NGUVU YA ULIMI-VIDEO 2 - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, February 6, 2018

NGUVU YA ULIMI-VIDEO 2

Ulimi ni kiungo kidogo sana lakini kinaweza kukuletea faida au madhara
kulingana na namna ambayo utakuwa unakitumia, wengine wamekuwa wanatumia ndimi zao kulaani wengine na kujitamkia laana na maneno ya kukatisha tamaa, lakini wapo ambao wanatambua matumizi ya ndimi zao wanazitumia kubariki na kujitamkia maneno ya baraka

Kuangalia video ya kipindi cha pili cha Mwanamke Thamani cha Nguvu ya Ulimi angalia video iliyopo juu kabisa au GUSA HAPA

1Petro 3:10 "Kwa maana, atakaye kupenda maisha, na kuona siku njema, auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila"

Kiuhalisia siyo matukio au hali ya hewa ndiyo inayoharibu siku bali ni namna ambavyo tunatumia ndimi zetu na midomo yetu kuongelea kilichotokea au kitakachotokea katika siku husika

Kila kitu kina uzuri wake lakini ukikaa kutafuta ubaya badala ya wema na kutumia ulimi na mdomo wako kuongelea hayo basi hata siku yako itakuwa mbaya na iliyokosa baraka

Biashara, kazi, mahusiano, udugu hujengwa kwa ulimi, namna ambayo unaongea na wateja wako, unavyoongea na familia yako, mkuu wako wa kazi na watendakazi  wenzio ndio itaamua ufanikiwe au ubomoe unachokifanya

Binadamu tumekuwa tunaongea maneno mabaya, maovu ya kukatishana tamaa na kujiambia kwamba hatuwezi kufika sehemu fulani au hatuwezi kufanikisha suala fulani lakini tunasahau kwamba kile ambacho tunakikiri kwa ulimi na midomo yetu ndicho ambacho hutokea

Kama haukusoma makala iliyopita ya ULE MSHAWASHA UTAKAOTOKEA GUSA HAPA

Neno ni sawa na kiapo, ndiyo maana viongozi huapizwa kwa maneno na kwa mujibu wa dini zao, Amini Amini nakuambia hakuna sababu yeyote ya kusema jambo ambalo haulitaki maishani mwako

Kama unataka utajiri usikae ukae chini na kukiri wewe ni masikini na huwezi kufanikiwa, kama unataka kuwa na mahusiano mazuri na watu usikae useme fulani anaringa na hataki kushirikiana na watu, kama unataka mafanikio kielimu usikae useme nitafeli somo fulani au mimi ni dhaifu sehemu fulani, kiri na tamka tena kwa ujasiri kitu ambacho unakihitaji pekee 

Hii ndiyo maana Biblia ikasema katika Waefeso 4:29 "Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia"

Una kila sababu ya kutamkia watu habari njema na za kufurahisha, una kila sababu za kuwabariki watu kwa kile ambacho Mungu amekupa, kiuhalisia hakuna mtu mbaya hata mmoja duniani kila mtu ana uzuri wake kabla ya kuangalia ubaya tafuta uzuri na utamke

Kumbuka kabla ya ombi lolote huanza shukurani na pongezi haijalishi hali ilikuwaje ndipo mengine hufuata baada ya kushukuru na kukipongeza kile kilichopo

Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana