KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA NNE - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, July 30, 2018

KUBALI KUBADILIKA- SEHEMU YA NNE

Ev. Tedy Stephen

Kukubali kubadilika siyo jambo linalotokea lenyewe kama muujiza bali ni jambo la kufanyia maamuzi, mabadiliko yoyote kama ni ya kukuletea mafanikio huna budi kuyafuata hata kama yatakugharimu


Kukubali kubadilika ndio kunatufanya tukatae kuenenda kwa njia za kale na tamaduni zisizo na mashiko katika maisha yetu, Mungu ni wa kufanya mambo kwa mizungu mingi ndio maana hakuna muujiza unaofanana na mwingine katika Biblia


Tuliona katika makala ya juzi kwamba Mungu ni wa mabadiliko lakini Yeye habadiliki, na tunapokuwa vyombo vya mabadiliko tunaendana na kile ambacho Mungu amekikusudia katika maisha yetu 2Kor 4:16 "Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku hata siku


Watu wengi wanashindwa kubadilika kwa sababu wameridhika na wameruhusu hali zao za sasa kutawala maisha yao, inawawia vigumu kufanya maamuzi ambayo yatabadilisha maisha yao, mtu mwenye hekima anatambua ili hali aliyonayo ibadilike ni lazima yeye abadilike na anatambua pia mabadiliko hayabadiliki ila yeye ndiye anayebadilika


Kama hukusoma sehemu ya tatu ya makala hii ya neno la Mungu ya Kubali kubadilika⇉⇉⇉BOFYA HAPA KUISOMA

Kuna watu ambao wanafikiri nguvu ya kuleta mabadiliko katika maisha yao itasababishwa na mtu mwingine na siyo wao, hawa ni wale ambao hawajaifahamu kweli nayo kweli ikawaweka huru katika maisha yao Yahana 8:32 "Tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru


Hakuna uhuru kwa mtumwa ambaye hazifahamu haki zake, uhuru umeandaliwa kwa mtu ambaye anajielewa na ajitambua ndiyo maana ni mpaka tulipojielewa ndipo tuliweza kupata uhuru, kutaka kubadilika ni ishara ya kutaka kuwa huru, kuhitaji uhuru kunamaanisha kuna stahiki zako umefahamu unapaswa kuzipata lakini huzipati hivyo unachukua hatua ya kutaka kubadilika


Mabadiliko tunayoyahitaji hayapo katika mwili bali katika roho, wengi hufikiri wakibadilisha ratiba na kusikiliza jumbe za kuwahamasisha inatosha kubadili maisha yao, lakini ukweli ni kwamba kama hujakubali kubadilika toka ndani ya moyo wako ni vigumu sana kudumu katika njia unayotaka kuiendea


Maisha tunayoishi yana maana pale tunapotoka ngazi moja kwenda ngazi nyingine kiroho, kiuchumi, kielimu, kitaaluma, kibiashara na hatuangalii uzee kwa umri aliokuwa nao mtu bali kwa vitu anavyojifunza mtu kila siku, hata kama ni kijana na hujifunzi utaitwa mzee na mzee anayejifunza ataitwa kijana kwa sababu kiwango chako cha ufahamu ndiyo kitakachokusaidia kubadilika katika kila eneo la maisha yako


Kamwe Mungu hawezi kumsaidia mtu kuzidi kiwango chake cha uelewa wa kiroho, ndio maana ni muhimu sana kujifunza neno la Mungu ili kuweza kulitumia ipasavyo, wengi wanataabika siyo kwa sababu wanapaswa kutaabika bali hawajui ni nini wanapaswa kufanywa kujiondoa katika nira za mateso waliyonayo


Hosea 4:8 "Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, ukikosa maarifa utaangamia katika Biblia Yesu alihuzunika mara mbili tuu ya kwanza wakati anaingia Yerusalemu na ya pili kwenye kifo cha Lazaro, ukosefu wa maarifa kwa wakazi wa mji wa Yerusalemu ulimfanya Yesu Kristo ahuzunike


Kama jinsi unavyokula ndivyo jinsi unavyotakiwa kuwa na kiu na hamasa ya kutafuta maarifa ya neno la Mungu kwa sababu ukiyakosa unageuka mtaji kwa Shetani na mawakala wake wote, ndio maana ninataka ushikwe na hasira useme kutoka moyoni mwako kwamba nabadilika na nitaanza kujifunza neno la Mungu kwa nguvu, akili na moyo wangu wote


Hakuna kitu kinachobadilika chenyewe kwenye maisha ya mwanadamu isipokuwa mwili wake pekee, vigine vyote vinamhitaji mwanadamu achukue hatua ya imani ili aweze kuvibadilisha na kufanya pambazuko jipya katika maisha yake ya sasa na hata ya baadae


Waliofika sehemu kwenye maisha haya siyo waliokimbia majukumu, siyo waliosingizia hali wanazopitia, siyo waliowalaumu wazazi na ndugu zao bali ni wale waliochukua hatua ya kubadilika na kukabiliana na hali na changamoto wanazozipitia


Hatuyatafuti mabadiliko nje yetu bali tunachunguza ndani kabisa kwenye mioyo yetu ndipo kuna chemchemu ya mabadiliko ya kweli, hakuna kitu kinachobadilika kiuhalisia kama hakijatoka ndani ya kilindi cha moyo wa mtu ndio maana ni muhimu kuuchunga moyo wako Mith 4:23 "Linda sana moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za uzima


Ni lazima usemezane na moyo wako, uuambie sababu za kubadilika ni faida gani utapata, ni kwa nini inakupasa kubadilika wengine hawabadiliki kwa sababu hawajapata muda wa kukaa chini na kupima faida za mabadiliko katika maisha yao


Kaa chini chukua daftari na kalamu yako andika kabisa ni mambo gani huyahitaji katika maisha yako na andika ni mambo gani unayahitaji na ni faida gani utapata ukiyapata na ni hatua gani za mabadiliko unapaswa kuzichukua ili kuweza kufikia mabadiliko unayotaka, yale ambayo huyataki yachane na yachome moto jiapize kwamba utachukua kila hatua ikupasayo kuyaondoa


Kubadilika siyo kuigiza kama watu wengi wanavyofanya katika mitandao ya kijamii na kwenye luninga, kubadilika ni kuuvaa ukweli, ni kusema ukweli juu ya maisha yako pasipo kujali watu watasemaje au watakuonaje, ni kuuvaa uhalisia wa maisha yako na kuchukua hatua


Kubadilika kunaambatana na hisia kali ndiyo maana chimbuko lake ni katika moyo wa mtu husika, hisia hizi ndizo zinazokusukuma uwe na shauku na kiu ya kutaka kuona mabadiliko katika sehemu ambayo inakutatiza katika maisha yako, hakuna mabadiliko kama hakuna hisia kali kutokea moyoni mwa mtu


Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,


Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote



Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;



SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote":

1 comment:

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana