CO-Founder at Mwanamke Thamani (MT) Sialove Lukumay |
Nilikuwa mtu wa kuigiza maisha, kuishi tofauti na ninachokipata na pia nilifikiri ninaweza kupata kila ninachokitaka kwa wakati mmoja, nilisahau kwamba Mungu hutupatia vitu tunavyohitaji kwa wakati sahihi
Hii ilipelekea kuwa na maisha ya ajabu, yasiyopendeza watu, kudharauliwa, kujadiliwa na kukashifiwa
Kama haukusoma makala ya jana ya Mungu hujibu kwa wakati ⇉⇉⇉BOFYA HAPA KUISOMA YOTE
Lakini Roho wa Bwana akaaye ndani yetu hakuwahi kukata tamaa juu yangu, kile alichokuwa amekiweka alikuwa anasema haya yatapita na utakuwa mpya
Dhambi humtenga mtu na uso wa Bwana na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, Warumi 3:23 "Kwa maana wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
Nafasi hii kaitoa kwa kila mtu haijalishi umefanya maovu mangapi, maasi kiasi gani Mungu bado anakupenda na anakuhitaji katika ufalme wake, tunaheabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu
Na ukweli ni kwamba watu ambao wamebeba kusudi la Bwana huwa wanaandamwa sana na Shetani sababu anajua huwa wanakuja kuuvunja ufalme wake, lakini ili kuweza kuondoka katika hila za Shetani ni lazima ukubali kubadilika
Ni mara nyingi sana tunajikuta tukisema sentensi hii kwa nini Kwa nini Mimi Mungu? (Why me Lord) huja baada ya kila jambo/mambo kwenda kombo lakini hiyo haimaanishi Mungu amekuacha
Ukikubali kubadilika kwa kujua kweli nayo kweli ikakuweka huru hata historia yako hubadilika, unakuwa mtu mpya na unaanza kutembea katika viwango vingine
Hakuna mtu wa kumlaumu juu ya changamoto na hali ngumu ya maisha unayoipitia isipokuwa wewe mwenyewe, kwa sababu Mungu amekupa uwezo wa kutatua kila changamoto au jaribu unalolipitia 1Kor 10:13 "Jaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita muwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya mlango wa kutokea, ili muweze kustahimili
Kila jambo baya ni jaribu haupaswi kukaa katika shida kwa muda mrefu kwa sababu kunao mlango wa kutokea, inabidi uwe tayari kupambana mpaka uondokane na changamoto unayopitia kwa sababu ni lazima Mungu afanye mlango wa kutokea
Tatizo la watu wengi hawapo tayari kunyenyekea kwa Mungu, kumuomba Mungu vya kutosha na kujifunza neno la Mungu ili kuweza kuliondoa jaribu wanalopitia, na kila mtu anayeshinda majaribu anainuliwa
Mlango wa majiribu ndio mlango wa kuinuliwa Yakobo 1:12 "Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaandalia wampendaao , ni dhahiri kwamba taji imeandaliwa kwa wale ambao wanayashinda majaribu tuu na siyo anayeyakimbia
Kubadilika ni kumjua Mungu na kuutafuta ufalme wake na haya mengine huwa tunazidishiwa, Math 6:33 "Utafuteni kwanza ufalme wa mbinguni na haki yake na haya mengine yote mtazidishiwa, unapoupeleka ufalme wa Mungu mbele na mambo yako hupelekwa mbele
Hatutangulizi matatizo yetu kwa BWANA kabla ya kuupeleka ufalme wake mbele, tunafanya yale yaliyo mapenzi yake katika Kristo Yesu ndipo tunapoweza kumtwika fadhaa zetu naye akatuokoa pasipo wasiwasi
Kubadilika ni kujifunza mambo mapya yanayokujenga kiimani, kiakili na kiroho lakini hatujifunzi mambo mapya kwa ajili ya kujifurahisha bali kwa ajili ya kuyafanyia kazi na kuweza kuona matokeo yake katika maisha yetu
Kubadilika ni kuambatana na watu ambao wanauelekeo sawa na ule unaouendea katika maisha, wengi wanaitwa matapeli, wazinzi, wahuni na misheni town kutokana na watu wanaongozana nao, ukiongozana na walevi 5 mlevi wa sita atakuwa wewe
Uzuri wa kubadilika ni huu, ukibadilika kila kitu hubadilika hadi watu waliokuwa wanakuchukia watakupenda, vitu vilivyokuwa vigumu vinakuwa vyepesi, changamoto zilizokuwa zinakusumbua zinaondoka, majaribu yanageuka mtaji kwako na unakuwa na pambazuko jipya
Tubadilike sababu ndio njia pekee ya kumjua Mungu na kuishi katika mpango wake, ndiyo njia pekee ya kukaribisha uwepo wa Mungu maishani mwako, ndio njia ya kuwa ushuhuda kwa wengine na mimi ni sehemu ya mabadiliko ninayotaka kuyaona
Kumbuka huwezi kubadilika kama hautaki kubadilika, kubadilika ni kumkubali Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, leo anasema na wewe katika ujumbe huu usiufanye moyo wako kuwa mgumu bali kubali naye ataweka makao ndani yako
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe
SALA YA TOBA
Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa
Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani
Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.
Kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana
Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana