Co-Founders at MT Sialove, Pendo wakiwa na Mwl Pallangyo |
Mabadiliko humfanya mtu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ambayo alikuwa hajaifahamu kwa kuiishi, kwa mfano mtu ambaye ameamua kubadilika na kuanza kujifunza neno la Mungu baada ya muda atakuwa na hekima Zaburi 111:10 "Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima, wote wafanyao hayo wana akili njema, sifa zake zakaa milele
Mabadiliko hayamfanyi mtu kujisikia vizuri mwanzoni, ndiyo maana inakuwa vigumu kwa watu wengi kubadilika, lakini kama umeshalifahamu hili ina maana upo kwenye nafasi nzuri ya kubadilika maana hata kama hujisikii vizuri lakini una uhakika baada ya muda mambo yatakuwa vizuri
Kama hukusoma sehemu ya nne ya makala hii ya kusisimua ya neno la Mungu ya kubali kubadilika⇒⇒⇒⇒ BOFYA HAPA KUISOMA
Mtu ambaye ameanza mazoezi ili kupunguza mafuta mwilini siku za mwanzoni huumwa kwenye viungo vya mwili hii yaweza kuenda hata juma moja lakini kwa sababu afya yake ni ya muhimu kuliko yale maumivu ya viungo huwa haoni shaka kuendelea na mazoezi
Uthamani wa kitu ndiyo unakufanya ukubaliane na kila pambano ambalo inabidi ulishinde ili uweze kupata kile unachohitaji, kilichomfanya Yesu Kristo akubali kuteseka msalabani na kudhihakiwa ni uthamani tuliokuwa nao kwake, Mungu anatupenda maana sisi ni viumbe wake na alituumba kwa sura na mfano wake
Mabadiliko huchochewa, siyo kitu kinachotokea chenyewe, waweza kufundishwa neno fulani au kujifunza kitu fulani na kikabadilisha maisha yako moja kwa moja, hivyo neno huchochea mabadiliko kwa sababu hutoa mwanga juu ya suala fulani Zab 119:105 "Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu
Lakini ili badiliko hilo liwe ni la kudumu ni sharti uliamini neno, mambo yanayotokea mdomoni huwa hayadumu hata siku moja, ndiyo maana mabadiliko ni suala la moyoni mwa mtu binafsi na Mungu wake
Maisha magumu mtu anayopitia kwa wakati fulani yanaweza kuwa chachu ya kusababisha mabadiliko katika maisha yake, ndiyo maana matajiri wengi wametoka katika familia masikini au walipitia changamoto sana, wakati mwingine ili kufikia mabadiliko Mungu anayoyataka maishani mwako hukupitisha katika dhiki
Warumi 5:3 "Wala si hivyo tu, ila mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta subira, hivyo kuna kubadilika ambako ni mpaka mtu apitie changamoto fulani kubwa sana ndio aweze kugundua kwamba anahitajika kubadilika, hili siyo fungu lako katika Jina la Yesu! Mungu akusaidie na akuwezeshe ubadilike sasa wakati huu unaopaswa kubadilika
Watu ambao unahusiana nao wana nafasi kubwa sana ya kukubadilisha na kukupeleka katika uelekeo fulani, kumbuka siyo kila mabadiliko ni mabadiliko mazuri, hata katika Biblia tunaona mabadiliko lakini siyo yote mazuri mfano badiliko la kwanza la Nabii Suleimani kupata hekima ya kuongoza lilikuwa zuri pia badiliko la kujenga hekalu lilikuwa zuri
Badiliko la tatu la kuoa wanawake wa mataifa wakaugeuza moyo wake na kuanza kuabudu miungu yao halikuwa badiliko zuri na alimalizia safari vibaya, ni heri yake mtu yule anayeanza vibaya na kumaliza vizuri kuliko anayemalizia vibaya
Hivyo ukiambatana na watu wanaoliendea na kulipenda neno la Mungu na wewe pia utalipenda na kuliendea neno la Mungu kwa sababu sisi ni wastani wa watu watano ambao tunakaa nao kwa wakati mrefu, mtu mmoja akasema nioneshe rafiki zako nikuambie tabia yako alikuwa na maana sana
Hali hii inatufanya tuwe makini na watu ambao ni marafiki zetu, siyo kila mtu anapaswa kuwa rafiki yako, ni jukumu lako kumpenda kila mtu lakini ni uamuzi wako kuchagua marafiki wa kuambatana nao katika safari yako ya mafanikio
Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;
SALA YA TOBA
Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa
Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani
Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.
Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu
Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana
Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636
Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote":
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana