CO-Founder at MT Sialove Lukumay |
Katika somo la jana niliandika kwamba ndiyo mwisho wa mfululizo wa makala hii ya kubali kubadilika ambayo tumekuwa nayo kwa takribani juma moja, lakini Roho Mtakatifu alinikumbusha tena kitu ambacho sikuwa nimekiandika katika mfululizo wa somo hili
Mungu anakupenda sana wewe ndio maana ameona kuna ujumbe huu maalumu ambao haukuupata katika masomo yaliyopita uweze kuupata kisha mambo mengine yaweze kuendelea kama kawaida, ni ombi langu ukutane na Neno lako leo ambalo litakubadili na Mungu akubariki katika Jina la Yesu
Kama hukusoma masomo ya nyuma ya mada hii ya kubali kubadilika unaweza ⇉⇉⇉⇉ KUBOFYA HAPA KUISOMA
Nilipoamua kubadilika na kusimama imara katika wokovu kila kitu kilibadilika na mimi, marafiki zangu niliokuwa naenda nao kwenye starehe walianza kumomonyoka taratibu mmoja baada ya mwingine, ule ukaribu ulianza kupungua na ilifikia kipindi ambacho kuwasiliana ni shida na ikawa ya kujilazimisha
Nilifikiri kuna kitu ambacho hakikuwa sahihi kwangu, hivyo mara nyingi nikawa kama najiuliza kwa nini mbona kila mtu wangu wa karibu ambaye nilikuwa naye kwenye starehe kama ananikaushia na sikupata jibu la kuniridhisha kwa wakati ule
Kiukweli wakati mwingine niliona ni sawa, wakati mwingine niliona siyo sawa lakini jambo la msingi ni kwamba nilikuwa njia panda, kuna watu wengi sana wanasubiria ubadilike ili ukawabadilishe na wao, kama usipokubali kubadilika hawatoweza kubadilika
Kuna rafiki yako, kuna ndugu yako anasubiria tuu wewe ubadilike na yeye aweze kuuchukua ushuhuda wako abadilike na kuwa mpya kabisa, ndiyo maana ni lazima uwe tayari kubadilika ili uwabadilishe wengine kwa utukufu wa Mungu
Hii dunia tunayoishi ina shida na matatizo kwa sababu ni watu wachache sana waliobadilika hivyo madhara ya kubadilika kwao hayawafikii wengi kwa wakati mmoja, ila tukibadilika wengi mguso unaotokana na mabadiliko yetu utawafikia wengi na kuwaleta kwa Kristo Yesu
Mabadiliko ninayoongelea hapa ni ya Kiroho ambayo yanaleta matokeo katika mwili, siongelei upendeze kiroho halafu uwe masikini Hapana na Mungu hataki hivyo, 3Yoh 1:2 "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo
Tunaanza kufanikiwa kiroho kisha mambo mengine yanafuata kama uchumi, afaya, taaluma, kazi, huduma, mahusiano n.k haya ndiyo mabadiliko ninayoongelea tangu somo hili lilipoanza na siyo mabadiliko yanayolenga eneo moja tuu hakuna furaha ya kuwa tajiri halafu ukawa mgonjwa wa kisukari au presha
Sasa ninaelewa kwa nini marafiki zangu walianza kumomonyoka na jibu ni kwamba giza halichangamani na nuru 2Kor 6:14 "Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawa sawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Ukiwa mtoto kiroho ni rahisi sana kurudishwa nyuma na kurudia tabia za awali ndiyo maana Mungu alinitenga nao kipindi kile
Sasa nina jukumu la kuwarudisha kwa Kristo kwa sababu nimesimama katika sehemu nzuri kiroho na ninamshukuru Mungu wengi wao tupo pamoja katika huduma na wanamtumikia Mungu na wengine Mungu anaendelea kuwabadilisha kadiri muda unavyozidi kusogea
Nimeshuhudiwa kuandika hili kwa sababu wapo watu wengi ambao humpokea Yesu Kristo na jambo hili likianza kuwatokea huwa wanaona kuna matatizo sehemu, ukweli ni kwamba hakuna, tena usishangae ukisema umeamua kuanza kumtumikia Mungu hata wazazi wako wakawa kinyume na wewe na kuona hakuna unachokifanya na pengine kukulazimisha ufanye mambo mengine ambayo kwako hayakuletei furaha na utoshelevu
Ninamshukuru sana Mungu kwa sababu ni mwema baada ya muda utofauti huonekana wazi wazi wale waliokuwa wanaona umepotea hao ndio huwa wamepotea, ninaomba nikuachie neno hili kwamba safari ya kubadilika siyo rahisi, Yesu alisema aliye tayari abebe mzigo wake amfuate, siyo amuombe mzazi wake ruhusa au amsikilize ndugu yake
Ukiamua kubadilika achana na tabia za ukinyonga za kugeuka nyuma, ukikubali kufanya hivyo unageuka mke wa Lutu yaani jiwe la chumvi, mkulima ambaye anashika jembe kisha akageuka nyuma hafai katika ufalme wa Mungu Luka 9:62
Tambua ya kwamba mabadiliko huwa yanalindwa, tena hutengenezewa mfumo maalumu wa kuyadumisha kwa kuendelea kuyafanyia kazi siku hadi siku, Wakolosai 3:16 " Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote...." mfumo wa kuyatunza mabadiliko ya kiroho ni kuendelea kujijaza neno la Mungu
Zipo sheli zenye mafuta ya kutosha ya neno la Mungu na katika kipindi hiki hii ni moja ya sheli hizo, hivyo unaingia katika sheli hizo unajifunza neno, unanunua vitabu vya kiroho, lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha unasoma Biblia yako, sheli zinakupatia tafsiri ambazo zilikuwa zinakutatiza awali
Yesu alitengeneza mfumo wa Injili ambao haujawahi kuchakaa na hautokaa uchakae ni mpya kila siku, alianza kwa kutengeneza wanafunzi kwa kuwalisha neno, baadae aliwapa kazi ya kuenda kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi kwa kuwafundisha na kuwabatiza ili kila aaminiye aokoke
Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;
SALA YA TOBA
Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa
Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani
Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.
Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu
Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana
Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636
Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote":
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana