KILA JAMBO LINA WAKATI WAKE - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Wednesday, July 25, 2018

KILA JAMBO LINA WAKATI WAKE

Baba Mwl Pallangyo na Co-founder MT Sialove Lukumay
Maisha yetu yana vipindi tofauti ambavyo Mungu aliviweka kwa sababu maalumu, vipindi hivi ndivyo vinatuandaa kwa ajili ya kusudi kubwa ambalo Mungu ametuandalia na vipindi hivi havitakaa vikome kwenye maisha yetu Mwanzo 8:22 " Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa joto, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku havitakoma


Vipindi hivi huwa vipo kwa kila mtu, watu wengi huwa wanaangalia watu ambao wamefanikiwa katika kitu fulani lakini huwa hawataki kuchunguza au kuwauliza ni vipindi gani walipitia kabla ya kufika hapo walipo, na siri ya mafanikio ya mtu ni kile alichokifanya katika nyakati ngumu na akafanikiwa

Kama haukusoma makala ya jana ya neno la Mungu, tuukomboe wakati⇒⇒⇒ BOFYA HAPA KUISOMA YOTE


Kabla Yusufu hajawa waziri mkuu katika ardhi ya ugenini alikuwa ni mtumwa tena aliyesingiziwa kesi ya ubakaji, ni kosa kumuongelea Yusufu katika uwaziri wake na kusahau kwamba alikuwa mtumwa, mfungwa na mtu ambaye alichukiwa na ndugu zake wote katika kipindi hiki Yusufu alikuwa anapitia kipindi cha usiku ambacho kilikuwa kinamuandaa kwa utukufu ambao Mungu amemuandalia


Mchana huwa haufuati mchana bali usiku na ni muhimu kuweza kutofautisha vipindi ambavyo tunapitia hapa duniani ili kuweza kulifikia kusudi ambalo Mungu ametuwekea wengi wanapopitia vipindi hivi kwa akili zao hufikiri Mungu kawasahau na hivyo hukata tamaa Wagalatia 6:9 "Tena tusichoke kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozima roho


Kuna wakati wa kulia, na wakati wa kucheka, wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna, wakati wa kuchekwa
na kuonekana hujui unachokifanya wala unakoelekea na wakati wa kupongezwa na kusifiwa kwa ulichokipata, vipindi hivi ndio vinafanya safari ya maisha kuvutia na kuwa na maana kwa kila mmoja wetu


Lakini kikubwa katika nyakati hizi zote ni kwamba unapaswa kufahamu wakati uliopo na ni nini unapaswa kukifanya wakati huo, neno la Mungu ambalo ni taa na mwanga wa maisha yetu ndilo linalotuongoza kuweza kujua tupo kipindi gani na ni hatua gani ambazo tunapaswa kuziendea


Ukishindwa kufahamu wakati uliopo itakuwia vigumu kujua unapaswa kufanya nini na wapi na pia unaweza kukata tamaa na kujidharau, ukiwa hapa duniani hupaswi kulewa sifa au kujisahau kwamba wewe ni binadamu na unaweza kufanya makosa kama watu wengine


Kuna mambo mengi ambayo huwa tunayafanya na tunaona ni sahihi mbele ya macho yetu lakini mwisho wako huwa ni majuto, Mithali 14:12 I"ko njia mabayo ionekanayo kuwa ni sawa machoni kwa mtu, lakini mwisho wake ni njia za mauti


Hii inatulazimisha tujisogeze kwenye uwepo wa Mungu kila wakati hata kama tumefanikiwa, mtu ambaye amefanikiwa katika eneo fulani ili kuyalinda na kuyaongeza mafanikio yake anamuhitaji Mungu zaidi Zab 1:3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji, uzao matunda yake kwa majira yake, wala jani lake halinyauki


Mafanikio huweza kugeuka na kuwa umasikini baada ya muda kama hutaimarisha mahusiano yako na Mungu, kumbuka kama ulipata ulichonacho kwa kumuomba Mungu au kwa neema ya Mungu ili kukidumisha kisinyauke hauna budi kuendelea kumuomba na kujisogeza karibu naye kila wakati


Hili linapotokea hata kama ulikuwa umefanikiwa na ghafla mambo yakaenda mrama bado una nafasi tena ya kurudi ulipokuwa, changamoto wanayokutana nayo Wakristo wengi huwa wanakuwa wagumu kujirudi na hapo ndipo shetani huzidi kujizolea utukufu katika matatizo wanayopitia


Moja ya nyakati ambazo utapitia kwenye maisha ni KIPINDI CHA USIKU



Hiki ni kipindi ambacho unatumia sana muda wako kupangilia mambo yako, ni kipindi ambacho kuna giza totoro lakini ndicho kipindi cha ubunifu, kuwa na ndoto na hakuna anayejua ulichonacho lakini wewe unaamini una kitu


Ni kipindi ambacho wakiwa wamelala wewe unasoma na kujifunza mambo mapya ukiamini kwamba kwa kufanya hivi mambo yako yatabadilika mbeleni


Ni kipindi ambacho watu wengi hawakuelewi kile unachowaambia na wanaona kama unapoteza muda na hujui ni wapi unapaswa kuenda


Hiki pia ni kipindi ambacho unapaswa kufanya maamuzi kuhusiana na jambo ambalo unalitaka katika maisha yako na kuwa tayari kupambana kulifanya mpaka tone lako la mwisho


Inawezekana unapitia kipindi hiki habari njema ni kwamba hakuna marefu yasiyo na mwisho, wasikukatishe tamaa kama ulikuwa mtoto mchanga huwezi kukaa, sasa unatembea na kuweza kufanya mambo yako peke yako kuna uwezekano wa kupita kipindi hiki


Hakuna gumu lisilo na wepesi au njia ya kulitatua na kulilegeza. Ni lazima tuu kuna njia ya kupita na kutokea kipindi kingine


Watu wengi wapo katika kipindi hiki, lakini hata hawafahamu kama ndio kipindi wanachopitia, unapomruhusu Mungu ashughulikie mambo yako unajiweka katika nafasi ya kufahamu kipindi ulichopo na kuanza kupanga mikakati ya kuhamia kipindi kingine kwenye maisha yako



Mungu ndiye anayetupitisha kutoka kipindi kimoja kwenda kingine ni vigumu sana kufanikiwa katika vipindi hivi kama hujaimarisha mahusiano yako na Mungu ndio maana kama hujampokea Yesu Kristo unakosa furaha na amani, hakuna maisha mabaya kama kuishi pasipo kumkubali Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako


Kama bado hujampokea leo anabisha hodi mlangoni pako, kumbuka kwamba yule ambaye atakayefungua mlango ndio ataingia na kufanya makao ndani yake


SALA YA TOBA


Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa

Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana


Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana