TENGENEZA MUDA WA KITU! - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Sunday, July 22, 2018

TENGENEZA MUDA WA KITU!



CO-Founder of MT Sialove Lukumay

Mhubiri Mh 3:1-8 akasema kila jambo na wakati wake, kuna wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna, wakati wa kuomboleza  na wakati wa kucheka, wakati wa kupata na wakati wa kukosa, wakati wa vita na wakati wa amani

Kama hukusoma makala ya subira yavuta heri sehemu ya pili⇉⇉⇉⇉ GUSA HAPA KUISOMA

Unapochanganya nyakati inakuwa vigumu kufanikisha mipango yako, kwa sababu kila jambo hufanyika kwa wakati uliokusudiwa, ni jambo la ajabu wakati wenzako wanavuna wewe ukaenda kupanda, watu watakushangaa


Haupaswi kujisifu kwa ajili ya kesho, kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja (Mithali 27:1) tunajiandaa kwa ajili ya kesho leo, kujisifu siyo sifa ya mwanadamu, sifa ni za Mungu pekee pale ambapo mtu anaanza kujisifu juu ya mambo yajayo anamuondoa Mungu kwenye nafasi yake

Tunapaswa kutambua kwamba tunaishi kwenye ulimwengu wa sasa ambao unatuandaa kwa ajili ya ulimwengu ujao, hivyo ulimwengu wa sasa siyo muhimu kuliko ujao, huu utapita ila ujao ni wa milele 

Jambo linalopaswa kufanyika leo halina budi kufanyika kikamilifu na kwa wakati kwa sababu hujui nini kitatokea dakika tatu zijazo, ndio maana Mungu amejifunua kwetu kwa namna ya tofauti sana unaweza kuwasiliana naye kwa wakati wowote ule hataki uairishe mambo yako

Wote tumepewa masaa 24 lakini matumizi ya masaa haya ndiyo huleta utofauti baina ya mtu mmoja na mwingine, wakati umelala wenzio wanafanya kazi, wakati unazunguka na kupiga stori wenzio wanapangilia maisha yao na kumuomba Mungu awaoneshe njia

Nimewahi kujiuliza ni kwa nini kuna watu wengine ni watumiaji wazuri wa muda na wengine hawawezi kabisa lakini sikuwahi kupata jibu, lakini baada ya kutafakari sana nimepata jibu hili ambalo ninafikiri linaweza kukusaidia na wewe

Namna ambavyo unatoa umuhimu na kipaumbele kwenye shughuli zako ndiyo inayosababisha mtu mmoja kuonekana bora zaidi ya mwingine

Muda na Mungu!!!!!

Hatuna budi kutengeneza muda na Mungu (Zaburi 55:16-17 ) "Nami nitamwita Mungu na Bwana ataniokoa, jioni, asubuhi na adhuhuri,

Biblia inamuelezea mfalme Daudi kama mtu ambaye alitengeneza muda wa kutosha na Mungu katika kushukuru na kuomba, aliwasiliana na Mungu mara kumi kwa siku Zaburi 119:114 "Mara saba kila siku nitakusifu, kwa sababu ya hukumu za haki yako, Zaburi 55:17 "Jioni, asubuhi na adhuhuri nitalalama na kuugua, naye atasikia sauti yangu

Unapotengeneza muda kwa ajili ya kuwasiliana na Mungu huwa tayari kukusaidia wakati wowote, ukisoma habari za Daudi yeye ndiye Mfalme wa Israel ambaye alipigana vita vingi kuliko wote na hakuwahi kushindwa hata siku moja, siri ni kwamba alikuwa ametengeneza muda wa kutosha na Mungu na alimtanguliza Mungu katika kila kitu

Kabla ya kwenda kupigana vita alikuwa lazima amuulize Mungu kama anapaswa kwenda katika vita hivyo au laa na kama atakwenda Jee atashinda? Mungu alipomuambia atashinda ndipo anapokwenda katika vita

Lakini pia nimejifunza kitu kingine kikubwa kwamba katika maisha kamwe huwezi kupata muda wa kufanya kitu chochote, kama unataka muda wa kufanya kitu ni lazima uutengeneze naam lazima utenge muda kwa ajili ya kitu fulani unachotaka kukifanya

Hii ndiyo maana mwandishi Suleiman akasema "Chochote mikono yako yaweza kukifanya, fanya kwa nguvu zako zote na akili yako pia, akiwa na maana usifanye vitu nusu kwa sababu hakutakuwa na matumizi mazuri ya muda, lakini pia hakutakuwa na utofauti mkubwa sana baina yako na ambaye hakufanya, anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi na vitu kwa utimilifu

Hivyo kiuhalisia neno nipo bize halipo kilichopo ni kwamba mtu huwa hajatengeneza muda wa kufanya jambo fulani

Wakati mwingine unapoomba miadi na mtu fulani akakuambia nipo bize jua kwamba alishatengeneza muda kwa ajili ya vitu vingine hivyo unapaswa kusubiri mpaka atengeneze muda kwa ajili yako

Kama unashauku ya kujiunga na grupu la wanawake linalojifunza neno la Mungu kwa pamoja unakaribishwa kujiunga nasi kwa whatsup number 0715113636

Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana