KUBALI KUBADILIKA -SEHEMU YA TATU - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Monday, July 30, 2018

KUBALI KUBADILIKA -SEHEMU YA TATU

MD at MT Mr. Humphrey Makundi
Unapotaka kubadilika usifikirie kutaka kuonekana vizuri, usifikirie kuwafurahisha watu, usifikirie watu wengine wakukubali, Yesu mwana wa Mungu alikataliwa na watu wewe ni nani upendwe na kila mtu, huwezi kumfurahisha kila mtu Isaya 53:3 "Alidharauliwa na kukataliwa na watu;.......


Ukifikiri kwamba kila mtu  atakupenda na kukubali kile ambacho unakifanya hutokaa ukue wala kubadilika, lakini ukitaka kuwa bora na kuboresha unachofanya ni lazima uwe tayari kuchukua hatua stahiki hata kama zitakuumiza



Ni lazima ukubali kwamba utafanya kila liwezekanalo, hata kama watu watakucheka, hata kama watu watakufikiria vibaya, hata kama watu hawatakuelewa, na tambua ya kwamba pale ambapo unapokuwa unaendea kile ambacho Mungu amekukusudia binadamu watakuzuia na kukukatisha tamaa Yoh 1:11 "Alikuja kwake, wala walio wake  hawakumpokea.



Kama haukusoma sehemu ya pili ya makala hii nzuri na ya kuvutia ya neno la Mungu yenye kichwa cha habari Kubali kubadilika sehemu ya pili ⇉⇉⇉BONYEZA HAPA


Yesu Kristo hakujali wala hakuacha habari ya kuhubiri Injili ya ufalme wa mbinguni na kutubu dhambi japokua watu walimkataa na kupinga kile alichokuwa anakifanya, na kubadilika inamaanisha na kuyakubali majukumu yako na kufanya kila liwezekanalo kuyatimiza


Ukiwa unafanya hivi jua kwamba watu hawaishi maisha yako bali wewe ndiye unayeyaishi maisha yako mwenyewe na unahusika katika kuyabadilisha na kuyapa mwanga mpya, unapoanza kumtumikia Mungu na watu wakakuchukia jua ya kwamba wametangaza vita na Mungu, Yoh 15:18"Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kwamba umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi



Kama unataka kuishi maisha ya mafanikio, kama kweli unataka kuwa bora jiandae kuonekana mbaya, kufanya kazi kwa bidii na kwa muda mrefu, kujifunza neno la Mungu pasipo kuchoka, kuomba pasipo mwisho na kukaa muda mrefu peke yako  ili uweze kusikia ule uchungu na uamshe kiu na shauku ya kumsikia Mungu kwa sababu hii ndio njia pekee ya kubadilika


Utasikia uchungu na maumivu mpaka utajiambia mwenyewe imetosha sasa na nahitaji kubadilika, na hapa ndipo Mungu ataingilia masuala yako, wakristo wengi wanamwabudu Mungu kwa midomo na miili yao ila siyo kwa roho zao hawajafahamu kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kubadilika kama hajapatwa na uchungu na akahitaji kubadilika


Lakini kabla hujachukua hatua ya kubadilika utasikia uchungu sana vinginevyo utaendelea kubakia hapo ulipo, ni uchungu wa kuona watu wa Mungu wanapotea  unafanya mtu akavune nafsi, ni uchungu wa kuona mwenzako anateseka unakufanya umuombee kwa mzigo, ni uchungu wa kuumwa unaamsha hasira ya kiungu na imani ya fujo ya kuukemea ugonjwa unaokusumbua


Kiburi chetu (Ego) kinataka tuendelee kuonekana vizuri mbele za watu, unataka watu wakukubali na ndiyo maana ukiambiwa juu ya mambo ya kiroho unadharau, ukiambiwa ujihusishe na uvunaji wa nafsi unaona siyo kazi yako, ukiambiwa toa fungu la kumi unaona unaibiwa, ukiambiwa funga kwa ajili yako na familia yako unapuuzia lakini kama unataka kubadilika na kuwa mpya ni lazima ukubaliane na ukweli na ukweli utakuweka huru


Uhuru wowote ule tunaoutaka maishani mwetu una gharama, mbinguni na hata duniani hakuna vyakula vya bure, 2Thel 3:10 "Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula, kama unataka kuwa huru na kupata kila unachotaka fanya kazi na tii amri za Mungu


Ikabili hofu ya kukubali kusemwa vibaya na kudhihakiwa, ikabili hofu ya kutokujali ni nini watu watakufikiria kwa sababu tunaishi mara moja tuu, wengi watasumbuliwa na ule msemo wa fainali uzeeni, kipindi hiki ungali una nguvu ni lazima kufanya kazi kwa nguvu na kwa akili, ni lazima kuomba, ni lazima kumkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako



Hebu jiulize ni maisha ya mtu gani unaishi, je unataka kuishi maisha ya rafiki zako, unataka kuishi maisha ya babu zako, unataka kuishi maisha ya wazazi au ndugu zako? Kama jibu ni hapana kwa nini unakaa kufikiria ni nini ambacho wao wanakufikiria? Kama kweli ni hapana umekuwa unasikia habari za Yesu Kristo kwa nini umeufanya moyo wako kuwa mgumu?



Kumbuka hakuna kitakachofanya kazi kama usipomkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi ya maisha yako leo, anayeleta mabadiliko halisi na ya kweli ni Yesu peke yake ndiyo maana leo anakuambia Hebr 3:15 "Leo kama mtaisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu kuwa migumu, kama wakati wa kuasi,


Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote


Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;


SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani


Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana



Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote":

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana