WANAWAKE WALIOCHUKUA HATUA ZA HATARI KWENYE BIBLIA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, November 20, 2018

WANAWAKE WALIOCHUKUA HATUA ZA HATARI KWENYE BIBLIA


Bwana Yesu asifiwe! Ni siku njema sana ambayo Bwana ameifanya kwa ajili yetu na tutaishangilia na kuifurahia, nina matumaini kwamba unaendelea vizuri na kazi zako za kila siku pasipo matatizo yoyote, nikukaribishe tena tujifunze neno la Mungu kwa pamoja

Tulipoishiia
Juma lililopita tulikuwa na somo lililokuwa na kichwa cha habari "Mtumwa ni nani" lakini ninasikitika kwamba imenibidi kukatiza lile somo kwa sababu ya changamoto zilizojitokeza, awali ya yote nilikuwa nina uhakika tungetembea na kichwa hiki mpaka mwisho wa mwaka huu kwa sababu ni somo refu sana na lina mambo mengi

Lakini facebook wanazuia post zote zenye kichwa hiki na kusema namna hii "The post goes against our community, so no one else can see it" yaani makala inakwenda kinyume na taratibu zetu, hivyo hakuna wa kuiona, makala zote zimefungiwa na nimejaribu kuripoti tangu wiki jana pasipo mafanikio, hili limeathiri hata wafuatiliaji wa masomo yetu walipungua kwa sababu makala hazikuwa zikioneshwa 

Hivyo nilipata wazo jipya masomo yale kipekee yatakuwa kwenye vitabu vitatu tutakavyoviandaa mbeleni kwa ajili ya utukufu wa Bwana, hivyo jiandae kwa ajili ya ujio wa vitabu hivyo na mbeleni ndiyo masomo yalikuwa mazuri zaidi

Kama mpaka facebook wanaona neno Mtumwa siyo sahihi jiulize wewe uliyeokoka na unakubali kuitwa mtumwa wa Bwana, huu pia uwe ni ushahidi tosha kwako kwamba neno mtumwa kama lilivyotumika kwenye Biblia baadhi ya sehemu halikuwa sahihi kama hukusoma mfululizo huo⇒⇒⇒ Bofya hapa kuusoma wote 

Tuendelee
Kuchukua hatua za hatari ni kuwa tayari kwa lolote litakalotokea, ni kuhatarisha maisha yako, ni kuwa kufanya vitu nje ya utaratibu uliozoeleka,  n.k ni kuuambia uwoga hapana na kufanya jambo jema ambalo unaamini ya kwamba lina manufaa

Watu wengi katika maisha ya leo hawejaweza kufika sehemu ambayo walitamani kufika kwa sababu hawapo tayari kuchukua hatua za hatari, hawapo tayari kufanya vitu vipya ambavyo watu wengine hawajawahi kufanya na ndio maana wamebakia pale walipo kwa miaka nenda rudi

Katika Biblia tuna wanawake ambao walichukua hatua za hatari na kufanya vitu tofauti kabisa na matarajio ya watu, kumbuka kazi ya kuieneza Injili haikuwa rahisi kwa Bwana Yesu Kristo alikutana na upinzani mwingi sana kutoka kwa adui, lakini katika hilo bado kuna wanawake walijitosa kufanya nae kazi na kumuacha Mungu aingilie kati maamuzi mazito waliyoyafanya

Unapomuacha Mungu kuingilia kati mambo yako wewe unakuwa mtizamaji na yeye anakamata usukani, kumbuka siyo watu wote wanaoshinda hupigana, wenye busara humwachia Mungu apigane kwa ajili yao vita vinapokuwa vikubwa nao hushinda kwa kishindo

2Nyak 20:14 "Akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati, BWANA anawaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu"

Wanawake hawa walisema ndio pasipo kusita japo ndio zao zilikuwa zinahatarisha maisha yao kwa asilimia kubwa, tuanze na wa kwanza;

RAHABU, habari yake utaipata kitabu cha Yoshua mlango wa pili, huyu alikuwa mwanamke kahaba ndiye aliyewaficha wapelelezi katika dari yake, hata pale mfalme alipotuma watu waingie ndani kwake alisema Yoshua 2:4 "Yule mwanamke akawatwaa wale watu wawili, akawaficha akasema, Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka"

Japokuwa Rahabu alijua nini kitatokea katika nchi ile lakini alikubali kuchukua hatua za hatari kwa kuwaficha watu wa Mungu, kumbuka ni upelelezi huu uliowapatia wana wa Israeli nchi ya Ahadi, hivyo hapa tunaona Rahabu alishiriki katika tukio hili kwa kutengeneza mazingira japo yalikuwa ni hatarishi kwake

Waebrania 11:31 "Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani" aliweza kutumia nafasi vizuri na akaponea hapo

Na kwa sababu wanawake wapo kwa ajili ya familia, Rahabu alifanya hivi kwa ajili ya kuilinda familia yake hata Joshua na pamoja na jeshi la Israel walipokuja kuiteka nchi familia ya Rahabu iliokolewa na haikuguswa

                      YESU NI BWANA!

Tutaendelea tena kesho.......!
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA 

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.

Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 
Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana
Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana