KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA SITA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, August 1, 2018

KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA SITA

Co-Founder at MT Sialove Lukumay

Tumekuwa na siku tano mfululizo tukifundisha juu ya mada hii ya kubali kubadilika, leo ni siku ya sita ambapo ninatamani nimalizie mada hii kisha mbeleni kama Roho Mtakatifu ataniruhusu kuendelea nayo nitaendelea



Ninatumaini umeweza kujifunza na kupata mafunuo mengi mapya ya mada hii ya kubali kubadilika na katika siku hii ya leo nitaandika japo kwa ufupi sifa za mabadiliko, jana tuliona vyanzo mbalimbali vya mabadiliko ambapo tuliona ni neno, hali fulani ngumu ya maisha mtu anayoweza kupitia kwa wakati fulana, marafiki/ watu unaohusiana nao


Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya jana na zilizopita unaweza ⇉⇉⇉⇉ GUSA HAPA KUZISOMA



Mabadiliko yana sifa zake, sifa hizi ndizo zinayafanya mabadiliko kuwa mabadiliko, kama tulivyoona makala za nyuma mabadiliko hayabadiliki ili binadamu ndiye anayebadilika na tukaona Mungu ni wa mabadiliko japokuwa Mungu habadiliki



Mwanzilishi wa mabadiliko ni Mungu mwenyewe, yeye ni mbunifu kiasi ambacho hawezi kufanya kitu kwa kurudia kama alivyofanya wakati uliopita, ubunifu ni sifa ambayo inatoka kwa Mungu mwenyewe ndiyo maana anaitwa Mungu wa mizungu mingi yaani namna nyingi



Katika Biblia tumeona Mungu akiponya watu kwa namna mbalimbali, wengine kwa tope, wengine kujichovya kwenye maji, wengine kwa kugusa nguo yake n.k lakini kila mmoja aliponywa kwa namna yake ya kipekee na ya ajabu



Mabadiliko yanaambukiza kwa sababu ni limbuko la imani, chanzo cha mabadiliko ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Mungu, Imani imejengwa juu ya msingi wa neno la imani na ina tabia ya usumaku inavutia watu wengine ambao hawana, ukikaa na mtu mwenye imani kubwa ukaona namna ambavyo anatenda matendo makuu na wewe unavutiwa na kile anachokifanya



Hivyo badiliko moja huandaa njia kwa ajili ya badiliko jingine kubwa zaidi, unapobadilika katika kitu kimoja na ukaona matokeo huwa unaimarika na unatamani kuona mabadiliko katika eneo jingine zaidi, mfano mtu ambaye hajawahi kufanya biashara na kupata faida ya laki moja kwa siku ikitokea akaipata kesho yake atakwenda kwa nguvu zaidi akitaka kupata zaidi



Huwezi kumaliza kubadilika siku moja, wokovu ni ghafla lakini kuishi wokovu ni mchakato ni suala la akili, matendo na roho Warumi 12:2 "Wala msifuate kanuni za dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu



Mabadiliko ni suala linalohusisha kubadili mifumo na taratibu za maisha zilizojijenga kwa muda mrefu ambazo zinahusisha tabia, mazoea pamoja na hisia juu ya mambo fulani, kuziondoa kwa siku moja ni neema ya Mungu lakini ni mara nyingi watu wanaokoka na bado wanafanya tabia walizokuwa nazo awali kama ulevi, uzinzi na ugomvi



Watu wa aina hii siyo kwamba hawajabadilika au hawajaokoka ni kwamba wapo kwenye kipindi cha kufanywa tena upya nia zao na kitu pekee kinachoweza kuwageuza moja kwa moja  ni neno la Mungu, kamwe usikubali kuokoka halafu ukakosa sehemu nzuri ya kujifunza masomo ya kiroho maana ni hakika utarudi sana nyuma



Sababu hii ndiyo inatufanya kila siku tuandae masomo maalumu kwa ajili ya watu waliookoka na wale ambao wanataka kuokoka, wanaweza kuzinoa upya akili zao kwa neno la Mungu na kufanywa upya nia zao na kuthibitika katika imani 



Mabadiliko huambatana na kipindi cha mpito ambapo tabia za awali hukinzana na tabia mpya ambazo zinaanza kutengenezwa, napoliona suala hili usiogope jihusishe zaidi na kusoma neno la Mungu na kuomba hivi ndiyo vitu pekee ambavyo humlinda mtu ambaye yupo kwenye hatua za awali katika kubadilika



Ukomavu wa wokovu ndiyo unaoleta utofauti baina ya watu, mtu aliyedumu katika wokovu kwa muda mrefu na akalisoma neno la Mungu kwa uelewa ana nafasi kubwa zaidi ya kubadilika kuliko aliyeokoka juzi au jana lakini hii inawezekana kwake kama atalisoma neno kwa kulielewa na kuliishi pekee, katika ulimwengu wa kiroho kupitwa ni suala la kaiwada kama haujiungamanishi na neno la Mungu



Mpaka tutakapobadilisha namna tunavyofikiri ndivyo tutakavyobadili maisha yetu, lazima kuwe na mabadiliko ya namna tunavyofanya vitu, tunavyoonekana, mitazamo yetu na namna tunavyoona vitu



Wanaobadilika ni wanaosikiliza neno la Mungu na kulifanyia kazi, tambua kwamba Mungu anatafuta watu ambao hawajakamilika ili awakamilishe kwa kuwabadilisha na kuwafanya kuwa wana wake, hata leo Yesu anakutafuta ili akubadilishe ili upate kutumika katika ufalme wake



Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;



SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636



Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote":

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana