Namshukuru Mungu aliyetulinda mwaka uliopita hata mwaka huu na tumeweza kufika hii leo, sifa na shukrani ziende kwake
Kwa kawaida mwaka mpya huja na mambo mapya, mipango mipya, malengo mapya, kujitoa upya na mipenyo mipya
Hatuhitaji wingu la mwaka jana lituongoze mwaka huu, kama mwaka jana ulikuwa na baraka double double mwaka huu zitazidishwa mara nne nne
Kila unapovuka mwaka mmoja kwenda mwingine na baraka zako hubadilika, tunahitaji wingu jipya na mafunuo mapya ya kumalizia kazi zetu mwaka huu
Mana inapositishwa ni lazima tujifunze namna ya kujitengenezea chakula na tujue kwamba tuna jukumu la kufanya kazi mbele yetu
Mwaka mpya unakuja na maandalizi mapya, Yohana Mbatizaji alimwandalia Yesu njia kwa ajili ya kazi yake Marko 1:2 "Namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako kuitengeneza njia yako"
Maandalizi yetu mwanzo huu wa mwaka ni pamoja na kupanga malengo yetu na namna ambayo tutayafanikisha (njia)
Kumbuka malengo yamegawanyika katika nyanja zifuatazo, Kiroho, Kiuchumi, Afya, Kitaaluma, Familia na Mahusiano
Ni vyema kuyapangia maeneo yote haya malengo mwanzo huu wa mwaka, kisha fanya kama wana wa Israel yabandike sehemu utakayoweza kuyasoma mara kwa mara ili kujikumbusha
Jambo jingine muhimu ni kuweka alama sehemu uliyopo mwanzo huu wa mwaka hii itakupa sababu ya kumshukuru Mungu kwa kila hatua ambayo utakayokuwa unavuka
Wakati mwingine hatujui wala hatuthamini tulipofikia kwa sababu hatukuweka alama tulipoanzia ndio maana ni vema kuwa makini katika hili
Tutakapomaliza robo ya kwanza ya mwaka unaweza kupima umefikia wapi na kujua ni sehemu gani ya kuwekea nguvu zaidi ili kusogea mbele
Kama ilivyokwisha kusemwa mwaka huu ni mwaka wa baraka sana kutakuwa na mafanikio mengi sana tutaona huduma nyingi zikistawi, biashara mpya, kazi na mipenyo mipya
Unahitaji kujiungamanisha na baraka za mwaka huu hakikisha unakuwa makini katika mambo yafuatayo:,
- Kuwa makini sana na matumizi ya muda wako Waefeso 5: 15-16 "Enenda kama mwenye hekima, ukiukomboa wakati maana hizi ni zama za uovu" usikubali kuenenda bila hekima, tumia muda wako vyema
Kumbuka utapaswa kutoa hesabu ya muda uliopewa siku moja, utasema nini mbele yake siku ile
Tunaitaka kesho njema na yenye utukufu tutaongea nini kesho kama leo yetu tunaitumia vibaya na hatujali muda?
- Kuwa makini na marafiki zako, huwezi kuchagua jirani ila rafiki unaweza, huwezi kuchagua ndugu ila urafiki ni uchaguzi kamwe usidanganyike urafiki mbaya huharibu hatima za watu
Mwaka huu pukutisha marafiki wote ambao hawakupeleki unakotaka kwenda Yesu alichagua mtu mmoja mmoja katika kila kabila la Israeli wewe ni nani unataka kuwa rafiki wa kila mtu
- Usikae barazani pa mzaha, kimbia na kaa mbali na watu wenye mzaha Roho Mtakatifu na Malaika hawafahamu utani kila kitu wanakuhesabia kama ulivyosema, mtu anaedharau uongozi uliopo, anayelaumu, anayetukana epuka kukaa sehemu hizo na kuongelea mada hizo
- Kama umepanga kufanya jambo usihairishe, kuwa kama Ibrahimu unapokea taarifa leo kutoka kwa Mungu kesho asubuhi safari inaanza huu ni mwaka wa kazi zaidi na utashuhudia mabadiliko makubwa
Usifanye tuu kama utakuwa umeshuhudiwa moyoni kwamba uache kinyume na hapo piga kazi, kama umeajiriwa fanya kazi mpaka bosi wako ashangae
Ni mwaka mpya na Pambazuko jipya kumbuka huwezi kupata zaidi ya vile ulivyo, Mungu akubariki uwe na imani na uyaweze yote katika yeye akutiaye nguvu
Mwanamke Thamani!
No comments:
Post a Comment
Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana