Moyo wa subira ni ule uwezo wa kuwa na uvumilivu, mpaka jambo fulani litakapotukia pasipo kukata tamaa wala kupoteza matumaini
Watu wengi wakishuhudiwa kitu fulani kitatukia hufikiri kesho yake ndio kitatukia au wiki ijayo huwa na haraka na pupa katika kila suala lao
Ni bora kwenda taratibu kuliko kuharakia lile ambalo Mungu amekuandalia, maana pupa huwaingiza watu kwenye majaribu na changamoto ambazo hawakupaswa kuingia
Yesu alijua kabisa tangu amezaliwa kwamba amekuja hubiri Injili, wakati fulani kwenye Biblia akiwa na miaka 12 alikwenda hekaluni na kuongea maneno ya hekima yaliyowaacha viongozi wa dini na mshangao
Japokuwa alifahamu kusudi lake hakukurupuka na kulianza kabla ya wakati bali alikuwa na subira hata alipofikisha miaka 30 ndio akaanza kuhubiri Injili
Katika makala yetu ya jana tulisema kuna mambo ya kuzingatia mwaka huu kama hukuisoma gusa hapa
Moja ya jambo tuliloongelea ni kutohairisha mambo lakini kabla ya kuanza mchakato wa kile unachotaka kufanya mshirikishe Mungu suala lako
Watu wengi hurukia vitu pasipo kumshirikisha Mungu na mara nyingi hufika katikati na kugundua walikosea tangu awali
Wengine kwa mioyo migumu hukataa kugeuza gari (kubadili uelekeo), wengine huwa tayari kuanza tena upya kusoma makala ya geuza gari inapobidi gusa hapa
Mtu mwenye subira pale anapopata ufunuo na anajua huu umetoka kwa Mungu huwa na uhakika kwamba utatimia
Moyo wenye subira huonesha ukomavu wa kiimani, ndoa yenye subira ni ile inayomtumaini Mungu na kuamini neno lake hata kama kuna miaka 5 imepita pasipo kupata mtoto
Wapo watu ambao wameoneshwa namna watakavyokuwa wakuu na wanafanya makosa kwa kutumia akili zao kujishawishi kwamba itawachukua muda mrefu sana kufikia ukuu wao
Leo nataka kuwakumbusha hata kama itakuchukua miaka 40 kutimiza ulichooneshwa haupaswi kuogopa wala kukosa subira
Hii ni kwa sababu muda utapita tuu uamini au usiamini kwa sababu hivyo ndivyo ilivyo jambo la msingi ni kuwa na mahusiano mazuri na Mungu
Wote tunamkumbuka Yusufu akiwa kijana kabisa Mungu alimuonesha katika ndoto namna atakavyokuja kuwa mkuu na kuwatawala ndugu zake
Baada ya kuelezea ndoto hii ndugu zake walijawa na wivu na kupanga njama za kumuuwa, lakini baadae nduguye mmoja aliwashawishi wamuuze utumwani
Jaribu kufikiri Mungu kakuonesha ukuu ulioko mbele yako na baada ya kuutamka umegeuka kuwa mtumwa, baada ya hapo tunakumbuka aliswekwa jela
Na kule alitabiria maakida wa Farao ndoto mara ya kwanza na mwanzo 40:14 baada ya kuwatafsiria aliomba ombi " Unikumbuke , unifanyie fadhili, ukanitaje kwa Farao na kunitoa katika nyumba hii"
Tizama kilichotokea, maakida hawa yalitukia mema kama alivyowatafsiria na walipata nyadhifa zao lakini kamwe hawakumkumbuka Yusufu
Kama nilivyokwisha kusema mtu anayemwamini Mungu ana subira hajali itamchukua muda gani kufanikisha kile ambacho Mungu kamuambia
Wengi wetu tungekata tamaa kwa sababu tungesema tumemtumikia Mungu vya kutosha, tumetabiri ndoto na zimetukia na bado tuu tunakaa gerezani
Tungehoji maswali kama huyu Mungu yuko wapi? Je ndoto aliyonionesha ilikuwa ya kweli au siyo? Kwa nini ananiacha nateseka kiasi hiki natenda mema lakini nalipwa mabaya
Lakini siyo Yusufu alionesha subira huku akimtumaini Mungu kwamba atamfanikisha hata kama haikuwa wakati ule
Wakati ulifika Farao akaota ndoto na walipotafuta mtu kote wa kutafsiri ndoto ile hakupatikana isipokuwa mtu mmoja mwenye subira na aliyemwamini Mungu
Kumtumikia Mungu kunalipa hapa Yusufu alichangamkia tenda chap chap na kutokea mlango huo alikuwa waziri mkuu wa Misri umeona sasa?
Angekosa subira na kumlaumu Mungu kwa wale maakida wa mwanzo kutomkumbuka angepoteza hii nafasi ya ukuu na heshima
Ukiwa kama Mkristo subira ni lazima siyo ombi, haupaswi kukurupukia mambo, Mungu amekupangia mambo mema kuliko unavyofikiri kwa akili yako ya kibinadamu
Kumbuka Yusufu aliyekuwa anadharaulika na kuonekana hafai Mungu alifanya suala lake kuwa la tofauti, wewe unawasiwasi wa nini?
Waache wakucheke, wakudharau, waambiane mabaya yako lakini kama yanakupata yote haya ukimtumikia Mungu wa kweli na kutokea moyoni....
Yafaa nini kuhangaikia dunia na mambo yake yote?, Kuna siku watauona wema wa Mungu maishani mwako hapo ndipo watajua subira, tumaini, upendo na imani yako havikuwa vya bure
Mwanamke Thamani
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana