani tunaenda kwenye mashindano na ushindi tunao tayari, umeshaambiwa hakuna kitakachokudhuru ni suala la kujifunza namna ya kupangilia silaha za vita


Njia zingine ambazo Shetani anatumia kugandamiza watoto wa Mungu ni pamoja na hizi tunaendelea jana tuliishia ya tano na tulikubaliana kwamba hatuzielezei kiundani kwa sababu itatuchukua muda mrefu sana kumaliza somo hili


vi/Kugandamizwa katika taaluma, hii huambatana na dalili zifuatazo; kadiri unavyofanya kazi na kuongeza elimu inapaswa cheo kukua na kuongezewa mshahara, unapoona watu wamekuja nyuma yako wana elimu sawa au ndogo kuliko wewe wanapandishwa vyeo na wewe unabakia nyuma jua unagandamizwa sehemu, unapoanya kazi kubwa na hueshimiwi wala kuonekana, mchango wako kazini unapuuzwa na kudharauliwa, unapoingizwa katika kashfa na shutuma ambazo hukushiriki


vii/Kugandamizwa katika lugha/ kauli, hii inaambatana na dalili hizi; umeokoka na bado una lugha ya matusi, unapokuwa unamuongelesha mwenzako vibaya bila sababu, unapokuwa mwepesi kutamka laana badala ya baraka, unapojinenea mabaya badala ya mema, unapoona mabaya kwa wengine na kuyasema hata kama hayakuhusu


viii/Kugandamizwa katika uchawi/wanga, hii inaambatana na dalili hizi; unapowaona wachawi usiku wakikuchezea na unashindwa kuwazuia; unapokuwa unafanishwa kazi na wachawi usiku; unapofanya kazi za kishirikina bila kujijua au kujijua; 


ix/Kugandamizwa kwa kurithi, hii inaambatana na dalili hizi; unapokuwa umeunganishwa na maagano usiyoyafahamu, unapokuwa unaumwa na magonjwa ya kurithi, unapoona tatizo linalofanana linatokea kwa watu wengi katika ukoo mmoja, unaposhiriki ibada za kafara na za wafu, unapohusishwa kwenye uchawi na nguvu za giza, vifo vinavyofanana vinapotokea katika ukoo, inapokuwa vigumu watu kuolewa kwenye familia, uzao unapokuwa changamoto kwenye ukoo nk


Tutaendelea ........


Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636 

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana