![]() |
Gospel Singer Angel Bernad and MD of MT Humphrey Makundi |
Jana tuliona sehemu ya kwanza ya makala hii ya Moyo wa Subira, leo tunaendelea na sehemu ya pili ya makala hii kama haukusoma sehemu ya kwanza ⇉⇉⇉ GUSA HAPA KUISOMA
Moyo wa subira unahitajika katika kila kitu ambacho mwanadamu anafanya chini ya jua, iwe ni uongozi, biashara, huduma, kazi, utumishi n.k, ukweli ni kwamba hakuna kitu ambacho huanza leo na kufikia mafanikio leo
Katika kitabu cha Luka 15:11-32 kuna habari ya mwana mpotevu, huyu alidai sehemu ya mali ambayo inamuangukia baba yake angali ana nguvu na yeye mwenyewe, kilichomfanya afanye vile ni kukosa moyo wa subira, hekima, maarifa pamoja na tamaa
Tunapokuwa na moyo wa subira tunakuwa na uvumilivu na tunatambua ya kwamba kila kitu hutokea katika wakati maalumu ambao umekusudiwa na Mungu mwenyewe na siyo sisi.
Samweli alimpaka mafuta Daudi kama mfalme wa Israeli alipokuwa na miaka 17 na ndio maana wakati wana wa Jese wanapita mmoja mmoja kwake amchague ambaye Mungu amempenda hawakumfikiria Daudi sababu alikuwa mdogo sana, kiumbo na kiumri
Ilimchukua miaka 12 zaidi ndipo alipokuwa mfalme wa Israel kwani alianza kuongoza akiwa na miaka 30 2 Samweli 4:5 "Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini
Jaribu kutafakari kipindi hicho chote Daudi alikuwa ameshafahamu yeye ni mfalme lakini hakuwa na pupa ya kwenda kumuondoa Sauli madarakani, na ukumbuke pia Daudi alipata kibali mbele ya Mfalme Sauli na huku akifahamu kabisa yeye ndiye Mfalme wa Israeli ambaye anafuata
Moyo wa subira ndio uliomfanya Daudi akaweza kusubiria mpaka wakati ambao Mungu alikuwa ameukusudia, Biblia imeweka wazi kwamba zaidi ya mara tatu Sauli alimvizia Daudi ili amuuwe baada ya Daudi kupata kibali mbele ya Waisraeli
Lakini Daudi hakuwahi kutaka kumuuwa Sauli wala hakuwahi kupanga njama za kumuuwa sababu alikuwa na moyo wa subira alitambua fika kuna wakati wa Mungu ambao ukishafika ufalme wa Sauli utaanguka naye ataingia madarakani
Mungu anapokuonesha ukuu aliokuandalia usijifanye una haraka sana kuufikia wewe kuwa na subira fanya kwa kusikiliza sauti yake na kile ambacho anakuambia, jana nilisema ni bora ukachelewa lakini ukaenda kwa njia sahihi watu wengi wametegwa na wamekumbana na majaribu na mateso kwa sababu walitaka kuharakia mambo
Hatuna budi kujitengenezea moyo wa subira na kuhakikisha tunasimama katika kusudi la Mungu na tumruhusu Mungu apigane vita kwa ajili yetu, vita ambavyo Daudi alikuwa akipigana havikuwa vya kwake bali ni Mungu peke yake ndiye aliyempigania
Kama haukusoma makala ya Mruhusu Mungu apigane vita vyako ⇒⇒⇒GUSA HAPA KUISOMA
Jambo ambalo wakristo wengi hawlifahamu ni kwamba wanafikiri kuokoka tuu ndio wamemaliza kila kitu, hawajui ya kwamba hata kwenda mbinguni kwa Baba yetu kunahitaji uvumilivu Mathayo 24:13 "Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka
Hivyo katika ukristo na wokovu wetu hasa nyakati hizi za miisho ya dunia ambapo kuna watu ambao wanawasaliti kwa sababu tuu ya kumtumikia Mungu, ambapo kumeibuka kundi kubwa la manabii wa uwongo wanaopotosha watu, ambapo maasi yameongezeka na upendo umepotea wale tuu ambao watavumilia ndio watakaookoka
Habakuki 2:3 "Maana njozi hii ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikia mwisho wake, wala haitasema uwongo; ijapokawia ingojee kwa maana haina budi kuja, haitakawia, hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kuvumilia kila jambo ambalo Mungu anatuambia juu ya maisha yetu
Mungu anatuambia njozi/ ndoto/ maono ni kwa wakati ulioamriwa, kuna kipindi maalumu ambacho Mungu amekiandaa kwa kila kusudi la mtu hapa duniani, kipindi hicho ni muhimu sana kuzingatiwa kwa sababu ndicho kinachoamua ufanikiwe au usifanikiwe katika kusudi hilo
Mungu anasema mwenyewe ijapokawia ingojee maana haina budi kuja hapa ndipo moyo wa subira unapohitajika, wengi huwa hawapo tayari kusubiria kile ambacho Mungu amewaandalia, hutaka kukipata kabla ya wakati wake ambapo ni kwenda kinyume na neno la Mungu
Wakati wa Mungu ndio wakati sahihi kwa sababu Mungu huandaa mazingira maalumu kwa ajili ya kukuwezesha kutimiza kusudi lako pasipo kutumia nguvu nyingi, Mungu huandaa watu, huandaa vifaa na kila kitu kwa wakati ambao ameuamuru Yeye peke yake siyo sisi
Mwimbaji mmoja wa nyimbo za injili nchini Kenya anayeitwa Guardian Angel akishirikiana na Paul Clement wa Tanzania wameufananisha wakati wa Mungu kama upepo mkali, kama tsunami ya maji wanaendelea kusema hakuna anayeweza kuuzuia kama haujauona wimbo huo⇉⇉⇉ GUSA HAPA KUUTIZAMA
Kama sasa unahangaika sana kutimiza kitu fulani na umefanya kila njia imeshindikana jua kwamba wakati ulioamriwa haujafika utakapofika kila kitu kitakaa katika mkao ambao unatakiwa na hautatumia nguvu nyingi
Kila mtu hufanikiwa katika wakati wake na njia yake, usiumie roho kuona rafiki yako au ndugu yako anafanikiwa katika jambo fulani, unachopaswa kufanya ni kuimarisha mahusiano yako na Mungu na kuendelea kuliamini Neno lake na ahadi zake katika maisha yako
Zaburi 37:7 "Utulie mbele za Bwana nawe umngojee kwa subira; Usihangaike juu ya afanikiwaye katika njia yake, wala mtu apangaye maovu, tambua siyo kila mafanikio hutoka kwa BWANA ndiyo maana unaambiwa usihangaike sababu haufahamu mtu alivyofanikisha mambo yake.
Inaendelea......
Kama una kiu na shauku ya kujiunga na mtandao wa wanawake wanaojifunza neno la Mungu kwa pamoja, wanaofunga, kuomba kwa pamoja unaweza kuwa mmoja wao nawe ukapata kulifahamu kusudi lako, wasiliana nasi kwa simu namba 0715113636 inapatikana whatsup pia, shea ujumbe huu kama umekubariki na Mungu akubariki sana
Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana